3338; Maana halisi ya kuwa tofauti.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Ushauri wa kuwa tofauti ili uweze kufanikiwa umekuwa unatolewa mara nyingi.
Lakini umekuwa ukitolewa kijumla sana kiasi kwamba watu wengi hawaelewi nini maana halisi ya kuwa tofauti.

Watu wamekuwa wanajaribu kufanya vitu vya tofauti na wengine, lakini vinakuwa ni vitu visivyo na tija na hivyo havileti tofauti yoyote kwao kimafanikio.

Ili kuwa tofauti na kupata mafanikio makubwa, ni lazima tuelewe vyema huo utofauti ni upi hasa.
Utofauti lazima uwe na tija kimafanikio.
Siyo tu kuwa tofauti kwa sababu ya kuwa tofauti, bali kuwa tofauti kwa sababu ina tija.
Kwa mfano hupaswi kutembea kwa kutumia mikono kwa sababu unataka kuwa tofauti na wengine wanaotembea kwa kutumia miguu.
Ukifanya hivyo utakuwa tofauti, lakini ni tofauti ambayo haitakuwa na tija.

Kanuni yetu kuu ni MAARIFA + VITENDO = MAFANIKIO.
Ni kwenye kanuni hiyo ndiyo penye fursa ya kuwa tofauti na kujenga mafanikio makubwa.
Tofauti hiyo unaileta kwenye sehemu mbili za kanuni.

Moja ni kwenye MAARIFA, unapaswa kujifunza yale ambayo hayafundishwi shuleni.
Pamoja na uwepo wa maarifa mengi na urahisi wa kuyapata, bado wengi hawaweki uzito kwenye maarifa yasiyofundishwa shuleni.
Hivyo unakuta kundi kubwa la watu linajua na kuamini yale tu waliyofundishwa shuleni.
Ukiwa na maarifa zaidi ya hayo na yanayokupa mwanga zaidi ya wengine, utakuwa tofauti kabisa na hao wengine.

Mbili ni kwenye VITENDO, unapaswa kufanya yale ambayo wengine hawawezi kuyafanya.
Hapa unafanya kwa upekee ambao haupo kabisa, ambao unakuweka kwenye nafasi ya kupata matokeo ambayo wengine hawayapati.
Wengi huwa wanafanya vitu kwa kuwaiga wengine, hivyo wewe anza kwa kutokuiga kabisa.
Lakini pia unachofanya, hakikisha inakuwa vigumu kwa wengine kuweza kuiga. Na hilo linawezekana kama utatumia uwezo wa kipekee na vipaji tofauti ulivyonavyo.
Kuna muunganiko wa tofauti kabisa ambao unao, kuanzia maarifa uliyopata, ujuzi na uzoefu na uwezo na vipaji. Ukileta hivyo pamoja, utaweza kufanya kitu ambacho hakuna mwingine anayeweza hata kukukaribia.

Kwa kuweka mkazo kwenye maeneo hayo mawili, kujifunza yasiyofundishwa shuleni au waziwazi na kufanya yasiyoweza kufanywa na wengine ndiyo utaweza kuzalisha matokeo makubwa na ya tofauti kabisa na wanavyozalisha wengine.
Hilo litakupa wewe mafanikio makubwa sana ambayo hayana ushindani wa moja kwa moja.

Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, hii ndiyo nguzo kuu.
Tunaiishi kanuni ya MAARIFA + VITENDO = MAFANIKIO kwa uhalisia kabisa.
Tunapata maarifa adimu na ya msingi, ambayo kwa wengine ni vitu vigeni kabisa.
Na tunachukua hatua za tofauti mara zote, tofauti na hata tulivyofanya sisi wenyewe.
Muunganiko huo unatupa mafanikio makubwa na ya uhakika kabisa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe