Habari wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO ambayo yana lengo la kutufanya kuwa wauzaji bora na kufanya mauzo makubwa. Kuwa muuzaji bora kunaanza na wewe kuwa mtu bora. Na ubora wako kama mtu unaanzia kwenye tabia ambazo unazo.
Upo hapo ulipo sasa kwa sababu ya tabia ambazo umejijengea huko nyuma. Na ili uweze kupiga hatua kubwa zaidi ya hapo ulipo sasa, lazima ujijengee tabia bora zaidi. Kuna tabia nyingi ambazo huwa zina athari kubwa kwenye mauzo, lakini moja ina nguvu zaidi kuliko nyingine.

Tabia hiyo yenye nguvu na athari kubwa kwenye mauzo na maisha kwa ujumla ni uaminifu. Mauzo huwa ni mabadilishano ya imani, wateja wanakuwa tayari kununua pale wanapokuwa na imani kwamba wanachonunua ni sahihi kwao na anayewauzia ni mtu sahihi.
Wateja wanaweza kuwa na uhitaji na kitu na hata wakawa wanamudu kukilipia, lakini wakasita kununua kama bado hawajawa na imani. Hivyo basi, ili uweze kuwa muuzaji bora na ufanye mauzo makubwa, unapaswa kujenga tabia ya uaminifu.
Muuzaji unapaswa kuwa na uaminifu usiotiliwa shaka yoyote ile. Wateja wanapaswa kukuamini wewe ni mtu sahihi kwao, rafiki yao wa kweli na ambaye unajali maslahi yao hasa. Wateja hawapaswi kuwa na chembe yoyote ya mashaka na wewe kama unataka kudumu kwenye mauzo kwa muda mrefu.
Ili kujenga uaminifu usiotiliwa mashaka, kila muuzaji anapaswa kufanyia kazi maeneo makubwa matatu.
Eneo la kwanza ni kusema ukweli mara zote.
Kama unataka kufanikiwa kwenye mauzo na kudumu kwenye mafanikio hayo kwa muda mrefu, mara zote sema ukweli. Usiseme uongo wala kuongeza chumvi kwenye mambo. Sema ukweli hata kama utapelekea ukose mauzo. Kwa sababu ukidanganya ili ukamilishe mauzo, utafanikiwa mara moja, lakini baadaye ukweli utajulikana na utakuwa umepoteza mauzo mengi ya mbele.
Huwa kuna kauli inasema unaweza kuwadanganya watu mara moja na ukanufaika, lakini unakuwa umejizuia kunufaika tena na watu hao. Kuepuka hilo, mara zote sema ukweli. Na kama kitu hujui, ni bora useme hujui kuliko kusema vitu ambavyo huna uhakika navyo na baadaye kuonekana ni mwongo.
Kama kitu unachouza hakina sifa fulani ambayo mteja anaitaka, mwambie ukweli kwamba hakika. Usimdanganye kwamba sifa hiyo ipo, akanunua halafu akaenda kuikosa, atajisikia vibaya sana na hataweza kukuamini tena.
Wateja huwa ni waelewa sana pale muuzaji anapokuwa mkweli. Wanaweza kuwa tayari kununua kitu ambacho hakina sifa zote wanazotaka, kama watashawishika muuzaji ni mkweli na mwaminifu kwao.
Tatizo la kusema uongo ni kwamba ukishaanza huwezi kuacha, kwa sababu uongo mmoja unatakiwa kufunikwa na uongo mwingine mkubwa zaidi. Hivyo kadiri muda unavyokwenda unajikuta unatumia uongo mwingi na mwisho haiwezekani tena kudanganya na ukweli unajidhihirisha.
Uaminifu unalipa sana, japo unaweza kuona unachelewa kwa kuwa mwaminifu, lakini mafanikio utakayoyapata ni makubwa na ya kudumu. Wengi ambao huwa wanapata mafanikio madogo na hayadumu, wanatumia njia zisizokuwa za uaminifu. Njia hizo huwa zina mwisho, ambao huwa siyo mzuri.
Hatua ya kuchukua; sema ukweli mara zote, ijue biashara yako kwa kina, wajue wateja wako vizuri na waeleze ukweli, watakuelewa, kukuamini na kununua kwako kwa muda mrefu.
Eneo la pili ni mara zote kufanya kilicho sahihi.
Kila unapojikuta njia panda na hujui ufanye nini, jibu ni moja tu, fanya kilicho sahihi. Fanya kile ambacho kama ungekuwa unaonyeshwa mubashara kwenye TV na watu wote wanaangalia, ungejivunia kwa kukifanya. Usifanye kitu chochote ambacho unahitaji kukificha kisijulikane, kitakuwa siyo cha uaminifu na kitakusumbua.
Ukiahidi, timiza kama ambavyo umeahidi. Usianze kutoa sababu kwa nini umeshindwa kutimiza, timiza hata kama ni kwa gharama kubwa kwako. Hakuna kitu ambacho kimewavunjia watu wengi uaminifu kama kushindwa kutimiza mambo ambayo wameahidi wao wenyewe. Kwa sababu kama umeahidi na ukashindwa kutimiza, nini ambacho unaweza? Wateja wanakosa imani na wewe pale unapoahidi na kushindwa kutekeleza.
Kuna nyakati utakutana na wateja ambao hawaijui biashara yako kama wewe unavyojua. Na hivyo wakawa wanataka kununua kitu ambacho wewe unajua kabisa hakiwezi kuwa na manufaa kwao. Kama unataka tu kufanya mauzo, utafurahi kuwauzia, kwa sababu si wametaka wenyewe? Lakini wanapoenda na kugundua hawakufanya maamuzi sahihi, watakosa imani na wewe. Ni wajibu wako kuwashauri wateja wako vizuri, hata kama hilo litapelekea wewe usiwauzie kwa wakati huo, lakini litakujengea kuaminika ambapo utauza zaidi baadaye.
Kuna mambo mengi sahihi unayojua unapaswa kuyafanya kama muuzaji, hakikisha unayafanya mara zote ili kujenga uaminifu na wateja wako. Hata pale unapoona kuna fursa ya kujinufaisha zaidi na wateja kuumia, usifanye hicho.
Hapa ishi kanuni ya dhahabu ambayo inasema; watendee wengine kile ambacho ungependa wakutendee. Chochote ambacho unataka kukifanya kwa mteja, jiulize kama wewe ndiyo ungekuwa mteja na muuzaji akakufanyia hivyo, ungefurahia na kumwamini zaidi? Kama majibu ni hapana, basi usifanye.
Hatua ya kuchukua; Kabla ya kufanya kitu chochote, jiulize kama hicho ndiyo kitu sahihi kabisa kwako kufanya, kama ndiyo fanya, kama siyo usifanye.
SOMA; Matumizi Bora Ya Mwili Ili Kufanikiwa Kwenye Mauzo.
Eneo la tatu ni kuwa na mwonekano unaoaminika.
Pata picha umeenda hospitalini unaumwa, unaingia kwenye chumba cha daktari na unamkuta hajachana nywele, amevaa mapete makuba kwenye vidole, macheni mengi shingoni na anavuta sigara. Utakuwa na imani kiasi gani ya kumweleza daktari huyo matatizo yako na kutumia matibabu atakayokupa? Unaona dhahiri hapo kuna namna mwonekano wa daktari utapunguza imani yako kwake na hivyo kutokuzingatia matibabu yake.
Hivyo pia ndivyo wateja wako wanavyokupima kwa mwonekano wako. Kitu cha kwanza ambazo mteja ananunua kabla hajanunua unachouza ni wewe. Yaani mteja anakununua kwanza wewe kabla hajanunua unachouza. Mteja inabidi akukubali kwanza wewe kabla hajakubali unachomshawishi.
Kwa sababu hiyo basi, unapaswa kuwa na mwonekano nadhifu na ambao utawafanya wateja wakuamini na kukubaliana na wewe. Hilo linaanza na usafi wako binafsi, kuanzia mwili mpaka mavazi. Nywele zako zinapaswa kuwa vizuri, mwili, kucha na vingine. Pia unapaswa kuvaa mavazi safi na nadhifu, kama muuzaji kuwa na sare ya mauzo ambayo unaivaa na kuhakikisha ipo kwenye hali ya usafi mara zote.
Kuna eneo moja ambalo wauzaji wengi huwa wanalisahau na linaathiri sana mwonekano wao. Eneo hilo ni viatu, kile unachovaa kwenye miguu yako kinapandisha au kushusha sana thamani yako. Pale unapowauzia wateja ambao wanakuona mpaka miguuni, mara zote vaa viatu vinavyofunika miguu hasa kwenye vidole. Kuvaa viatu vya wazi na hasa ambavyo ni vya thamani ya chini kama ‘yeboyebo’ inawafanya wateja wasikupe uzito mkubwa sana.
Changamoto ya mwonekano ni kwamba wateja hawatakuambia kwamba hawakuamini kwa sababu ya mwonekano, ila kisaikolojia tu hawatakuwa tayari kukubaliana na wewe. Yaani wanaanza kukuzima kisaikolojia kabla hawajakuzima kwenye mauzo. Hivyo hakikisha mara zote unakuwa na mwonekano unaowafanya watu kujisikia vizuri kuwa karibu na wewe.
Hatua ya kuchukua; unapokuwa kwenye mauzo, kuwa nadhifu kwa kuwa msafi na kuvaa sare safi za mauzo pamoja na viatu vya kufunika miguu.
Mambo haya uliyojifunza unaweza kuona ni ya kawaida, lakini athari zake ni kubwa sana kwenye mauzo. Hakikisha unayazingatia ili ujenge kuaminika na wateja kwa kuwa muuzaji bora na mwaminifu, kitu ambacho kitapelekea ufanye mauzo makubwa zaidi.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.