3336; Unajenga nini?
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Jinsi ambavyo binadamu tumeumbwa, hasa mikono yetu, ni kwa ajili ya kujenga vitu.
Katika kundi la wanyama, ni sisi binadamu pekee ndiyo tuna mikono inayoweza kushika zana mbalimbali na kujenga vitu.
Waweke watoto mahali na bila hata ya kuwapa maelekezo yoyote, baada ya muda mfupi utakuta kuna vitu wanajenga.
Wanaweza hata kuharibu vitu vilivyopo, ili wapate vifaa vya kujenga kile wanachotaka.
Hiyo inaonyesha jinsi ambavyo kujenga ni asili yetu.
Japo kwa asili tulikuwa tunajenga kwa kutumia mikono, bado kujenga ni kujenga, hata kama hutumii mikono yako.
Kitendo tu cha kuzalisha kitu ambacho hakikuwepo, inakupa hali ya kuridhika na kuona maisha yako yana maana.
Hivyo basi rafiki, pale unapojikuta ukiwa na msongo au hali ya kukosa mwelekeo wa maisha yako, ukijitathmini, unakuta hakuna unachojenga.
Au kama kuna kitu unajenga, kinakuwa siyo sahihi kwako, bali umeiga tu.
Maisha ya zama hizi yanatupa nafasi nyingi za kuwa watazamaji badala ya wajengaji.
Kuangalia TV, kuperuzi mitandao, kufuatilia habari na mambo ya wengine, yote hayo siyo kujenga.
Kadiri mtu unavyotumia muda wako mwingi kwenye mambo hayo ambayo hakuna kitu yanajenga kwenye maisha yako, ndivyo unavyopata msongo na kuchoshwa na maisha yako mwenyewe.
Suluhisho pekee unalohitaji ni kujenga.
Hakikisha kila wakati wa maisha yako kuna vitu unajenga.
Hakikisha kila asubuhi unayoamka una msukumo mkubwa wa kwenda kuendelea kujenga.
Hivyo ndivyo unavyoweza kufanya makubwa huku maisha yako yakiwa na maana kubwa.
Kuna vitu vingi sana vya kujenga kiasi kwamba hupaswi hata kupata muda wa kuhangaika na mambo yasiyokuwa na tija.
Kama kweli unataka mafanikio makubwa, unapaswa kuwa umetingwa na mambo unayojenga kiasi cha kukosa kabisa muda kwa mambo yasiyokuwa na tija.
Kama bado hujui nini ujenge, kuna haya matatu ambayo kila anayetaka mafanikio makubwa anapaswa kuyajenga.
Kitu cha kwanza ni kujijenga wewe mwenyewe kwa kuwa halisi kwako.
Hapa unajiendeleza wewe binafsi ili kutambua na kutumia uwezo mkubwa ulio ndani yako.
Hii inajihusisha kujifunza na kuchukua hatua ili kukua kimwili, kiakili, kiroho na kihisia.
Kila wakati unapaswa kujijenga ili kuwa bora zaidi ya ulivyokuwa awali.
Kitu cha pili ni kujenga ujuzi wa aina mbalimbali ambao unahitaji sana kwenye maisha yako.
Kulingana na kazi au biashara unazofanya, kuna ujuzi wa aina mbalimbali unaopaswa kujijengea.
Ujuzi wa kazi unayofanya, ujuzi wa mauzo, ujuzi wa kujenga biashara, ujuzi wa uwekezaji ni baadhi ya ujuzi muhimu unaopaswa kujenga.
Kila wakati endelea kuboresha ujuzi ulionao ili kufanya makubwa zaidi.
Kitu cha tatu ni kujenga mafanikio makubwa.
Kujenga mafanikio ni kuleta pamoja maendeleo yako binafsi na ujuzi ambazo umejenga.
Hapa unajenga kitu ambacho kinakuwa na manufaa kwako na kwa watu wengine.
Unaleta pamoja vitu vyote ulivyojenga na kuhakikisha haviwezi kuanguka kirahisi.
Kujenga mafanikio ni kazi endelevu, haina mwisho wala kumaliza.
Kila unapokuwa hai, unakuwa na kazi ya kufanya kwenye kuyajenga mafanikio yako.
Kama unayajenga hayo matatu, kila siku unakuwa na kazi nyingi za kufanya kiasi cha kukosa muda kwenye mambo yasiyo na tija.
Hivyo basi, kama kuna mambo yanayokusumbua, tatizo linaanzia kwenye kukosa mambo unayojenga.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, tunaletwa pamoja na ujenzi wa mafanikio makubwa.
Kila aliyepo kwenye hii jamii ametingwa sana na kujenga mafanikio makubwa kwake kiasi kwamba hahangaiki na mambo yasiyokuwa na tija kwake.
Kanuni yetu kuu ni MAARIFA + VITENDO = MAFANIKIO.
Mara zote tumetingwa na kupata maarifa na kuyaweka kwenye vitendo na mafanikio yanajidhihirisha yenyewe.
Kama hujatingwa na kujenga, KISIMA CHA MAARIFA haiwezi kuwa sehemu sahihi kwako na hutadumu ndani yake kwa muda mrefu.
Kwa sababu ujenzi haudanganyi, ni matokeo yataonekana kama unafanyika na kama hakuna matokeo basi ujenzi haujafanyika.
Kuwa mwanajamii mtiifu wa KISIMA CHA MAARIFA kwa mara zote kutingwa na ujenzi wa mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe