3292; Kuvutiwa na maneno.

Rafiki yangu mpendwa,

Maneno huwa ni rahisi sana kuyatoa,
Na matendo huwa ni magumu sana kuonyesha.
Watu ni rahisi kukupa maneno mazuri na yanayoshawishi.
Lakini inapokuja kwenye matendo, wengi huwa siyo watekelezaji wazuri wa yale wanayoongea.

Hivyo basi, unapaswa kuwa makini sana na maneno ya watu.
Usiyape maneno uzito mkubwa kama hayajaambatana na matendo yanayodhihirisha maneno hayo.

Usiwe rahisi kuvutiwa na maneno pekee, hata kama anayeyatoa anakuwa na ushawishi kiasi gani.
Sikiliza, lakini subiri uone matendo kabla hujavutiwa na maneno peke yake.

Kwa bahati mbaya sana, wale wanaojieleza sana, ambao pia ndiyo wanaoshawishi, huwa siyo watendaji wazuri.
Kuvutiwa na maneno ya watu wa aina hiyo na kuweka matumaini makubwa kwao ni kujiandaa kuangushwa na kukatishwa tamaa.

Umeshasikia maneno mengi sana mpaka sasa, lakini matendo ni machache.
Weka thamani kubwa kwenye matendo kuliko maneno ili usiangushwe na matumaini hewa.

Kwa upande wa pili, yaani kwako mwenyewe, usiwe mtu wa maneno mengi.
Bali kuwa mtu wa matendo zaidi.
Fanya kile unachokuwa umesema utafanya.
Hiyo ndiyo njia rahisi ya kuaminika na hata kupata mengi unayotaka.

Fanya kile kilicho sahihi na kinachopaswa kufanywa.
Na ukimaliza nenda kwenye kingine kinachopaswa kufanywa.
Usipoteze muda kwenye maelezo mengi, wanaokuelewa hawayahitaji hayo maelezo na wanaoyahitaji bado hawatakuelewa hata uwaelezeje.

Matendo yana nguvu kubwa kuliko maneno.
Weka thamani kubwa kwenye matendo na utapunguza usumbufu mwingi na matumaini hewa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe