Kuna watu huwa wanaweka juhudi kubwa sana kwenye yale wanayofanya kwenye maisha yao. Kama ni biashara wanakuwa wanajituma sana, kadhalika kwenye kazi na mengine ambayo wanafanya.

Lakini matokeo ambayo wanayapata, yanakuwa hayaendani kabisa na juhudi wanazokuwa wanaweka. Watu wa aina hiyo huwa wanaweza hata kuonewa huruma, na kuonekana kama watu ambao hawana bahati. Wengine hudhani kuna namna wamefanyiwa ili wasifanikiwe. Wapo wanaoenda mbali na kusema watu hao wameibiwa nyota zao, hivyo juhudi wanazoweka zinawanufaisha watu wengine.

Maelezo yote hayo ni ya nje tu, ambayo yanashindwa kuona chanzo halisi kinachowafanya watu kushindwa kupata matokeo makubwa licha ya kuweka juhudi kubwa.

Sababu halisi ya watu kushindwa kupata matokeo makubwa licha ya juhudi kubwa wanazokuwa wanaweka ni hali ya wao wenyewe kutokujikubali na kutokujiamini. Hii ni hali ambayo inaweza kuchukuliwa kirahisi, lakini ina madhara makubwa sana kwa mtu.

Mtu yeyote anayeweka juhudi kubwa kwenye yale anayofanya, lakini akawa hajiamini au hajikubali, hawezi kupata mafanikio makubwa. Hiyo ni kwa sababu atashindwa kusimamia mambo yaliyo sahihi kwake kwa sababu tu hajikubali wala kujiamini. Mtu anaweza kuwa ana kitu chenye thamani kubwa, lakini akashindwa kutoza gharama anayostahili kulipwa kwa sababu hajiamini wala hajikubali.

Mtu asiyejiamini na kujikubali, huwa anafanya mambo ili kuwaridhisha wengine, hata kama ni mambo yasiyokuwa na faida kwao. Kwa njia hiyo wanajikuta wakihangaika na mengi ili kuwaridhisha wengine, wakati wao wenyewe hawanufaiki.

Watu wasiojiamini na kujikubali pia huwa ni rahisi kukata tamaa pale wanapokwamishwa na wengine. Wanakuwa wanategemea sana kukubalika na wengine kama ukamilifu wao. Pale wengine wanapowapinga au kuwakosoa, wanajiona hawana thamani na hivyo kuhangaika kuwaridhisha.

SOMA; Bila huu ung’ang’anizi huwezi kufanikiwa.

Ili juhudi unazoweka ziweze kuzalisha matokeo makubwa, lazima mtu ujiamini na kujikubali wewe mwenyewe. Jiamini kwamba unaweza kufanya makubwa kadiri utakavyo. Jikubali kwamba umekamilika kwa namna ulivyo. Hata kama wengine hawaoni hayo ndani yako, wewe jua tayari unayo. Pale wengine wanapokupinga na kukukosoa, wapuuze kabisa. Jua hakuna yeyote mwenye nguvu au mamlaka ya kuathiri maisha yako bila ya ruhusa yako.

Ukiweza kujiamini na kujikubali, unakuwa umeondoa kikwazo kikubwa sana ambacho kilikuwa kimekuzuia kwa muda mrefu. Juhudi zozote unazoweka zinaanza kuzalisha matokeo makubwa mpaka watu wanashangaa nini kimebadilika.

Ukweli unakuwa umebadilika ndani, kwa kujiamini na kujikubali sana na matokeo yanaonekana nje.

Hatua ya kuchukua hapa ni wewe kuanza kujiamini na kujikubali. Fanya hivyo hata kama ni kwa kuigiza. Jiambie kwa kurudia rudia kwamba wewe ni bora, wewe ni mkuu na maneno mengine ya vile unavyotaka kuwa. Fanya hayo kwa imani kabisa na usikubali kuyumbishwa na chochote. Ukifanya hivyo kwa muda mrefu bila kuacha, utaanza kuona mabadiliko ya ndani na hatimaye ya nje. Fanya zoezi hili kwa uhakika ili juhudi unazoweka ziweze kuzalisha matokeo makubwa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.