💯KCM2324059; Maana.

Tumejipata, Tunaachilia Breki.

#JumatanoYaUwajibikaji

Mwanamafanikio,

Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.

Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.

Fuata mwongozo huu ili kuwa na maisha ya mafanikio. 0678977007


💯 Neno la leo; Maana.

Leo ikiwa ni #JumatanoYaUwajibikaji tunaona jinsi aambavyo maana ya maisha inaanzia kwenye kuwajibika.

Hali ya maisha kwa zama hizi imekuwa bora sana kuliko kipindi kingine chochote hapa duniani.

Maradhi ambayo yalikuwa yanawaua wengi kwa sasa yana dawa.
Vita na mapigano mengi yamepungua.
Na hata vyakula, vimekuwa vingi, siyo wengi wanaokufa njaa kama kipindi cha nyuma.

Lakini pamoja na ubora huo mkubwa wa maisha, watu wengi bado hawaridhishwi wala kufurahishwa na maisha yao.
Hiyo ni kwa sababu maisha yao yanakuwa yamekosa maana.

Maisha ya wengi hapa duniani yamekuwa hayana tofauti na ya minyoo, wanaingia duniani, wanakula na kufa. Hakuna alama yoyote wanayoiacha.

Hilo linasababishwa na wengi kusukumwa na kuendesha maisha yao kutafuta raha na starehe.
Watu wanahangaika kufanya vile tu ambavyo vinawapa raha na starehe.
Lengo lao kuu linakuwa ni kupata furaha muda wote.

Hiyo ndiyo sababu ya watu kujikuta wanahangaika na mambo ambayo yanaweza kuwapa kuridhika kwa muda mfupi, lakini kwa muda mrefu yanawaacha wakiwa wanaona maisha yao hayana maana.

Maana ya maisha inapatikana kwenye uwajibikaji.
Ni pale mtu unapowajibika kwenye kitu fulani, ambacho kinakusukuma kutumia uwezo mkubwa ulio ndani yako ndiyo unakuwa na mchango mkubwa kwenye maisha.

Wajibu unakuondoa kwenye njia rahisi ya kukimbizana na raha na starehe na kukuweka kwenye njia ngumu yenye mchango kwa wengine.
Uwajibikaji unakuweka eneo ambalo huwezi kutoroka kirahisi.
Ni kwa njia hiyo ndiyo unakuwa na mchango wa kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora na hapo maisha yako kuwa na maana.

Angalia hata kwenye njia za kuingiza kipato.
Kuna njia nyingi za mkato, ambazo mtu anaweza kuingiza kipato bila kufanya kazi kubwa.
Lakini unapoyaangalia maisha ya wale wanaotumia njia hizo, unaona dhahiri jinsi yalivyokosa maana.
Kwani hata kipato wanachoingiza, huwa wanaishia kukitumia hovyo.

Lakini wale wanaoingiza kipato kwa shughuli inayowataka kuweka kazi ambayo ina mchango mzuri kwa wengine, pamoja na ugumu wa kazi hizo, huwa wanaridhika zaidi.
Na kipato hicho huwa wanakitumia vizuri na kinakuwa na mchango mzuri kwao.

Utaipata maana ya maisha yako kupitia kuwajibika kwa wengine kwenye vitu fulani.
Kama maisha yako yamekosa maana ni kwa sababu umekuwa mbinafsi, unafanya mambo kwa raha na starehe zako mwenyewe tu na hujali wengine wananufaikaje.

Wajibika kwa wengine na utaachilia breki ambazo zimekuwa zinakuzuia usipate mafanikio makubwa yaliyo ndani ya uwezo wako.

💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MJASIRIAMALI MJANJA na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.

Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu athari za wengine. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/12/27/3283

Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kuwajibika kwa wengine ili kutumia uwezo wako wa ndani kufanya makubwa zaidi.

Kocha.
💯