Rafiki yangu mpendwa,

Wewe kama muuzaji, kazi yako ya kwanza ni kuwafanya watu wakubaliane na wewe. Kabla hujaishia hapa na kusema wewe siyo muuzaji, nikukumbushe tu kwamba kwenye maisha kila mtu anauza. Tofauti ni unauza nini.

Kama umeajiriwa unauza muda wako, nguvu zako na ujuzi wako kwa mwajiri wako. Kama ni kiongozi unauza maono yako kwa wale unaowaongoza. Kama ni mtu wa afya unauza afya, mwalimu unauza elimu na kutaka kuwashawishi watu wajifunze kile unachofundisha.

Baada ya kukubaliana kwamba sisi wote ni wauzaji, sasa turudi kwenye jambo la msingi. Mauzo ni kuwashawishi watu na huwezi kuwashawishi watu bila kuzungumza nao. Na hapo ndipo kazi kuu ya mauzo na ushawishi inaposimamia, ongea na watu.

Upo usemi wa Kiswahili kwamba ONGEA NA WATU UPATE VIATU, unaonyesha jinsi ambavyo ni muhimu kuongea na watu wengi zaidi kupata kile tunachotaka. Hivyo ndivyo mauzo na ushawishi ulivyo, kadiri unavyoongea na watu wengi, ndivyo unavyoweza kuwashawishi wengi pia.

Mauzo na ushawishi ni mchezo wa namba, fikia wengi, shawishi wengi. Kuongea na watu wengi ndiyo kitu ambacho muuzaji yeyote akikifanya ataweza kufanya mauzo makubwa zaidi.

Unaweza kuwa unajiuliza hili linakuwaje jambo linalohitaji mtu ufundishwe, si ndiyo kitu mtu unafanya kila siku? Ni kweli unaweza kuwa unaongea kila siku, lakini unaongea na nani na unaongea naye nini ndiyo kilicho muhimu zaidi.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza kwa kina namna sahihi ya kuongea na watu wengi zaidi ili uweze kufanya mauzo makubwa zaidi. Karibu uangalie kipindi hicho, ujifunze na kwenda kutumia muda wako vizuri kuongea na wengi na kuuza zaidi.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.