Rafiki yangu mpendwa,

Ni mara ngapi unakuwa umepanga kuamka asubuhi na mapema ili kuweza kuanza siku yako kwa ushindi mkubwa. Kuhakikisha unawahi kweli kuamka, unaweka kabisa alamu kwenye simu yako, ili muda unapofika ikuamshe. Kweli muda unafika, alamu inaita, halafu kinachofuata ni nini? Unaizima alamu na kujiambia wacha nimalize usingizi kwa dakika 5 tu halafu nitaamka. Ukija kushtuka kumeshakucha kabisa na umechelewa kuamka.

Kila mmoja wetu ameshapitia hali za aina hiyo mara nyingi sana kwenye maisha yake. Vipi kama leo nikikuambia ipo dawa ya kuondokana kabisa na hali hiyo, dawa ambayo itakomesha kabisa hilo na kukuwezesha kuamka asubuhi na mapema na kuwahi kwenye mambo yako? Habari njema ni dawa hiyo na unaweza kutumia kabisa.

Rafiki, hebu pata picha pale muda wa kuamka asubuhi unajiambia maneno haya; “Naamka kwenye kufanya kazi ambayo ni binadamu tu anaweza kuifanya. Nawezaje kusita na kulalamika wakati nakwenda kufanya kazi ambayo nilizaliwa kuifanya? Je nimeletwa hapa duniani kulala kwenye blanketi lenye joto? Angalia miti, ndege, nyuki na viumbe wengine, wote wanakazana kufanya kazi zao, ambazo wameumbwa kufanya. Kwa nini mimi nisite kufanya kazi ambayo ndiyo wajibu wangu?”

Rafiki, hiyo ni kauli ambayo Mstoa Marcus Aurelius aliiandika kwenye kitabu cha tano kwenye andiko lake la Meditations. Marcus alikuwa anajisukuma kuachana na uvivu unaomzuia kuamka asubuhi na kwenda kutimiza majukumu yake.

Hivyo pia ndivyo na sisi tunavyoweza kutumia mbinu hiyo ya falsafa ya Ustoa kuvuka uvivu na kuweza kufanya makubwa kwenye maisha yetu. Kwa sababu kwa asili, sisi binadamu ni wavivu, huwa hatupendi kuumia au kuchoka, tunataka kupata vitu kwa urahisi, jambo ambalo siyo sahihi.

Ili kutumia falsafa ya Ustoa kushinda uvivu, yafuatayo ni ya kujikumbusha kila siku;

Moja ni haupo hapa duniani kuzurura na kustarehe tu. Upo hapa duniani kwa sababu kuna wajibu ambao umekuja kuutimiza. Una kazi umepewa ya kuhakikisha dunia inakuwa bora kupitia yale unayofanya. Kukwepa kazi hiyo ndiyo imepelekea wengi kuwa na maisha ya hovyo na yaliyokosa maana.

Hatua ya kuchukua; Jua kusudi la wewe kuwa hapa duniani, siyo tu wewe unapata nini, bali wengine wananufaikaje na uwepo hapa duniani. Halafu kila unapopata uvivu wa kutekeleza majukumu yako, angalia jinsi ambavyo unawakwamisha wengine wanaotegemea kile unachofanya.

Mbili ni muda wako hapa duniani ni mfupi sana. Mara nyingi unakuwa na uvivu kwa kuona muda bado upo. Umepanga kufanya kitu leo, lakini muda wa kufanya ukifika unajiambia utafanya kesho. Kama vile hiyo kesho una uhakika nayo. Ukweli ni kwamba muda wetu hapa duniani ni mfupi sana, kutokutimiza majukumu yako kwa wakati ni kujiweka kwenye hatari ya kutokuyatimiza kabisa.

Hatua ya kuchukua; Kila unapopatwa na uvivu wa kufanya yale uliyopanga, jikumbushe kwamba muda wako hapa duniani ni mfupi sana. Kila unapojiambia unataka kupumzika, jikumbushe ukishaondoka hapa duniani utapumzika sana. Tumia muda mchache ulionao kukamilisha yote muhimu.

Tatu ni mara zote kufikiri na kufanya yaliyo sahihi bila ya kujali wengine wanafikiria, kusema au kufanya nini. Mara nyingi sana tumekuwa tunakwamishwa na maoni ya wengine, kama vile hiyo ndiyo sheria. Maoni ya wengine ni maoni tu na siyo sheria ambayo wewe unapaswa kuifanyia kazi. Wajibu wako ni kufanya yale ambayo ni sahihi kwako na kuyasimamia bila ya kujali wengine wanakuchukuliaje. Utaweza kufanya makubwa sana ukiacha kuhangaika na maoni ya wengine ambayo hayana manufaa kwako.

Hatua ya kuchukua; Jua kile hasa unachotaka kwenye maisha yako na pambania kukipata hicho. Wapuuze wengine wote wanaotoa maoni ya kukukwamisha kwenye hayo uliyochagua. Tingwa na kufanya yale yaliyo sahihi kiasi kwamba hutoi nafasi kwa wengine kukuvuruga.

Tukiweza kufanya haya matatu tuliyojifunza hapa, tutaweza kuondokana kabisa na uvivu na kuweza kufanya makubwa kwenye maisha yetu kitu ambacho kitatupa mafanikio makubwa na kuifanya dunia kuwa sehemu bora zaidi.

Yapo mengine ya kukusaidia kushinda uvivu na kufanya makubwa kutoka kwenye falsafa hii ya Ustoa, nimeyafafanua kwa kina kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini. Fungua kipindi ujifunze na kuendelea kuwa bora.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.