3307; Chagua kwa usahihi.

Rafiki yangu mpendwa,
Wakati mwingine watu wanashindwa kwenye kile wanachofanya, siyo kwa sababu hakiwezekani, bali kwa sababu wanakuwa hawajachagua kwa usahihi wale wanaowalenga.

Unaweza kuwa na biashara ambayo ni nzuri kabisa, ambapo kuna thamani kubwa unayoitoa, ambayo watu wana uhitaji nayo, lakini bado ikashindwa.
Biashara kama hiyo inashindwa kwa sababu unakuwa hujachagua kwa usahihi wateja ambao unawalenga.

Kufanikiwa kwenye biashara, huwezi tu kuchukua kila aina ya mteja kwa sababu ana uhitaji.
Lazima kuwe na sifa ambazo unaziangalia kwa wateja ambao watakufaa zaidi.
Na moja ya sifa hizo ni uwezo wa wateja kumudu kulipia kile unachouza.

Siri kuu ya kupata fedha ni kuwahudumia watu ambao tayari wanazo.
Pamoja na mengine mengi unayoweza kuwa unaangalia, hilo la uwepo wa fedha ni muhimu kulizingatia.

Biashara nyingi zimekuwa zinashindwa kwa sababu zinahangaika na wingi wa wateja, lakini wasiokuwa na uwezo wa kumudu kulipia kinachouzwa.

Wateja wasiokuwa na fedha, wanaweza kuwa na uhitaji kabisa, lakini kwa kushindwa kumudu, wanakuwa hawawezi kukipata.

Kwa upande mwingine, wateja wasio na fedha hukazana kuangalia nini wanaweza kufanya wenyewe ili kuokoa fedha, hata kama watatumia muda zaidi.

Wateja wazuri kwenye biashara yoyote ile, ambao ni wateja wenye fedha, huwa wapo tayari kulipa ili kuokoa muda, hata kama watatumia gharama zaidi.

Kama hupati kiasi cha fedha ulichopanga na kutegemea kupata, usianze kwa kuangalia wingi wa unaowalenga, bali anagalia ubora wao kwa uwezo wao wa kumudu kulipia.

Kupata fedha, chagua kuwahudumia vizuri sana wateja ambao tayari wanao uwezo wa kumudu kulipia unachouza.
Kwenda kinyume na hilo ni kujipa kazi ngumu na itakayokukwamisha.

Je wanaweza kumudu?
Hilo ni swali muhimu ambalo litafungua mengi mbele yako.
Kupata fedha, jihusishe na wale ambao tayari wanazo.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe