Habari Matajiri Wawekezaji,

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo ya uwekezaji, ambayo yanatupa maarifa sahihi na hatua za kuchukua ili kuweza kujenga utajiri mkubwa kupitia uwekezaji wa kiasi kidogo kidogo kwa muda mrefu.

Tunaendelea kujifunza kuhusu uwekezaji wa mifuko ya pamoja, uwekezaji rahisi kufanya kwa kila mtu bila kujali uelewa wake kwenye uwekezaji au mtaji alionao.

Pia tunaendelea kujifunza kwenye mifuko ya uwekezaji wa pamoja ambayo inasimamiwa na dhamana ya uwekezaji Tanzania ambayo ni UTT AMIS. Leo tunakwenda kuangalia mfuko wa JIKIMU. Karibuni tujifunze na kuendelea kupata uelewa mpana ili kuwekeza vyema.

FAIDA YA UWEKEZAJI.

Kabla ya kuingia kwenye mfuko wa JIKIMU, tujikumbushe jinsi ambavyo faida inapatikana kupitia uwekezaji. Pale unapowekeza, kuna njia mbili za kuingiza faida.

Njia ya kwanza ni kukua kwa thamani ya uwekezaji. Hii ndiyo njia kuu ya kupata faida kwa kila uwekezaji. Kwa mfano kama umenunua kipande mwaka 2024 kwa shilingi 1,000/= halafu miaka 5 baadaye kipande hicho hicho kikawa shilingi 1,500/= hapo thamani ya uwekezaji wako inakuwa imeongezeka. Ukiuza vipande vyako, unapata fedha nyingi kuliko uliyowekeza. Hivyo pia ndivyo ilivyo kwa uwekezaji mwingine, mfano kununua ardhi kwa bei ya chini na kuja kuuza kwa bei ya juu.

Njia ya pili ni kupata gawio kutoka kwenye uwekezaji. Hii ni njia inayotumika kwa baadhi ya uwekezaji, pale fedha unayowekeza inapoenda kuzalisha na kuleta faida, sehemu ya ile faida inarudishwa kwa wawekezaji kama gawio. Mfano mzuri ni kwenye hisa, unaweza kuwa na hisa za kampuni fulani na mwisho wa mwaka ikapata faida na kutangaza gawio kwa kila hisa, hivyo unalipwa gawio lako kulingana na hisa zako, huku uwekezaji wako ukibaki pale pale.

Ili kuweza kujenga utajiri mkubwa na kufikia uhuru wa kifedha, unapaswa kufanya uwekezaji ambao unakuingizia faida kwa njia zote mbili, yaani unakua thamani wakati muda unakwenda, lakini pia unaendelea kukupa gawio mara kwa mara. Uwekezaji unaoweza kuwa na sifa hii ni wa hisa na baadhi ya mali ambazo zinaingiza kipato.

Kwenye mifuko ya pamoja ya uwekezaji ambayo tumeshajifunza mpaka sasa, tumeona faida inapatikana kwa ongezeko la thamani pekee. Lakini UTT AMIS kwa kuwapa wawekezaji fursa ya kunufaika, iliweza kuanzisha mfuko maalumu ambao unamwingizia mwekezaji faida kwa njia zote mbili, ongezeko la thamani na gawio la mara kwa mara. Mfuko huo ni wa JIKIMU na ndiyo tunaenda kujifunza kwenye somo hili kwa kina.

MFUKO WA JIKIMU

Mfuko wa Jikimu ni mfuko wa nne kuanzishwa na taasisi ya UTT AMIS mnamo tarehe 3 Novemba 2008. Mfuko huu ni mfuko wa wazi ulioanzishwa ili kuwawezesha wawekezaji kupata gawio kila robo mwaka au mara moja kwa mwaka na kutoa fursa ya kukuza mtaji.

MALENGO YA MFUKO

Mfuko huu ni mpango ulio wazi wenye lengo la kukuza na kutoa gawio kutokana na mapato ya ziada katika vipindi tofauti na pia kukuza mtaji kwa mwekezaji wa muda mrefu.

UKWASI/KUUZA VIPANDE.

Malipo ya mauzo ya vipande yatashughulikiwa ndani ya siku 10 za kazi baada ya kupokelewa. Fedha zitatumwa moja kwa moja katika akaunti ya benki ya mwekezaji.

WANAORUHUSIWA KUWEKEZA

Wawekezaji wote ikiwa ni pamoja na watu binafsi, taasisi, makampuni, na vikundi vya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

SERA YA MFUKO

Mfuko unaruhusiwa kuwekeza kwenye hisa zilizoorodheshwa, ikizingatiwa kuwa kiasi cha pesa kitakachowekezwa kwenye sehemu hiyo kisizidi 35% ya uwekezaji wote wa mfuko na 65% iliyobaki itawekezwa kwenye dhamana mbalimbali za serikali zenye ukomo tofauti, hatifungani za kampuni binafsi, na kwenye akaunti za amana.

SOMA; Mfuko Wa Uwekezaji Wa Pamoja Wa Umoja Wa UTT AMIS.

SIFA ZA MFUKO:

1. Mfuko una mipango mitatu ya uwekezaji kama ifuatavyo:

(a) Mpango wa gawio la robo mwaka [Kiwango cha chini cha uwekezaji ni TZS. 2,000,000]

(b) Mpango wa gawio la mwaka [Kiwango cha chini cha uwekezaji ni TZS. 1,000,000]

(c) Mpango wa mwaka wa kukuza mtaji [Kiwango cha chini cha uwekezaji ni TZS. 5,000]

2. Kiwango cha chini cha uwekezaji wa nyongeza ni:

(a) TZS 15,000 kwenye mpango wa gawio la mwaka au la robo mwaka.

(b) TZS 5,000 kwenye mpango wa kukuza mtaji.

3. Vipande vinauzwa kwa thamani halisi ya wakati huo (hakuna gharama za kujiunga).

4. Umiliki wa mtu mmoja au umiliki wa pamoja unaruhusiwa katika mfuko huu.

5. Ni rahisi kwa mwekezaji kupata fedha pindi atakapozihitaji, (ndani ya siku 10 za kazi baada ya kupokelewa kwa maombi katika ofisi za UTT AMIS).

6. Mwekezaji anaruhusiwa kutoa sehemu ya uwekezaji wake au kiasi chote.

7. Gharama za kujitoa ni kama ifuatavyo:

    (a) 2% kwa uwekezaji uliodumu kwa kipindi kisichozidi mwaka 1.

    (b) 1.5% kwa uwekezaji uliodumu kwa kipindi cha zaidi ya mwaka 1 na chini ya miaka 2.

    (c) 1.0% kwa uwekezaji uliodumu kwa kipindi cha zaidi ya miaka 2 na chini ya miaka 3.

    (d) Hakuna gharama za kutoka kwa uwekezaji uliodumu kwa kipindi cha zaidi ya miaka 3.

8. Mfuko unaruhusu uhamishaji wa vipande kutoka mwekezaji mmoja kwenda kwa mwekezaji mwingine.

9. Mwekezaji akifariki, mrithi, mwakilishi au mwombaji wa pili ataruhusiwa kuendeleza uwekezaji huo.

10. Vipande vinaweza kutumika kama dhamana ya mkopo katika taasisi za fedha.

MJADALA WA SOMO.

Karibu kwenye mjadala wa somo hili, shirikisha majibu ya maswali haya kama sehemu ya wewe kujifunza kutoka kwenye somo hili.

1. Eleza aina mbili za faida kwenye uwekezaji na mifano ya kila faida.

2. Nini tofauti ya kukua kwa thamani ya uwekezaji na kupata gawio kwenye uwekezaji? Toa mifano ya uwekezaji inayoleta vyote kwa pamoja.

3. Ili ufikie uhuru wa kifedha, ulipwe hata kama hufanyi kazi, lazima uwe na uwekezaji wenye faida zote mbili, shirikisha mpango wako wa kujenga na kufikia hilo kwenye miaka 10 ijayo.

Shirikisha majibu ya maswali haya kama sehemu ya wewe kujifunza, kuelewa na kwenda kufanyia kazi ili kunufaika na uwekezaji.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.