Mteja Balozi

Balozi sio neno geni katika masikio yetu. Neno hili katika utendaji wetu wa kawaida lina maana ya mtu anayewakilisha serikali ya nchi yake katika nchi nyingine. Balozi awapo katika nchi husika kazi yake kubwa ni kumwakilisha rais wa nchi yake katika nchi husika.

Kazi kubwa ya balozi ni kutetea maslahi ya nchi yao katika nchi wanazofanyia kazi. Japo kila kitu nchi yao ndiyo inayokuwa inafadhili, lakini uwepo wao una manufaa makubwa. Kwa lugha rahisi unapoingia katika ubalozi wa nchi fulani jua umefika katika nchi hiyo.

Katika ulimwengu wa biashara, balozi ni mteja ambaye amenunua mara nyingi katika biashara yako. Anaweza kuwakilisha biashara yako mahali pengine au kwa watu wengine. Maana huyu amezidi ngazi za chini kama uanachama. Ni mengi anayajua kuhusu biashara yako.

Sifa kuu ya mteja balozi;
Moja; Anaijua biashara yako tofauti na mteja mwanachama.
Mbili; Anakupa wateja wa rufaa wengi zaidi.
Tatu; Amenunua mara nyingi (zaidi ya mara tano+)
Nne; Anaiamini na anaipenda biashara yako.

Wateja balozi ni wateja unaopaswa kuwa nao karibu mno ili nao wawe karibu yako. Ili wakakutangaze kwa watu wengine. Maana kukusemea kwa wengine ni moja ya wajibu wao. Wakipata changamoto wasaidie ikiwa unaweza kuitatua. Kwani wataona umetenga muda wako kuwasaidia pale walipokuwa na uhitaji. Mtu kama huyu inapotokea amepata mtu anayetaka huduma yako hawezi kukataa kumleta kwako. Kwa sababu tayari ulishaonyesha nia ya kumsaidia.

Wape faida sio sifa. Sifa ni vile kitu kilivyo na faida ni suluhu juu ya kitu husika. Hivyo, unapokuwa unazungumza na watu hawa hakikisha unalizingatia hili. Mtu mara zote yupo tayari kuweka nguvu pale anapoona panampatia faida. Vile vile kupitia kujua faida hizo inamrahisishia yeye kuwa mtetezi wako mahali pengine anapoona mtu anahitaji huduma yako.

Kadiri mazungumzo na mahusiano yanavyozidi kukua ndivyo unavyozidi kuwa na uwanja mpana wa kuwaomba rufaa. Kwenye kuomba rufaa usiogope kuomba, wewe waambie, kumbuka aombaye hupewa. Waambie unamjua mtu mmoja anayeweza kunufaika na huduma au bidhaa yetu. Hapo unaomba kwa kuwaambia kama kuna mtu wanamjua. Wenye uwezo Wakisema ndio endelea kuomba mawasiliano, mahali walipo na kampuni zao. Ukipata wateja wa rufaa waingize kwenye mchakato wako.

Mambo ya kuzingatia ili kutengeneza wateja balozi;
Moja; Uaminifu.
Wanahitaji uaminifu mkubwa maana wapo tayari kukuletea wateja wengine.
Mbili; Kuwa nao karibu.
Wakipata changamoto wasaidie kulitatua.

Tatu; Mpe huduma bora

Je, biashara yako inao wateja wangapi balozi?

Endelea kutengeneza wateja balozi wengi zaidi ili kuikuza biashara yako. Jifunze, elimika na uchukue hatua.

Imeandaliwa na Lackius Robert, Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo. Tuwasiliane 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz