Kabla watu hawajanunua chochote kile unachouza, wanaanza kukununua wewe kwanza. Hii ni kusema hatuuzi tu kile tunachouza, bali tunajiuza sisi wenyewe kwanza.
Wengi wanaposikia umuhimu wa kujiuza wao wenyewe, huwa wanafanyia kazi vitu vinavyoonekana kama kuwa na tabasamu, kuwa nadhifu na vingine vya aina hiyo. Hivyo ni vitu muhimu sana kufanyia kazi, lakini kuna vingine muhimu zaidi ambavyo havionekani ila athari yake ni kubwa kwenye mauzo.

Moja ya vitu hivyo visivyoonekana lakini vinaathiri sana mauzo ni hali ya mtu KUJIAMINI na KUJIKUBALI yeye mwenyewe. Hivi siyo vitu ambavyo vinaonekana kwa nje, lakini athari yake ni kubwa.
Huwa tunasema mauzo ni mabadilishano ya imani, mteja ananunua pale anapoamini. Na imani ya kwanza kwa mteja siyo kwenye kile anachonunua, bali kwa yule anayeuza kitu hicho.
Mara nyingi sana mteja hana uelewa mpana wa kile anachonunua kama muuzaji. Na hana muda wa kujifunza mpaka akabobea, anachotaka yeye ni kupata kitu kitakachomwezesha kutatua changamoto alizonazo. Hivyo uwezo wake wa kufanya maamuzi kwenye kitu anachonunua siyo mkubwa sana.
Kutokana na uwezo wake wa kufanya maamuzi kuathiriwa na uelewa finyu alionao, huwa anatumia imani ya muuzaji kufanya maamuzi. Mteja huwa ananunua pale anapoamini kwamba muuzaji anaamini kweli kwenye kile anachouza.
Muuzaji anaweza kuamini kweli kwenye kile anachouza kama anajiamini na kujikubali yeye mwenyewe. Hapo ndipo anapoweza kusimamia vyema kile anachouza na kuwashawishi watu kununua.
Watu huwa wana hisia ya sita, ambayo ni machale na hisia hiyo huwa inanusa kwa haraka sana kile ambacho watu wanakificha. Pale mtu anapokuwa na wasiwasi au hofu juu ya kitu, hisia hiyo ya sita huwa inanasa haraka sana.
Hivyo muuzaji yeyote ambaye hajikubali na kujiamini huwa anakuwa na wakati mgumu kuuza, kwa sababu wateja wanalinasa hilo kupitia hisia zao za sita. Muuzaji anaweza kuelezea bidhaa au huduma yake vizuri, lakini kile kitendo cha kutokujiamini na kujikubali, kinawafanya wateja wasiwe tayari kuchukua hatua mara moja.
SOMA; Tabia Sahihi Zitakazokupa Mafanikio Kwenye Mauzo.
Wateja huwa wanapima kujiamini na kujikubali kwa muuzaji kwa njia mbalimbali, baadhi ya njia hizo ni;
1. Kumpuuza muuzaji ili kuona ana ung’ang’anizi kiasi gani. Mfano kutokupokea simu, kukata simu, kukataa salamu n.k.
2. Kumpa muuzaji mapingamizi mengi na kuona kama anaweza kuyavuka. Mfano kusema bei ni ghali, ubora ni hafifu n.k.
3. Kumdanganya muuzaji ili kuona kama anaujua ukweli. Mfano kusema kitu hicho hakifanyi kazi au ni feki.
4. Kumpa muuzaji ahadi hewa ambayo anajua kabisa hataitekeleza. Mfano kumwambia muuzaji atamtafuta akiwa tayari.
5. Kuweka oda kabisa lakini kukwepa kukamilisha malipo. Mfano kumwambia muuzaji anaenda kuchukua fedha na atarudi.
Hizo ndizo njia ambazo wauzaji wengi wamekuwa wanapoteza mauzo na ni njia ambazo wateja huwa wanazitumia pale wanapokosa imani kwa muuzaji.
Kwa upande wa wauzaji, kuna dalili ambazo huwa wanakuwa nazo zinazoonyesha hawajiamini wala kujikubali kiasi cha kutosha kuweza kufanya mauzo makubwa. Baadhi ya dalili hizo ni;
1. Kuhofia kuwafuatilia wateja kwa kuona utakuwa unawasumbua, wakati wateja hao hawajakuambia unawasumbua.
2. Kukata tamaa haraka baada ya kukataliwa mara kadhaa na mteja.
3. Kujisikia vibaya pale mteja anapotoa mapingamizi na kuona kama anakushambulia wewe.
4. Kuwakubalia wateja kwenye ahadi hewa wanazotoa kwa kuamini ni za kweli.
5. Kuongozwa na mteja wakati wa mchakato wa mauzo, kwa mteja kuwa ndiye anayeuliza maswali na muuzaji kumjibu, mwisho anashindwa kumuuzia.
Wauzaji wote ambao hawafanyi mauzo makubwa, huwa wana hizo dalili za kutokujiamini na kujikubali na hivyo kutokuaminika na wateja.
Kujiamini na kujikubali siyo tabia ambazo mtu anazaliwa nazo, bali ni tabia ambazo mtu anafundishwa au kujifunza mwenyewe. Hivyo kama umegundua kutokujiamini na kutokujikubali ndiyo kumekuwa kikwazo kwako, ambao ndiyo ukweli kwa wauzaji wengi, chukua hatua zifuatazo;
1. Kila siku andika na jiambie kwa sauti; MIMI NI MUUZAJI BORA KABISA KUWAHI KUTOKEA. Jiambie kauli hiyo ukiwa unamaanisha kabisa na ukiwa umejawa furaha.
2. Jifunze kuhusu bidhaa/huduma unazouza na jua kuliko wengine wote. Kuwa mtu aliyebobea kwenye kile unachouza na wafundishe na kuwashauri wengine vyema. Mfanye kila mteja anayeongea na wewe aondoke amejifunza kitu ambacho hakuwa anakijua.
3. Ongoza mazungumzo ya mauzo kwa kuwa muulizaji wa maswali na kusikiliza kwa umakini. Pale mteja anapokupiku na kuanza kuongoza kwa maswali, gundua hilo na rudisha kibao kwa kumuuliza maswali. Fanya hilo kwa umakini mkubwa kwa sababu ndipo ushindi unapoanzia.
4. Furahia pale mteja anapoleta mapingamizi, ukijua huyo ndiye mteja wa kununua kwa uhakika. Pokea mapingamizi na yajibu kwa namna ambayo unaondoa kila wasiwasi ambao mteja anao. Hata kama mapingamizi ni magumu kiasi gani, usionyeshe kama yamekugusa wewe, tambua ni mapingamizi kwenye kile unachouza na siyo kwako wewe kama mtu. Ukiweza kujitofautisha wewe na kile unachouza, hakuna mapingamizi yanayoweza kukuumiza.
5. Ng’ang’ana mpaka uuze, mfuatilie mteja mpaka anunue au akuambie yeye mwenyewe usimfuatilie tena. Kila ahadi ambayo mteja anakupa, ifuate hivyo hivyo. Amekuambia nitafute jumatano ijayo, mtafute siku hiyo kweli. Akikupa ahadi tena, ifuatilie. Kuwa na ufuatiliaji wa karibu kwa wateja wako bila kuchoka na kuna ambao watanunua kwa kuheshimu ung’ang’anizi wako. Kama hujiamini utasema hutaki kuwafuatilia sana wateja kwa sababu utawasumbua na hawatanunua. Sikiliza, kama mteja atakataa kununua kwa sababu umemfuatilia sana, jua asingenunua hata kama usingemfuatilia, sasa kwa nini ukubali akudanganye na kukupa ahadi hewa? Fuatilia ahadi za wateja kama walivyokupa na utaweza kuuza kwa sababu tu unaonekana unajiamini kuliko wengine.
Muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea, poteza yote kwenye mauzo lakini usipoteze kujikubali na kujiamini. Hiyo ndiyo nguvu yako ya kufanya miujiza kwenye mauzo. Kila siku ichochee kwa kujifunza na kujinenea mambo chanya na utaweza kufanya makubwa sana.
Kuwa muuzaji bora kunaanza na wewe kuwa mtu bora. Mtu bora ni yule anayejikubali na kujiamini kwenye kile anachofanya. Wewe umejifunza hapa, nenda kajijengee kujikubali na kujiamini, hata kama kutakuwa ni kwa kupitiliza. Ni bora usiuze kwa kujiamini kuliko usiuze kwa kutokujiamini.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.