3328; Kifo kikutenganishe.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Ndoa za Kikristo huwa zina kiapo cha watu kuwa mwili mmoja mpaka kifo kiwatenganishe.
Kiapo hicho kinamaanisha watu wataendelea kuwa pamoja bila ya kujali ni nini wanapitia.
Kama tu wapo hai, basi wataendelea kuwa pamoja, wakihimili kila aina ya magumu na changamoto ambazo zingeweza kuvunja ndoa hiyo kama kiapo hicho kisingekuwepo.

Hiki ni kiapo kizuri sana kwako kufanya wewe na safari yako ya mafanikio.
Kwenye safari yako ya mafanikio, unaweka kiapo kwamba utakaa kwenye mchakato wa mafanikio mpaka kifo kikutenganishe.
Kwamba kwa kipindi chote cha uhai wako, utauishi mchakato wa mafanikio, bila ya kujali nini ambacho unapitia.
Hata pale unapokutana na magumu na changamoto ambazo zinawakatisha tamaa wengine, wewe hukati tamaa, bali unaendelea na mchakato wako.
Kiapo hiki kina nguvu kubwa sana kwa sababu kama mtu hutauacha mchakato wa mafanikio kwa maisha yako yote, ni labda utayapata mafanikio unayoyataka au utakufa ukiwa unayapambania.
Kwa vyovyote vile utakuwa umefanikiwa, kwa sababu kitendo tu cha kutokuuacha mchakato ni mafanikio, hata kama hujapata kila unachotaka.
Huo mchakato wenyewe ni upi hasa?
Mchakato ambao unafunga nao ndoa ni MAARIFA + VITENDO = MAFANIKIO.
Kwanza kabisa unajua wazi nini hasa unachokitaka kwenye maisha yako, hiyo ndiyo hatua muhimu ili usihangaike na mengi.
Mbili unapata maarifa sahihi ya kukuwezesha kupata kile unachotaka. Kwa kuwa maarifa ni mengi na huwezi kuyamaliza yote, kujifunza kunakuwa endelevu kwako.
Tatu ni kuweka kwenye matendo yale yote unayojifunza, yaani kuchukua hatua. Kila wakati unafanya kwa ubora zaidi ya ulivyofanya huko nyuma. Unavyoendelea kufanya kwa ubora, ndivyo unavyojisogeza karibu na matokeo unayoyataka.
Ni kwa kuzingatia hayo yote ndiyo unayazalisha matokeo unayoyataka, ambayo ndiyo mafanikio kwako.
Kiapo hiki ni muhimu siyo tu kuyavuka magumu ambayo yanaweza kukukatisha tamaa, bali pia kuepuka tamaa ambazo zinaweza kukuhamisha kwenye kile kikuu unachofanya.
Kwenye KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, kila mwanachama amejitoa kweli kufanikiwa.
Hakuna kubahatisha, bali ni safari ya uhakika, kwa kufuata mchakato wa uhakika.
Kuwa ndani ya KISIMA CHA MAARIFA umekata shauri wewe mwenyewe kwamba ndiyo mahali utafia.
Husubiri kusukumwa ndiyo ukae kwenye mchakato, bali unajisukuma wewe mwenyewe.
Unafurahia kuzungukwa na wengine ambao nao wanayapambania mafanikio makubwa, kitu ambacho ni kizuri sana na tofauti na kwenye jamii za kawaida ambapo wengi wamekata tamaa na wanawakatisha wengine tamaa pia.
KISIMA ni sehemu ya kukufanya uache kujidanganya, hasa pale unaposhindwa kwenye yale unayotaka. Badala ya kujiambia haiwezekani kama wengi wanavyojidanganya kwenye jamii ya kawaida, hapa unakutana na wengine ambao tayari wameweza, hivyo unakuwa huna cha kujitetea zaidi ya kuendelea kupambana.
Lakini pia kuwa ndani ya KISIMA inakuzuia usiridhike haraka pale unapoanza kupata mafanikio, maana hicho ni kingine kinachowapoteza wengi. Hapa kila hatua unayopiga ni mwanzo wa hatua nyingine kubwa zaidi. Hakuna hatua utakayofika na kuona tayari umeshamaliza kila kitu. Bali kila hatua ni mwanzo kabisa wa hatua nyingine kubwa na ngumu zaidi.
Weka kiapo hiki cha mafanikio leo, jiwekee mwenyewe kiapo hiki na kishirikishe kwenye kundi la KISIMA CHA MAARIFA kama njia ya kuidhihirishia jamii hiyo kujitoa kwako.
Andika; MIMI …. (majina yako) NA MCHAKATO WA MCHAKATO MKUU WA MAFANIKIO AMBAO NI MAARIFA + VITENDO = MAFANIKIO NI MPAKA KIFO KITUTENGANISHE. NITADUMU KWENYE MCHAKATO HUU KWA MAISHA YANGU YOTE, BILA KUJALI NAPITIA NINI.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe