Rafiki yangu katika mauzo,
Kila siku usiache kujiambia kwamba wewe ni muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea.
Usisubiri mtu mwingine akuambie bali jipe cheo hicho wewe mwenyewe na akili yako ya ndani itaanza kufanyia kazi hilo.

Mpendwa muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea, kabla hatujaendelea na somo letu la leo tujikumbushe kidogo tulichojifunza kwenye somo la nne(04).
Tulijifunza kwamba njia pekee ya kuwa na mazungumzo mazuri na kuwafanya watu wakukubaliane na wewe ni kuwa msikilizaji mzuri. Thamini kile wanachoongea kwa kuwa msikilizaji mzuri na watakua tayari kukubaliana na wewe.

Kwenye njia ya tano ya kuwafanya watu wakukubali kwenye kila eneo la maisha yako ni ; Ongelea kile ambacho mtu anapendelea.

Njia nyingine ya kuwafanya watu wakubaliane na wewe ni kuongelea yale ambayo mtu anayapendelea.

Kila mtu kuna kitu anapendelea zaidi, inaweza kuwa vitabu, michezo, siasa, na mengine. N katika mambo hayo kila mtu ana upande wake.
Na watu huwa wanathamini sana upande ambao wapo.

Mtu anapogundua kwamba uko upande wake, anaona unamthamini na hivyo atakuwa tayari kukubaliana na wewe.

Kwa mfano, aliyekuwa raisi wa marekani Roosevelt alikuwa na utaratibu wa kujifunza kuhusu kile ambacho mtu anayekwenda kukutana naye anakipendelea.

Kama kesho anakutana na mtu anayependa mchezo wa mpira wa miguu, basi alitumia usiku kabla ya mkutano kujifunza kuhusu mpira ili kesho yake awe na njia uhakika ya kuingia kwenye moyo wa mtu ni kuongelea vile anavyovithamini.

Hatua ya kuchukua leo;

Jijengee utaratibu huu kama Raisi Roosevelt, kwa kila unayetaka kukutana naye awe ni mteja au siyo jua ni vitu gani anavyopendea na kisha jielimishe katika yale ya msingi kwenye vitu hivyo na katika mazungumzo yenu weka kipaumbele kwenye vitu hivyo.

Na kwa kuwa watu wanapenda kujieleza, huhitaji kujua kwa kina, kwani ukimuuliza swali na kuonesha una nia ya kujifunza atakua tayari kukueleza kwa kina.

Kitu kimoja cha kuondoka nacho ni ukitaka watu wakukubaliane na wewe na kuteka mioyo yao, ongelea yale ambayo mtu anapendelea na utaweza kuwateka.

Kwenye mauzo, kuwa upande wa wateja, ongelea yale ambayo mtu anapenda kusikia. Kwa mfano, wewe kama muuzaji hutakiwi kuwa upande wa timu fulani, kuwa timu ya mteja wako, na muunge mkono kwenye hoja yake ili upate kile unachotaka.

Kutoka kwa muuzaji mwenzako, rafiki anayekupenda na kukujali,

Mwl.Deogratius Kessy

Mwalimu/Mwandishi/Mkufunzi wa mauzo.
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz