3289; Kusubiri kuanza.

Rafiki yangu mpendwa,
Kama kuna kitu ambacho unataka kukifanya, lakini kwenye kuanza unasubiri kwanza, hujakitaka kweli kitu hicho.

Kadiri unavyosubiri kwa muda mrefu kuanza kufanya kitu, ndivyo inavyokuwa vigumu kuanza kukifanya na hata kupata mafanikio. Hiyo ni kwa sababu kusubiri kunapooza kitu na kuondoa ule msukumo na uharaka wa kuchukua hatua.

Kitu ambacho wengi huwa wanasingizia kwenye kusubiri kwa muda mrefu ni kufanya maandalizi ya kutosha.
Lakini hilo ni kujidanganya tu, huhitaji maandalizi makubwa sana ndiyo uanze kufanya kitu.
Unatakiwa kuanza kwanza, halafu mengine yafuate.
Ukianza kabla hata ya kukamilisha maandalizi, utajua ni maandalizi gani ya muhimu zaidi.

Kuamini kwamba siku fulani zijazo utakuwa tayari zaidi kuanza kuliko sasa ni kujidanganya tu.
Wakati ambao upo tayari zaidi kuanza kufanya kitu ni pale unapokuwa umepata wazo la kukifanya.
Hapo ndipo unakuwa na shauku kubwa ya kufanya, ambayo kadiri muda unavyokwenda inakuwa inapungua.

Muda unavyokwenda, kitu kinapoa na ule msukumo wa kukianza unapungua na kuondoka kabisa.
Mwishowe unajikuta ukiwa na sababu nyingi za kutokufanya kuliko sababu za kufanya.

Kuwa mtu wa kuanza kufanya mara moja yale unayokuwa unayataka.
Usiwe mtu wa kusubiri mpaka ufanye maandalizi fulani, anza na maandalizi mengine yataendelea.
Maandalizi unayokuwa unayafanya wakati unaendelea kufanya huwa yanakuwa sahihi kuliko yale unayofanya ukiwa unasubiri.

Kama kweli kuna kitu unachokitaka sana, basi unapaswa kukipambania kwa ukubwa sana.
Unapaswa kuanza kukifanyia kazi mara moja na kwenda ukiboresha kulingana na matokeo unayoyataka.
Kusubiri ni kiashiria kwamba hukitaki kitu hasa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe