3273; Usifanye mambo kuwa magumu zaidi.

Rafiki yangu mpendwa,
Nimekuwa nasema maisha tayari ni magumu, lakini watu huwa wanayaongezea ugumu kwa yale wanayokuwa wanayafanya.

Unakuta watu wanahangaika na mambo ambayo hayana tija wala mchango kwenye kila wanachotaka.
Ila wanafanya kwa sababu ndiyo wamezoea kufanya au ndiyo kila mtu anafanya.

Kuepuka kuyafanya maisha kuwa magumu zaidi ya ambavyo tayari yapo, zingatia yafuatayo.

1. Angalia yale yanayofanywa na wengi na yaepuke.

Wengi hawafanikiwi kwa sababu wanafanya mambo kwa mazoea na kwa kufuata mkumbo.
Wanafanya kile kinachofanywa na kila mtu kwa sababu hata wakikosea, hawataonekana ni wa ajabu.
Kufanya kile kinachofanywa na wengi kwa sababu tu ni rahisi, unakuwa umechagua kuyafanya maisha kuwa magumu zaidi ya yanavyopaswa kuwa.
Ni rahisi zaidi kwako kufanya tofauti kuliko kufuata mkumbo.

2. Angalia yale ambayo jamii inakulazimisha uyafanye.

Kuna ambayo wewe mwenyewe unachagua kuiga kufanya, halafu kuna ambayo jamii inayokuzunguka inakulazimisha ufanye.
Kwa kutaka kuwaridhisha na kuwafurahisha wengine, unayafanya.
Kwa haraka unaweza kuona ni rahisi kufanya yale jamii inakutaka ufanye, lakini ni kuyafanya maisha yako kuwa magumu zaidi.
Kwa sababu unaweza kudhani unawaridhisha wengine, lakini kama wewe mwenyewe huridhiki, jua hakuna unayemridhisha.
Yale ambayo jamii inakulazimisha ufanye, siyo kwa sababu yana manufaa kwako, bali kwa sababu yanainufaisha jamii hata kama kwako yana madhara.
Chagua kujisikiliza wewe mwenyewe badala ya kuburuzwa na jamii inayokuzunguka.

3. Jihoji wewe mwenyewe kwa kila unachofanya.

Wengi huwa wanayaendesha maisha yao kwa kufanya leo kile walichofanya jana.
Hata kama kilichofanya kazi jana leo hakifanyi kazi tena, watu bado huwa wanaendelea kukifanya.
Ili kuondokana na hilo, unapaswa kujihoji wewe mwenyewe kwa kila unachofanya.
Kila unapoanza kufanya kitu, jiulize kwa nini unakifanya? Je hicho ndiyo kitu muhimu zaidi kwako kufanya kuliko vitu vingine?
Na je, kama ungekuwa unaanza upya, bado ungekifanya kitu hicho? Kwa namna ambavyo umekuwa unafanya?
Hakuna mtu ambaye anafanya makosa makubwa kwa siku moja. Mara nyingi mtu anayakusanya makosa kidogo kidogo mpaka yanafikia hatua ambayo ni makubwa na yenye madhara.
Unapojihoji kwenye kila jambo unalofanya ni rahisi kuona wapi penye makosa na kuyarekebisha kabla hayajawa na madhara makubwa.

Kitu kikubwa sana ambacho tumekiona kwenye maeneo hayo makubwa matatu ni kile unachoona rahisi kufanya, ndiyo kinazidisha ugumu wa maisha.
Hivyo tunaweza kuhitimisha kwa kusema; KUTAFUTA URAHISI NDIYO KUNAYAFANYA MAISHA KUWA MAGUMU ZAIDI.
Kama utaacha kukimbizana na urahisi na kufanya yale yaliyo sahihi kwako, utaweza kufanya makubwa kadiri unavyotaka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe