Rafiki yangu mpendwa,
Maisha ni safari ya magumu, changamoto na vikwazo mbalimbali. Siku uliyozaliwa ulilia na utaendelea kulia kwa kipindi chote cha maisha yako. Hili ni jambo ambalo wengi huwa hawalijui, hivyo wanakuwa na matumaini hewa.
Matumaini hewa ambayo wengi wanakuwa nayo ni kudhani wakishapiga hatua fulani, basi wametengana kabisa na mateso ya maisha. Lakini hivyo sivyo inavyokuwa. Kwani kwenye kila hatua ya maisha, kuna mateso yake.

Mtu akiwa mtoto anaona akikua basi ataachana na mateso ya maisha, asichojua ni akikua anakaribisha mateso ya utu uzima. Mtu anadhani akipambana na kutoka kwenye umasikini atakuwa ameachana kabisa na mateso ya maisha. Anachokuja kushangaa ni mateso ya utajiri anayokuja kukutana nayo akishakuwa tajiri.
Hivyo basi rafiki, kwa kuwa mateso ni sehemu ya maisha, haina maana kujaribu kuyakwepa au kuyalalamikia. Badala yake tunapaswa kuangalia namna ya kuyatumia vizuri ili kuweza kufanya makubwa licha ya mateso tunayokuwa tunapitia.
Kila mmoja wetu anapaswa kuyafanya mateso yake yawe na maana kubwa kwenye maisha yake. Anapaswa kuwa na sababu kubwa ya kwa nini ateseke na kupitia yale anayopitia. Kama mtu hana kwa nini kubwa ya kufanya kitu, atakata tamaa na kuishia njiani.
Je wewe ni KWA NINI ipi kubwa inayokusukuma ufanye yale unayofanya? Ni kwa nini uendelee kuteseka kwa yale unayopitia sasa? Haya ni maswali ambayo unapaswa kuwa na majibu yake ndiyo maisha yako yaweze kuwa na maana. Uendelee kuweka juhudi licha ya changamoto utakazoendelea kukutana nazo.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimekushirikisha jinsi ya kuyageuza mateso unayopitia kuwa maana ya maisha yako. Ni pale mateso yanapokuwa na maana kubwa ndiyo yanaacha kukuumiza na yanakuwa kitu kinachokusukuma kufanya makubwa zaidi. Karibu uangalie kipindi, ujifunze na kwenda kuchukua hatua ili mateso yako yawe na tija kwako.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.