Kwenye jamii yoyote ile huwa kuna matabaka ya watu. Japo watu huwa hawapendi kuongelea matabaka, ukweli ni kwamba yapo.
Kwa miaka ya nyuma, watu walikuwa wanalazimishwa kuwa kwenye matabaka fulani kutokana na mifumo ya utawala iliyokuwepo. Mtu aliyezaliwa na mtumwa aliingia kwenye tabaka la watumwa moja kwa moja.
Aliyezaliwa kwenye familia ya wakulima alikuwa mkulima wakati aliyezaliwa familia ya kifalme alikuwa mfalme. Hivyo ndivyo maisha ya watu yalienda kwa miaka mingi ya nyuma.
Kwenye zama hizi, ambapo dunia inaonekana kuwa na uhuru mkubwa kiutawala, matabaka ya kulazimishwa hayapo tena. Kila mtu anazaliwa akiwa huru kabisa. Lakini cha kushangaza, bado matabaka yameendelea kuwepo.

Kuna ngazi nyingi za matabaka, lakini ukiangalia kwa haraka haraka, kwenye kila jamii watu wanagawanyika kwenye matabaka matatu. Tabaka la chini ambao huwa ni masikini sana, tabaka la kati ambao siyo masikini lakini pia siyo matajiri na tabaka la juu ambalo lina matajiri.
Wengi bado wanaweza kulalamika kwamba kuna namna matabaka hayo yametengenezwa kuwatenga watu. Lakini tukiangalia kwa undani, tunaona kitu cha tofauti. Matabaka hayo hayajawekwa na watu, bali watu wenyewe ndiyi wamechagua kuwa kwenye tabaka walipo.
Hiyo ina maana kwamba waliopo kwenye tabaka la chini wamechagua wao wenyewe, kadhalika walio kwenye tabaka la kati na tabaka la juu. Unaweza kukataa kwamba watu hawachagui haya matabaka, lakini huo ndiyo ukweli. Hapa unakwenda kujifunza ni jinsi gani watu wanachagua matabaka waliyopo na nini cha kufanya ili uweze kwenda tabaka la juu kabisa.
Watu wengi kwenye maisha, huwa wanafuata mkumbo, wanafanya kile ambacho wengine wanafanya. Wanachokuwa wanaamini ni wengi wapo sahihi au kifo cha wengi ni harusi. Ukweli ni kwamba wengi hawapo sahihi na ndiyo maana wengi huwa wanaishia kushindwa na kukaa kwenye umasikini mkubwa. Watu wanaofuata mkumbo wanakuwa wamechagua kuishi kwenye gereza kwa maisha yao yote. Wanakuwa hawaoni kama kuna namna bora ya kuyaendesha maisha yao zaidi ya vile walivyozoea na wanavyoona kwa wengine. Hawa ndiyo wanaobaki kwenye tabaka la chini, ambao hawajalazimishwa na yeyote kufuata mkumbo.
Watu wachache huwa wanakataa kufuata mkumbo, hawa huwa wanapambana kubadili hali wanayokuwa nayo, wanakuwa ni wanamageuzi. Wanamageuzi hawa licha ya kuwa bado wanakuwa kwenye gereza, hawakubali kukaa chini kabisa. Bali wanapambana na kupanda juu ili kupata mwanga mzuri na hewa safi. Japo bado wanakuwa gerezani, lakini hali yao inakuwa ni afadhali ukilinganisha na wale wanaokuwa chini kabisa. Hawa ndiyo wanaokuwa wamechagua kuwa kwenye daraja la kati kwenye maisha, bado wapo kwenye gereza, lakini hawapo chini kabisa.
Wachache sana wanachagua kuvunja kabisa kuta za gereza na kuwa huru. Hawa wanakataa kabisa zile hali wanazokuwa wameanza nazo. Hawa wanakuwa waasi ambao wanaleta mapinduzi makubwa kwenye maisha yao na kuondoka kabisa kwenye gereza ambalo wameanzia. Hawa ndiyo wanaochagua kuwa kwenye daraja la juu kabisa kwenye maisha na kupata mafanikio makubwa.
Lengo langu kwako rafiki yangu, kupitia maarifa haya ambayo nimekuwa nakushirikisha ni uondoke kabisa kwenye tabaka la chini. Yaani kwa kujifunza tu kupitia haya maarifa uondoke kabisa kwenye hilo tabaka la kufuata mkumbo. Angalau uwe mwanamageuzi ambaye unayabadili maisha yako badala tu ya kukubali kile kilichopo.
Halafu sasa, kama utaingia kwenye ngazi za juu za huduma ninazotoa, lengo langu linakuwa ni wewe ufike tabaka la juu kabisa. Nakufanya kuwa muasi ambaye unaleta mapinduzi makubwa kwenye maisha yako na kupata mafanikio makubwa sana.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimefafanua zaidi dhana hii ya kuwa muasi na kuleta mapinduzi na hatua za wewe kuchukua ili uweze kufika daraja la juu la mafanikio kwenye maisha yako na kuwa na uhuru kamili. Karibu usikilize kipindi hiki na uchukue hatua sahihi ili uwe huru na kupata mafanikio.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.