3282; Unapojikwamisha mwenyewe.

Rafiki yangu mpendwa,
Kuna maeneo mengi huwa tunakwama kwenye maisha kwa sababu ya watu ambao tunajihusisha nao.

Huwa ni rahisi kuona kwamba watu hao ndiyo wanaotukwamisha.
Lakini ukweli ni kwamba sisi wenyewe ndiyo tunaojikwamisha.

Watu wapo kama walivyo na wataendelea kuwa walivyo bila ya kujali wewe unataka nini.
Kama kwa watu kuwa walivyo inakukwamisha wewe, tatizo siyo wao, tatizo ni wewe mwenyewe.

Watu wengi ulionao kwenye maisha yako ambao unaona wanakukwamisha, hawakupaswa kuwepo kabisa kwenye maisha yako.
Ulipaswa kuwa ulishaachana nao muda mrefu sana.
Lakini kwa uzembe fulani uliofanya, umejikuta ndiyo unaowategemea na hivyo huwezi kuwaacha mara moja.

Una wafanyakazi ambao siyo waaminifu, hawajitumi na wanakuwa mzigo kwenye kila kitu. Ni wazi hao hukupaswa kuwa nao kabisa. Ulipaswa kuwa ulishawafukuza kazi muda mrefu sana. Lakini kwa sababu huna wengine wa kushika nafasi zao, inabidi tu uendelee kubaki nao.
Na kwa sababu hakuna juhudi za makusudi unazofanya za kupata mbadala, unabaki na hao kwa muda mrefu. Kitu ambacho kinaendelea kukukwamisha sana.

Hilo pia lipo kwa wateja. Umechagua kuingia kwenye biashara kwa sababu unataka uhuru wa muda, kipato na maisha kwa ujumla. Lakini umejikuta una wateja ambao hawajali unachouza, hawakulipi kwa wakati na pia hawafanyi manunuzi ya kutosha kupata kile unachotaka.
Unajikuta umekwama na biashara ambayo haikupi kile ulichotaka, lakini pia bado unaitegemea sana. Na hilo linakuwa limesababishwa na uzembe wako wa kutokuendelea kutengeneza wateja bora kila wakati.
Baada ya kupata wateja ulionao sasa, hujataka kujisumbua tena kutengeneza wateja wengine wengi zaidi.
Kazi yako kubwa kwenye biashara ni kila wakati kutengeneza wateja wapya ambao ni bora zaidi ya wale ulionao sasa.
Hilo linapaswa kuwa zoezi endelevu na ambalo halina mapumziko kama kweli unataka biashara itakayokupa kila unachotaka.

Tatizo la watu ni wako vile walivyo wao na siyo vile unavyotaka wawe.
Wengi wanapokuwa na uhitaji wa kitu ulichonacho, wataigiza kuwa vile unavyotaka. Lakini wakishapata wanachotaka, ndiyo wanakuwa halisi kwao, kitu ambacho kitakukwamisha sana.
Sasa kama utakuwa unawasubiri wabadilike, utajichelewesha sana.
Unachotakiwa ni kuendelea kutafuta watu wengine wengi zaidi, ili angalau kati ya hao wengi upate ambao ni sahihi kwao.

Ukiona umechukua muda mrefu bila ya kuingiza watu wapya kwenye biashara na maisha yako, jua siku zijazo utapitia kipindi kigumu sana.
Kwa sababu wale ulionao ambao unaona unaweza kuwategemea, watakukwamisha kwenye kipindi ambacho hukuwa unategemea.

Zoezi la kuingiza watu wapya kwenye biashara na maisha yako linapaswa kuwa endelevu, ambalo linafanyika mara zote, kwa msimamo bila kuacha.
Ni kufanya zoezi hilo kwa mwendelezo ndiyo itakupa wewe uhuru wa kuwa na maisha unayoyataka.
Ukizembea kufanya zoezi hili kwa uendelevu utalipa kwa kupitia mkwamo mkubwa kwenye kile unachofanya.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe