3266; Kwa nini huna imani?

Rafiki yangu mpendwa,
Hivi karibuni kuna mtu aliniandikia akiomba ushauri ni biashara gani ya mtaji mdogo anayoweza kuifanya na ikampa faida kubwa?

Kama kawaida yangu, huwa sikimbilii kumwambia mtu nini afanye, bali namuuliza kwanza maswali ili kumwelewa kwa kina.
Na kupitia kumuuliza maswali mtu huyo niligundua tayari kuna biashara anafanya.

Na hapo ndipo nilipomuuliza swali moja muhimu sana, ambalo pia nataka kukuuliza wewe hapa. Nilimuuliza; “Kwa nini unatafuta biashara nyingine ya kufanya yenye faida kubwa badala ya kukuza hiyo uliyonayo sasa?”

Hili ni swali ambalo nakuuliza na wewe rafiki yangu, ambaye kuna biashara tayari unaifanya sasa, lakini unatafuta biashara nyingine ya kufanya.
Au unafanya biashara zaidi ya moja kwa sasa na zote zinakutegemea wewe moja kwa moja.

Ila kwako nitalirahisisha zaidi hilo swali, ili likusaidie kufanya maamuzi.
Swali ninalokuuliza wewe rafiki yangu ni; “Kwa nini huna imani?”

Kwa nini huna imani kwamba biashara unayofanya sasa inaweza kukupa mafanikio makubwa mpaka unatafuta nyingine ya kufanya?

Kwa nini huna imani ya kuweka juhudi zako zote kwenye biashara moja mpaka ifanikiwe kabla ya kutawanya kwenye biashara nyingi ambazo zinakutegemea?

Rafiki, kadiri unavyohangaika na mambo mengi, unaonyesha jinsi ulivyokosa imani kwenye jambo lolote moja.

Najua unachofikiria ni unahitaji kuwa na vyanzo vingi vya kipato. Na utaonyesha kwa mifano jinsi ambavyo wale wenye utajiri mkubwa wana vyanzo vingi vya kipato.

Kitu ambacho utakuwa hujui, au kama unajua basi unajisahaulisha ni kwamba hao wenye utajiri mkubwa unaowaona sasa wana vyanzo vingi vya kipato hawakuanza vyote kwa pamoja.
Badala yake walianza na chanzo kimoja, wakakifanyia kazi kwa umakini mkubwa mpaka kikawa cha uhakika na kisichowategemea. Ndipo wakaenda kwenye vyanzo vingine.

Turudi kwako rafiki yangu, kwenye swali kuu la ukurasa huu wa leo; Kwa nini huna imani kwenye hicho unachofanya sasa mpaka unatamani kufanya vitu vingine au unafanya vingi kwa pamoja?
Karibu ushirikishe majibu yako hapo chini.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe