Kwenye uchumi wa soko huria, ambapo wengi tupo kwa sasa, ushindani wa biashara ni kitu ambacho kipo na kina nguvu. Soko huria linatoa fursa kwa yeyote mwenye bidhaa au huduma bora na anayoweza kuitoa kwa bei ambayo wateja wanamudu kuweza kuingia sokoni.
Ushindani mkali kwenye soko umekuwa unapeleka biashara nyingi kufa. Zinakuwa ni biashara ambazo zina uwezo mzuri, lakini kwa ushindani mkali wa soko zinakosa wateja au gharama zinakuwa kubwa na hivyo kushindwa kujiendesha.

Kufa kwa biashara kwenye soko huria ni kitu cha kawaida, ambacho kina manufaa makubwa kwenye uchumi. Japo ni jambo la kuumiza kwa yule ambaye biashara yake inakufa, lakini uchumi kwa ujumla unakwenda vizuri.
Ni hatari ya kufa kwa biashara ndiyo inawasukuma wote wanaocheza kwenye soko huria kuwa na tahadhari kubwa. Kunawasukuma wajenge biashara ambazo zinaweza kuhimili ushindani ili zisife kabisa.
Inapokuja kwenye ushindani wa biashara, wengi huwa wanatumia njia ya mkato ya kushindana ambayo ni kupunguza bei. Lakini hiyo ni njia rahisi ambayo inaweza kutumiwa na kila mtu. Na mmoja anaposhusha bei, wengine pia wanashusha bei. Matokeo yake ni wafanyabiashara wote kujikuta wakipata hasara.
Wafanyabiashara mbalimbali wakubwa wamewahi kujaribu njia mbalimbali za kukabiliana na ushindani, ikiwepo ya kukubaliana kupanga bei baina ya wafanyabiashara wakubwa na kuzuia wapya wasiingie kwenye soko. Mbinu hizo kwa sasa haziwezekani tena kwa sababu kumewekwa sheria zinazozuia hilo kutokea.
Pamoja na sheria mbalimbali zilizowekwa ili kuhakikisha ushindani unaendelea kuwepo, bado zipo njia halali za kukabiliana na ushindani. Zipo njia ambazo hazivunji sheria lakini zina nguvu kubwa ya kuzuia ushindani usiue biashara.
Mfanyabiashara yeyote makini anayetaka kujenga biashara yenye mafanikio makubwa, anapaswa kuzijua njia hizo na kuzifanyia kazi kwa uhakika ili ajiwekee kinga ya ushindani wa kibiashara.
Kuwa na kwa nini kubwa inayokusukuma kuingia kwenye biashara ni kitu cha kwanza ambacho unapaswa kuwa nacho na kikakusaidia kukabiliana na ushindani. Pamoja na kwamba moja ya sababu za kuingia kwenye biashara ni kupata fedha, haipaswi kuwa ndiyo sababu pekee. Unapaswa kuwa na msukumo mwingine mkubwa zaidi. Msukumo huo ndiyo unaokuwezesha kuvuka kila aina ya changamoto na kufanikiwa.
Kuwa na kitu cha kipekee kwenye biashara ambacho hakiwezi kuigwa na watu wengine ni njia ya kuepuka ushindani wa kibiashara. Licha ya kwamba vitu vingi ni vya kawaida na vinavyoweza kuigwa, bado kuna vitu ambavyo biashara inaweza kuwa navyo na ikawa vigumu kuigwa. Inaweza kuwa ni ugunduzi ambao una hati miliki na hivyo wengine hawawezi kutumia bila ruhusa. Lakini pia unaweza kuwa ubunifu wa kipekee au sifa binafsi zinazoweza kutumika kwenye biashara
Kujenga jina lenye sifa na linaloaminika (brand) ni njia nyingine ya kujenga nguvu ya ushindani kwenye biashara. Watu huwa wanakuwa na imani kubwa kwenye majina yenye sifa na yanayoaminika kuliko kwa bidhaa au huduma nyingine zinazofanana na hizo lakini siyo za jina hilo. Jina huwa linajengwa kwa sifa fulani ambazo biashara inajitambulisha nazo kwa msimamo na muda mrefu. Inaweza kuchukua muda mrefu kujenga jina, lakini likishajengeka na sifa yake ikalindwa, huleta nguvu kubwa ya kuhimili ushindani.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza kwa kina njia hizi za kujenga biashara imara na inayoweza kuhimili ushindani uliopo sokoni. Karibu usikilize kipindi na utoke na mambo ya kwenda kufanyia kazi kwenye biashara yako ili iwe imara na ya mafanikio makubwa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.