Rafiki yangu mpendwa,

Tunapowaangalia watu walioweza kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yao, halafu tukajiangalia sisi wenyewe, tunaona kuna namna watu hao walistahili mafanikio yao kuliko sisi.

Japo tunaweza kuamini kabisa hilo, lakini sivyo uhalisia ulivyo. Kwa bahati mbaya sana huwa tunawajua wale waliofanikiwa baada ya kuwa wamefanikiwa. Sehemu kubwa ya kule walikopita mpaka wakafanikiwa huwa haionekani.

Na kwa bahati mbaya sana, siyo watu wote huwa wapo tayari kuweka wazi yale yote ambayo wamepitia kwenye safari ya maisha yao mpaka kufanikiwa. Na hilo limekuwa linapelekea wengi ambao hawajafanikiwa kutokupata uhalisia wa safari ya mafanikio.

Tunapokutana na watu wachache ambao wameweza kujenga mafanikio makubwa, licha ya kuanzia kwenye magumu na wakawa tayari kushirikisha yote ambayo wamepitia, inakua ni fursa kubwa sana kwetu kujifunza.

Hebu fikiria mtu aliyefanikiwa sana, kiasi cha kuwa bilionea, anakushirikisha kwamba kwenye safari ya maisha yake amewahi kubakwa, tena siyo mara moja. Hayo ni mapito ambayo wengi hutaka kuyafukia kabisa, hasa baada ya kufanikiwa.

Lakini hivyo sivyo ilivyo kwa mwanamama Oprah Winfrey, ambaye ni mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa duniani, akiwa na mafanikio na utajiri mkubwa. Ni mmoja wa mabilionea duniani, thamani ya utajiri wake ikikadiriwa kuwa dola bilioni 2.8 mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka 2023.

Unaposikia mtu ni bilionea, ni mafanikio ya juu sana, kifedha, ushawishi na mengine. Lakini vipi ukisikia mtu ambaye ni bilionea, kuna kipindi cha maisha yake ambapo alikosa kabisa nguo za kuvaa na kulazimika kuvaa magunia?

Hayo ni maisha ambayo Oprah aliyapitia, baada ya kuzaliwa na mama ambaye alikuwa ni binti, akalelewa na bibi ambaye alikuwa masikini. Kwa miaka sita ya kwanza ya maisha yake aliishi kwenye umasikini wa kutumbukia.

Lakini anaeleza pia miaka hiyo sita ndiyo iliyojenga msingi wa mafanikio yake ya baadaye kama mtangazaji na mwendeshaji wa kipindi cha TV kilichokuwa na wafuatiliaji wengi duniani.

Katika kipindi hicho, bibi yake alikuwa anampeleka kanisani na kumtaka asome na kukariri mistari ya biblia. Alifanya hivyo na akawa anaisema mistari hiyo ya biblia aliyoikariri. Hilo lilimfanya watu waanze kumwita mhubiri tangu akiwa mtoto.

Baadaye alikwenda kuishi na mama yake, ambaye kutokana na umasikini alilazimika kufanya kazi muda mwingi na hivyo hakuwa anapata muda kabisa na mama yake. Hilo lilipelekea malezi yake kuwa magumu na kujikuta kwenye mazingira hatarishi yaliyopelekea kubakwa zaidi ya mara moja, tena na watu wa karibu.

Alipata ujauzito akiwa na umri mdogo wa miaka 14 na kujifungua mtoto ambaye hakuwa ametimia. Mtoto huyo alifariki dunia siku chache baada ya kuzaliwa.

SOMA; 3273; Usifanye mambo kuwa magumu zaidi.

Mambo yalianza kubadilika kwa Oprah baada ya kuanza kuishi na aliyeambiwa ni baba yake. Alimsisitiza umuhimu wa elimu na Oprah alizingatia. Akiwa shule alipata nafasi ya kutangaza kwenye kituo kidogo cha redio. Aliifanya kazi hiyo kwa kujituma na shauku kubwa. Hilo lilipelekea azidi kupewa nafasi kubwa zaidi kwenye utangazaji. Kwa kila nafasi aliyopewa, alifanya vizuri sana na kupata wafuasi wengi.

Hilo ndiyo lilipelekea kuweza kuanzisha kipindi chake cha TV cha mahojiano, ambapo aliweza kuwahoji watu wa kila kada. Kuanzia watu wa kawaida ambao walikuwa wanapitia changamoto mbalimbali mpaka watu wenye ushawishi mkubwa.

Kipindi chake kiliruka kwa zaidi ya miaka 20 na kilimpa mafanikio makubwa sana kiushawishi na kifedha. Aliweza kuanzisha kampuni za habari, kuanzia uzalishaji na usambazaji wa maudhui mbalimbali. Pia aliweza kushirikiana na watu wengine wenye ushawishi mkubwa kupiga hatua kubwa.

Mpaka sasa Oprah ni mmoja wa watu wenye mafanikio makubwa, licha ya kuhitimisha kipindi chake maarufu, bado ameendelea kubaki kwenye ulimwengu wa biashara kwa eneo la habari.

Lakini pia amekuwa mmoja wa watoa misaada wakubwa kwa watu wenye uhitaji, kuanzia kufadhili masomo mpaka kutoa usaidizi wa moja kwa moja kwa wale wenye changamoto.

Oprah amekuwa wazi kwenye kueleza mapito yake, ambayo yalimuumiza sana na kuonyesha kamba kilichomfanya afanikiwe sana ni yale aliyopitia. Badala ya kuyachukulia kama kikwazo, yeye aliamua yawe ndiyo kichocheo kwake.

Alikuwa na kila sababu ya kujiona hafai kwa yale aliyopitia, manyanyaso, kubakwa, kuzalishwa akiwa mtoto na mengine. Lakini hakukubali hayo yawe kikwazo, alipambana kufanikiwa.

Hata baada ya Oprah kufanikiwa, amekuwa anahakikisha wote wanaopitia magumu kama aliyopitia yeye hawakati tamaa, badala yake wanapambana kubadili hali zao na kupata ushindi. Hilo ndiyo limekuwa kusudi la maisha yake, ambalo limemwezesha kubadili maisha ya wengi na kupata mafanikio makubwa.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini tumekuwa na mjadala mzuri kuhusu maisha ya Oprah na yale tunayojifunza na kufanyia kazi. Karibu ujifunze zaidi kwenye kipindi hicho ili na wewe uweze kuyaboresha maisha yako. Fungua hapo chini kujifunza.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.