3324; Unachokitaka zaidi.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Huwa kuna usemi kwamba ukitaka kujua ukuu wa mtu, angalia vitu ambavyo vinamsumbua.
Ikiwa na maana kwamba mtu anayesumbuliwa na vitu vidogo vidogo, hata mafanikio anayopambania ni madogo.
Yule anayepambania mafanikio makubwa, mambo yanayomsumbua ni makubwa pia.
Pale mtu anapotaka sana mambo makubwa, haruhusu chochote kidogo kuwa kikwazo kwake.
Utaenda mbali kiasi gani kwenye maisha yako inategemea zaidi nini unachotaka zaidi.
Kadiri unavyotaka makubwa na kuamini utayapata, ndivyo unavyokuwa tayari kuyapambania.
Ukubwa wa yale unayoyataka unakufanya usahau au kupotezea kabisa changamoto ndogo ndogo ambazo unakutana nazo kwenye safari yako.
Na hilo ndiyo limekuwa linawashangaza wale ambao hawafanikiwi sana pale wanapowaangalia waliofanikiwa.
Wanashindwa kuelewa iweje kile kilichowakwamisha wao kwa wengine kimekuwa kama kichocheo?
Ukweli ndiyo huo, kwamba hao wanaofanikiwa sana hawaangalii kingine chochote isipokuwa mafanikio makubwa wanayoyataka.
Hivyo chochote kinachokaa kati yao na mafanikio makubwa wanayoyataka wanakisambaratisha bila hata ya kufikiri mara mbili.
Wanaofanikiwa sana wanaweza kuonekana kama wanapenda kujitesa.
Lakini sivyo uhalisia ulivyo.
Wao wanataka sana kupata mafanikio makubwa wanayoyataka kiasi kwamba hawajali nini wanachokutana nacho njiani.
Wanakuwa tayari kuvuka chochote bila kujali ukubwa wake, kwa sababu wanataka sana kukipata.
Hata kwenye kuweka juhudi kubwa za kazi, siyo lazima mtu apende sana kazi.
Kinachohitajika ni mtu kutaka sana matokeo anayoenda kuyapata.
Hayo yanampa msukumo wa kuweka juhudi kubwa za kazi bila hata ya kuchoka.
Unapotaka sana matokeo unayokwenda kupata na kadiri matokeo hayo yanaonekana kuwa karibu, ndivyo juhudi kubwa zaidi zinaweza kuwekwa bila kusita.
Uchovu na usingizi vinapotea vyenyewe kutokana na shauku kubwa mtu unayokuwa nayo ya kupata matokeo unayoyataka.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA kila mtu anapambana kufikia mafanikio makubwa sana.
Hivyo chochote ambacho mtu anakutana nacho, hakimtishi, bali anakisambaratisha mara moja.
Macho yetu yapo kwenye matokeo makubwa tunayotaka kuyazalisha na hivyo hatuhangaishwi na kingine chochote.
Ni kupitia sisi kutaka sana mafanikio makubwa ndiyo vitu vingine vyote vinaonekana kuwa vidogo na visivyo na madhara.
Hivyo ndivyo tunavyokwenda, na msukumo huo wa ndani unatufanya tuvuke makubwa ambayo yanawakwamisha wengi.
Kwa matamanio ya mafanikio makubwa tuliyonayo na ambayo ndiyo tunayapambania, hakuna chochote kinachokuwa na nguvu ya kutukwamisha kwa namna yoyote ile.
Kuwa kwenye jamii hii ya KISIMA CHA MAARIFA na kukwamishwa na chochote unakuwa hujaielewa, kuiamini na kuiishi falsafa kuu inayotuongoza.
Unatakiwa kurudi kwenye misingi mikuu na kuizingatia ili uweze kufanya makubwa sana yaliyo ndani ya uwezo wako.
Kuwa na matamanio ya mafanikio makubwa ambayo unakuwa na uhakika kabisa wa kuyapata na mengine yote yataonekana kuwa madogo kwako.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe