3284; Kuanza na kumaliza.

Rafiki yangu mpendwa,

Watu wamekuwa wanaanzisha vitu vingi kuliko ambavyo wanavimaliza au kuvikamilisha.
Hiyo ni kwa sababu kuanza ni rahisi kuliko kumaliza.

Japokuwa pia kuanza huwa kunaweza kuwa kugumu kwa baadhi ya watu, wale ambao tayari wana msukumo wa kufanya, huwa wanaanza bila shida.

Tatizo huwa linakuja kwenye kumaliza au kukamilisha. Ni wachache sana ambao wanafanikisha hilo. Na wachache hao ndiyo wanaoyapata mafanikio makubwa.

Watu wamekuwa rahisi kukimbilia kuanza vitu vingi kuliko wanavyomaliza kwa sababu ya maana isoyokuwa sahihi kwao ya mafanikio.

Kwa wengi, wanaona mafanikio ni wingi wa vitu walivyoanzisha.
Hivyo mtu anajisikia vizuri na kuona amefanikiwa pale anaposema ameanzisha biashara 5 au 10 na kadhalika.
Hawataenda mbele kuonyesha biashara hizo nyingi walizoanzisha zimeweza kufanyaje.

Unapokuja kuchunguza, unaona ni dhahiri mtu alianzisha biashara nyingi, lakini hakuna hata moja ambayo iliweza kufikia hatua ya kuweza kujiendesha yenyewe bila ya kumtegemea mwanzilishi.
Hicho ndiyo kipimo cha mafanikio na kukamilika kwa biashara.

Kama mtu angechagua kuachana na kuanzisha biashara nyingi, akapeleka nguvu zake zote kwenye biashara moja, angeweza kufikia hatua ya biashara hiyo kujiendesha yenyewe.

Lakini kwa sababu maana hiyo ya mafanikio haipo kabisa kwenye akili yake, haiwezi kufikiwa.

Kaa chini na jitathmini maana ya mafanikio kwako ni ipi. Wapi unaridhika na kujisikia vizuri?
Je ni kwenye kuanzisha vitu vipya? Au ni kwenye kukamilisha kila unachoanza?

Kama unaridhika zaidi kwenye kuanza vipya, jua wazi umeshaharibiwa na wengi ambao hawafanikiwi.
Fanya kazi ya kubadili hilo na pima mafanikio yako kwa yale uliyokamilisha.

Hivyo kwa chochote unachoanza, jiambie kabisa kukamilika kwake ni nini, kisha kaa nacho mpaka kikamilike.
Epuka tamaa na vishawishi vya kuanza kitu kipya, hasa pale unapokutana na magumu au changamoto kwenye hicho unachofanya.

Kukamilisha machache ni mafanikio makubwa kuliko kuanzisha mengi.
Acha kujisifia kwa kuanzisha, jisifie kwa kumaliza au kukamilisha.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe