Rafiki yangu mpendwa,

Maisha kwa ujumla yana vikwazo na changamoto mbalimbali. Sehemu kubwa ya changamoto hizo huwa inaanzia kwa watu, hasa wale ambao tunakuwa nao karibu.

Maisha ya kupambania mafanikio, yanafanya vikwazo na changamoto kuwa kubwa zaidi. Na sehemu kubwa ya changamoto hizo ni kukwamishwa na watu wa karibu, ambao tunakuwa tunawahitaji sana kwenye hiyo safari ya mafanikio.

Tunapokuwa tunaanza safari ya mafanikio, wale wa karibu yetu huwa wanakuwa ni watu wa kututia moyo tuendelee na safari hiyo. Jambo hilo huwa linatupa sana faraja kwa kuona wanaotuzunguka wapo pamoja na sisi.

Lakini mambo huanza kubadilika pale unapoanza kupata mafanikio ambayo umeyapambania sana. Kadiri unavyozidi kufanikiwa, ndivyo mahusiano yako na watu wako wa karibu yanavyozidi kudhoofika. Watu hao wanaanza kuona mafanikio yako yakiwa kikwazo kwao.

Kwa kifupi ni kwamba, watu wako wa karibu, wanataka ufanikiwe, lakini siyo ufanikiwe sana kuwazidi wao. Wanataka mafanikio yenu yawe yanalingana, ili muwe sawa. Ni pale unapowazidi mafanikio wale wanaokuzunguka ndipo changamoto zinapoanza kuwa kubwa.

Utakosolewa, kupingwa na hata kusalitiwa, hiyo yote ikiwa ni juhudi za kukuzuia usipate mafanikio makubwa kuliko wale wanaokuzunguka. Kwa bahati mbaya sana, hili huwa linatokea bila hata ya wahusika kujua. Yaani wale wanaokukwamisha hawajui kama wanafanya hivyo na wewe unayekwamishwa hujui kama unakwamishwa.

Matokeo yake ndiyo tunaona watu walio kwenye eneo moja wanafanana kwa mambo mengi. Angalia watu wanaoishi eneo moja, wanaofanya kazi au biashara ya aina moja na wanaotumia muda mwingi pamoja, wengi utakuta wanafanana kwenye mafanikio yao. Aina ya nyumba, magari, hata idadi ya watoto. Unaweza kudhani ndiyo kiasi ambacho wameweza, lakini nataka nikuambie kuna nguvu kubwa inawazuia wenye kutaka kwenda juu zaidi ya hapo washindwe.

Rafiki, ndiyo maana nimekuwa nasema, marafiki zetu ni watu wazuri sana, wenye nia njema kwetu. Lakini inapokuja kwenye mafanikio makubwa, huwa wanakuwa kikwazo, hapo wanageuka maadui ambao wanatuzuia tusifanikishe, kwa sababu wanataka tuendelee kufanana nao.

Hivyo basi, inapokuja kwenye mafanikio, unahitaji kuwa na rafiki ambaye hawezi kukukwamisha wala kukusaliti hata iweje. Rafiki ambaye atayafurahia mafanikio yako na kukusukuma upate mafanikio zaidi. Rafiki ambaye ataendelea kumbatana na wewe muda wote na kamwe hatakuacha.

Kwa bahati mbaya sana, rafiki huyo ni mmoja tu na hujamjua na kumpa nafasi ambayo anastahili kuipata. Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimekuonyesha rafiki huyo na jinsi unavyoweza kujenga naye mahusiano mazuri na kunufaika zaidi kupitia yeye.

Karibu uangalie kipindi hicho hapo chini, umjue rafiki sahihi kwako, ujenge naye mahusiano mazuri na uweze kupata mafanikio makubwa na yasiyokuwa na ukomo.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.