Watu huwa wanapenda kuwa na furaha. Kwa hakika hicho ndiyo kitu kinachotafutwa na watu wengi zaidi. Kila kitu ambacho watu wanafanya, lengo kuu ni kuwa na furaha.

Lakini kwa bahati mbaya sana, furaha imekuwa kitu kigumu kwa wengi kukipata. Na hata kwa wachache wanaoipata furaha, imekuwa haidumu kwa muda mrefu.

Kuna mengi ya kuzungumza kuhusu furaha, kuanzia kwamba siyo kitu cha kukimbiza kwa sababu inazidi kukukimbia. Lakini leo tunakwenda kuangalia upande mwingine wa furaha ambao umekuwa haupewi uzito na watu wengi.

Upande huo wa furaha ni ile inayotokana na hali ya kuridhika na kitu ambacho mtu amekifanya. Katika vitu vingi ambavyo watu wanafanya, kila mtu kuna ambacho huwa kinamridhisha zaidi anapokifanya, bila ya kujali yeye amenufaikaje.

Mara nyingi kinachokuwa kinamnufaisha mtu kwenye vitu vya aina hiyo ni namna wengine wanavyokuwa wamenufaika na hicho anachofanya. Pale mtu anapopokea shukrani kutoka kwa wengine kwa jinsi ambavyo kike alichofanya kimewasaidia, anaridhika na kufurahia.

Sasa basi, ili furaha iweze kudumu kwa mtu, angepaswa kufanya zaidi hicho ambacho kinampa hali ya kuridhika. Lakini kutokana na mahitaji mengine ya maisha, kwa wengi inakuwa haiwezekani kukifanya hicho kuwa ndiyo shughuli yao kuu.

Na hapo ndipo wanapoagana na furaha yao. Kwa sababu wanakuwa na mahitaji mengine ya maisha ambayo yanawataka wahangaike zaidi na shughuli zinazowaingizia kipato, wanaachana kabisa na kile kinachowapa furaha. Hapo wanasumbuka na yale ya kuwaingizia kipato na kusahau kabisa kile ambacho kinawapa kuridhika.

Watu wa aina hii huwa wanadhani wakishapata fedha basi watapata furaha. Na kwa mapambano yao huwa wanapata fedha, lakini furaha hawapati, kwa sababu wamesahau kile kilichokuwa kinawapa furaha. Kwa wasioelewa wanasema fedha hainunui furaha, kumbe hakuna uhusiano hapo kati ya fedha na furaha.

Kuna ambao wanapita njia ya pili, ya kuamua kugeuza kile kinachowapa furaha kuwa ndiyo njia yao kuu ya kuingiza kipato. Njia inayoonekana kuwa nzuri, kwa sababu kuna mpaka semi mbalimbali kwamba ukifanya kile unachopenda basi hutafanya kazi maisha yako yote. Lakini hapa watu wanachanganya kupenda na kupata furaha. Unaweza kupenda unachofanya na bado kisikupe furaha.

Hatari inayokuja kwa wale wanaogeuza kile kinachowapa furaha kuwa ndiyo njia yao kuu ya kuingiza kipato ni pale fedha inapohusika ile hali ya kuridhika inaondoka. Fedha ikishahusika, mahitaji na matakwa yanabadilika. Pale ambapo mtu alikuwa anafanya kwa msukumo wa kuwa na mchango kwa wengine, anajikuta akifanya kwa msukumo wa kupata fedha zaidi.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; The Psychology Of Money (Masomo Kuhusu Utajiri, Tamaa Na Furaha)

Pale ambapo mtu alikuwa huru kufanya kwa vile anavyoona inafaa na hivyo kuleta matokeo ya kibunifu, analazimika kufanya kwa namna ambavyo itawaridhisha wengine ili walipwe zaidi. Hapo mambo hubadilika na kilichokuwa chanzo cha furaha kinakuwa chanzo cha kuvurugika kabisa.

Kuondokana na hayo yote na ili kuhakikisha furaha yako inadumu, tenga muda kwenye maisha yako kwa ajili ya vile vinavyokupa furaha na usivihusishe moja kwa moja na fedha. Shughuli kuu ya kukuingizia kipato isihusiane moja kwa moja na kile unachofanya na kupata kuridhika ndani ya roho yako. Na hapa nisisitize, haina uhusiano na kufanya kile unachopenda.

Kama kauli maarufu inayosema kinachokupa furaha kifiche, ndivyo unavyopaswa kuyaendesha maisha yako. Kile ambacho ukikifanya unapata kuridhika ndani yako na kuwa na furaha, kitengee muda kwenye maisha yako na hakikisha wengine hawajihusishi nao hasa kwa upande wa fedha. Ukiweza kutengeneza maisha ya aina hii, mara zote utakuwa na furaha hata kama hujapata kila unachotaka.

Zamani kulikuwa na dhana ya wito kwenye baadhi ya tasnia, ambapo watu walipata fursa ya aina hii. Lakini kutokana na mabadiliko ya maisha, wito pekee hautoshi kuendesha maisha ya mtu.

Hivyo kilichobaki sasa ni mtu kuchagua kwenye ‘hobi’ zako, moja ambayo utaifanya kuwa kitu muhimu kwako na ambayo hutaiharibu kwa namna yoyote ile. Utaitengea muda na pia hutaihusisha na fedha. Inakuwa sehemu nzuri kwako kuondokana na msongo na mengine unayokuwa unayapitia kwenye safari yako ya mafanikio.

Kila mtu ana hobi mbalimbali, hata kama baadhi utazigeuza kuwa sehemu ya kuingiza kipato, tenga moja utakayoifanya kuwa sehemu ya furaha yako kisha ilinde ili ikupe furaha ya kudumu.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.