Mpendwa muuzaji bora kuwahi kutokea,

Ikiwa leo ni jumamosi ya ushawishi tunaongozwa na kauli mbiu inayosema HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.

Leo tunakwenda kujifunza njia namba nne ya kuwafanya watu wakukubali ambayo ni kuwa msikilizaji mzuri.

Usikilizaji ni moja ya sanaa iliyosaulika sana kwenye mauzo na ina miujiza kwenye mauzo. Kama ni njaa ambayo watu wengi wanayo katika zama hizi za ujuaji basi ni usikilizaji.

Watu wana njaa ya kusikilizwa ndiyo maana watu wengi wanaoendesha huduma za maombi wanapata wateja kwa sababu wanatenga muda wa kuwasikiliza, wanaacha watu wajieleze wao wenyewe kuondoa kile ambacho kipo ndani yao.
Wakati mwingine hata wewe unakua na vitu vinavyokusumbua na unajikuta unamtafuta mtu umwambie mtu na akusikilize na baada ya hapo unakuwa sawa.

Njia rahisi ya kuwashawishi watu kukubaliana na wewe ni kuwa msikilizaji mzuri na kuwapa wengine nafasi ya kujieleza kuhusu wao.

Watu huwa wanathamini sana kile wanachokiongea, na unapoonesha kukithamini kwa kusikiliza vizuri, wataona unawajali na hivyo kuwa tayari kukubaliana na wewe.

Wewe kama muuzaji, kuwa msikilizaji mzuri kwa wateja wako na wote unaojihusisha nao kwa kuweka umakini wako wote kwa yule anayeongea, huku ukimwangalia usoni na kuonesha ishara kwa lugha ya mwili kwamba unamsikiliza.

Unapokua na mteja, mfanye yeye ndiyo aongee zaidi. Utawezaje hili? Ni kwa kumuuliza maswali yanayompa nafasi ya kujieleza zaidi na hilo litamfanya mtu akubaliane na wewe.

Kwa mfano, hata kama mtu anaongea kwa hasira, anakosoa, na kutoa maneno makali, unapotoa nafasi ya kumsikiliza ,yeye mwenyewe anakuwa mtulivu na kuongea vizuri.

Mwanasaikolojia Sigmund Freud ni mmoja wa watu ambao walikuwa wasikilizaji wazuri sana.
Kuna mtu mmoja alifanikiwa kukutana na mwanasaikolojia Sigmund Freud anaeleza kwamba, anasema hajawahi kuona mtu mwenye umakini mkubwa kama wake. Na usikilizaji wake ulimshangaza kiasi kwamba hawezi kumsahau kamwe.
Anasema wakati wote anaongea naye, aliweka umakini wake wote kwake, alimwangalia na sauti yake ilikuwa ya chini huku akiwa hana kingine anachofanya.

Wewe kama muuzaji unapaswa kumsikiliza mteja huku ukiwa huna kitu kingine unachofanya.
Unapoongea na mteja, acha kila ulichokuwa unafanya na msikilize bosi wako kwa umakini mkubwa. Kuongea na mteja huku ukiendelea na mambo yako mengine kama kushika simu ni dharau kwa mteja wako.

Kama unataka watu wakukwepe na kukudharau, usiwe msikilizaji, kila wakati taka kuongea wewe na pale anapoongea usisubiri amalize, wewe mkatishe na sema kile unachofikiri.

Kwenye mauzo kuwa msikilizaji mzuri, na kumwonesha mwingine kujali na kuthamini kile anachosema kwa kumpa umakini mkubwa.

Kusikiliza kwa MAKINI, ni sanaa iliyosaulika sana lakini yenye nguvu kubwa sana ya ushawishi.
Watu wengi ni waongeaji sana, kitu kinachowazuia wasiweze kuwajua wengine na kuwashawishi.

Mwandishi wa kitabu cha How I Raised Myself from Failure to Success in Selling anasema kwamba, shirika moja kubwa liliwahi kuandika ujumbe huu kwa watu wake wa mauzo;

“Unapoangalia maigizo, angalia jinsi waigizaji wanavyosikiliza kwa makini. Ili uwe mwigizaji mzuri, lazima uwe msikilizaji mzuri pia. Pale unapokuwa msikilizaji mzuri, yule anayeongea anavutiwa kuendelea kujieleza zaidi kitu kinachokupa nafasi ya kuwajua kwa undani. Hilo litakupa nafasi ya ushawishi, kwani hata kabla hujamwambia mtu kitu, kwa jinsi ulivyomsikiliza, anakuwa tayari ameshashawishika na wewe”

Muuzaji bora kuwahi kutokea, kusikiliza kwa makini ni sanaa ambayo ina nguvu kubwa siyo tu kwenye mauzo bali hata kwenye mahusiano yote ya watu.

Hatua ya kuchukua leo;

Moja, kuwa msikilizaji mzuri na makini.

Mbili, uliza maswali ambayo yatampa mtu nafasi ya kujieleza zaidi.

Tatu, kama mtu anaongea na kuna kitu unataka kuongeza, subiri amalize kuongea ndipo ueleze kitu hicho, usimkatishe mtu akiwa anaongea.

Nne, usisikilize huku ukiwa unachezea simu au kufanya kitu kingine. Acha yote unapoongea na mtu.

Kitu kimoja zaidi, watu huwa wanathamini sana kile wanachoongea, ukikithamini kwa kuwa msikilizaji mzuri, watakuwa tayari kukubaliana na wewe.

Mwisho, kuwa msikilizaji mzuri na unayejali , itaongeza sana ushawishi wako kwa wengine.

Kutoka kwa muuzaji mwenzako, rafiki anayekupenda na kukujali,

Mwl.Deogratius Kessy

Mwalimu/Mwandishi/Mkufunzi wa mauzo.
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz