3350; Mapenzi na fedha.
Kutoka mezani kwa Kocha.
Rafiki yangu mpendwa,
Kuna sababu mbili pekee za kukusukuma wewe kufanya kitu chochote kile; mapenzi na fedha.
Unafanya kitu kwa sababu unakipenda au kwa sababu kinakuingizia fedha.
Lakini sasa, hapo kuna tahadhari muhimu ambazo unapaswa kuwa nazo.
Kuna vitu ambavyo utakuwa hupendi kufanya na havikuingizii fedha. Hivi unatakiwa uvifute kabisa kwenye maisha yako, yaani uachane navyo kwa sababu havina manufaa yoyote kwako.
Kuna vitu ambavyo utakuwa unapenda kufanya, lakini havikuingizii fedha. Hivi unapaswa kuwa navyo kwa udogo wana, kama sehemu ya wewe kuondoa msongo unaotokana na mengine unayokuwa unapitia.
Kuna vitu ambavyo utakuwa hupendi kufanya, lakini vinakuingizia fedha. Hivi unapaswa kuwa navyo na kwa muda mfupi ili kujijengea msingi imara kifedha. Muhimu ni fedha unayokuwa unaingiza iwe kubwa sana kufidia ile hali ya kutokupenda kitu unayokuwa nayo. Hakikisha kufanya hivi haiendi kwa maisha yako yote, inapaswa kuwa kwa kipindi fulani tu ili kuweka misingi ya kifedha sawa na kuwa huru kufanya yale unayopenda.
Kuna vitu ambavyo utakuwa unapenda kufanya na vinakuingizia fedha. Hapa ndiyo pazuri na ambapo unapaswa kupajenga kwa maisha yako yote. Pale unapofanya unachopenda na kulipwa kupitia hicho unakuwa kwenye njia nzuri sana ya kujenga mafanikio makubwa. Unakuwa na nguvu kubwa ya ushindani, ambayo wengine hawawezi kuiiga na kukuzidi.
Hapa ndiyo pa kujenga kwa maisha yako yote, kuhakikisha yale unayopenda sana kufanya ndiyo pia yanayokuingizia kipato kikubwa.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, nguvu kubwa tunaweka kwenye kujenga kile tunachopenda zaidi kufanya kuwa ambacho kinatulipa zaidi pia.
Kwenye safari ya maisha tunaanza na kufanya tusiyopenda ila yanatulipa.
Kufanya hayo kwa kipindi fulani hakuna ubaya. Lakini kwenye hicho kipindi tunatakiwa kuwa tunajenga tunachopenda kufanya na kulipwa fedha kukifanya.
Wajibu wako ndani ya jamii ya KISIMA CHA MAARIFA ni kuhama kutoka kufanya usivyopenda kufanya na kwenda kwenye kufanya vile unavyopenda kufanya.
Hilo ni zoezi ambalo ukikamilisha kulifanya, unakuwa umejijengea nguvu kubwa sana ya kufanikiwa na ambayo haiwezi kushindwa na yeyote.
Kwa sababu wakati wengine wanaona ugumu kufanya yale wanayopaswa kufanya, kwako inakuwa ni kama mchezo tu.
Pale kile ambacho kwa wengine ni kazi ngumu, ila kwako ni mchezo, ndipo penye nguvu kubwa ya ushindani.
Pambana kujenga hilo na hakuna kitakachoweza kukuzuia.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe