3351; Kuwa asiyevurugwa.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Watu wanaokuzunguka, tayari wanakujua vizuri na wanajua namna bora ya kupata chochote wanachotaka kutoka kwako.
Njia rahisi kabisa wanayoitumia ni kukuvuruga. Wanajua ni vitu gani huwa vinakukasirisha kwa haraka na hivyo kuvitumia hivyo kukuvuruga.
Wanajua ukishavurugwa unafanya maamuzi yasiyo sahihi na wao kunufaika na maamuzi hayo.
Unaweza usiamini hili, lakini jua kabisa kwamba chochote kinachokukasirisha na kukuvuruga haraka, wengine huwa wanakitumia kupata kile wanachotaka kutoka kwako.
Wanakufanyia kwa makusudi yale ambayo yatakuvuruga na kukukasirisha ili uchukue hatua ambazo zitawanufaisha wao.
Kuna watu wanakutega kupitia kukasirika na kuvurugwa kwako ili ukosee halafu wao wanufaike.
Kama unataka kuwa bora mara 10 ya ulivyo sasa, kukamilisha mara 10 ya yale unayokamilisha sasa na kutajirika mara 10 zaidi ya utajiri ulionao sasa, siri ni moja tu; kuwa asiyevurugwa.
Bila ya kujali chochote kinachokutokea, jidhibiti sana usiwe na hasira wala kuvurugwa.
Kuwa na utulivu mkubwa kwenye mambo yote na fikiri kwa kina kabla ya kufanya maamuzi na kuchukua hatua ya aina yoyote ile.
Acha kiburi na ufahari unaojipa na uwe mnyenyekevu, mengi yanayokukasirisha yatakosa nguvu kabisa.
Kiburi kina tabia ya kukuza mambo hata kama ni madogo na kuyafanya kuwa makubwa.
Ukiacha kiburi na ufahari, utaweza kupuuza mambo mengi ambayo yamekuwa yanakuvuruga kirahisi.
Usiwe mtu wa kulipuka hisia kwa haraka. Na pale unapokuwa na hisia zozote kali, usiamue wala kufanya chochote. Jipe muda, hisia hizo zitashuka na utaweza kufikiri kwa usahihi zaidi.
Mara zote hisia zinapokuwa juu, kufikiri kunakuwa chini na maamuzi yoyote unayofanya yanaishia kukuumiza zaidi.
Kwa kuwa na subira, utajipa nafasi ya kutuliza hisia ili zisikuvuruge.
Jikubali na jiamini sana wewe mwenyewe kiasi kwamba huhitaji wengine wakukubali ndiyo ujione umekamilika.
Jione tayari umekamilika hata kama wengine wanakuambia tofauti na hilo.
Usitegemee wengine ndiyo ujione umekamilika.
Kwani wale utakaowategemea kujiona umekamilika, ndiyo unakuwa umewapa nguvu ya kukuvuruga pale watakapokuonyesha kwamba hujakamilika.
Muhimu zaidi ni usiweke uzito mkubwa kwenye sifa unazopewa, kama hutaki ukosoaji ukuumize.
Kwa sababu wale wanaokusifia leo, ndiyo hao hao watakaokukosoa kesho.
Kama utaweka uzito kwenye sifa zao, lazima ukosoaji wao utakuumiza na kukuvuruga.
Lakini kama utapuuza sifa zao na kuendelea kufanya mambo yako, utaweza pia kupuuza ukosoaji wao na kufanya mambo yako.
Kuwa mgumu sana kuvurugwa kiasi kwamba hakuna mtu anayeweza kukutega na kujinufaisha kupitia wewe.
Watu wameshazoea kuchezea hisia zako kupata yale wanayotaka, wazuie kwenye hilo kwa kuzingatia haya uliyojifunza hapa.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, tunakuwa na ngozi ngumu sana kiasi kwamba hakuna kinachotubabaisha.
Yale yanayowavuruga watu wa kawaida, kwetu tunayacheka na kuyapuuza.
Tunafanikisha hayo kwa kujiamini sisi wenyewe na kukaa kwenye mchakato sahihi wa safari ya mafanikio mara zote.
Kitu kikubwa tunachoamini ni mchakato, hivyo bila ya kujali nini kinaendelea au kimetokea, tunarudi kwenye mchakato wetu.
Tunaamini sana kwenye mchakato wetu kiasi kwamba hakuna kingine chochote kinachoweza kutuvuruga.
Hata tupate matokeo ya aina gani, tunarudi kwenye mchakato wetu.
Hata wengine watufanyie nini, tunarudi kwenye mchakato.
Tunachojua ni kwa kufuata mchakato kwa usahihi na msimamo, inatuepusha na makosa mengi yanayowanufaisha wengine.
Kwa kukazana mara zote kukaa kwenye mchakato wetu sahihi na kuisimamia misingi yetu, tuna uhakika wa kuwa bora mara 10 zaidi, kukamilisha mara 10 zaidi na kutajirika mara 10 zaidi.
Ni kwa kusimamia mchakato na misingi yetu mikuu ndiyo tunapata uhakika wa hayo yote.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe