Rafiki yangu mpendwa,

Tofauti kubwa kati yetu sisi binadamu na viumbe wengine waliopo hapa duniani ni uwezo wa kufikiri tuliopewa na mikono ya kufanya kazi.

Wanyama wengine huwa wana ubongo, lakini hawafikiri kama sisi, badala yake wanayaendea maisha yao kwa mazoea ambayo tayari yapo ndani yao.

Lakini pia miguu yao ya nyuma na ya mbele, imeumbwa kwa ajili ya kutembea na kushikilia vitu, lakini siyo kufanya kazi.

Ni sisi binadamu ndiyo tunaoweza kufikiri mambo kwa utofauti kwa kutumia akili zetu na kuyabadili kwa kutumia mikono yetu. Na hivyo ndivyo tumeweza kuifanya dunia kuwa sehemu bora zaidi ya kuishi.

Pamoja na uwezo huo mkubwa ulio ndani yetu, wa akili ya kufikiri na mikono ya kufanya kazi, bado watu wengi wamekuwa wanashindwa kutumia rasilimali hizo vizuri. Matokeo yake ni wanaishia kuwa na maisha duni na kukosa vile ambavyo wanataka.

Falsafa ya Ustoa ni falsafa ambayo inatuongoza sisi binadamu kurudi kwenye asili yetu, kuweza kutumia fikra zetu vyema na kuchukua hatua ili kuifanya dunia kuwa sehemu bora zaidi ya kuishi.

Wakati falsafa nyingi huwa ni za kujadiliana na kubishana kuhusu maana ya maisha na maswali mengine magumu, Ustoa ni falsafa ya vitendo, unayowaongoza watu nini wafanye ili kuwa na maisha bora.

Na moja ya vitu ambavyo falsafa ya Ustoa inasisitiza sana watu kufanya ili kuwa na maisha bora ni KAZI. Ustoa unaipa kazi heshima kubwa, kwa sababu ndiyo wajibu ambao tupo hapa duniani kuutimiza. Falsafa hii inasisitiza kwamba wakati tupo hapa duniani, tunao wajibu wa kuifanya dunia kuwa bora kupitia yale tunayofanya.

Ili kuweza kufanya kazi na kuwa na mchango kwenye dunia, tunapaswa kujijengea NIDHAMU KALI ya kazi na kuifuata bila ya kuyumbishwa.

Mstoa Marcus Aurelius kwenye kitabu cha sita cha Meditations, ameshirikisha jinsi mtu unavyopaswa kujijengea nidhamu kali ya kazi na kuweza kufanya makubwa. Kuna mambo ya msingi sana ambayo ameshirikisha kuhusu kazi, ambayo tukiyazingatia tutaweza kufanya makubwa.

Kitu cha kwanza ni kutekeleza majukumu yako kwa kadiri ya uwezo mkubwa ulio ndani yako. Hapa anatuasa tusiwe wavivu na kufanya vitu kwa juu juu, au kutafuta visingizio vya kutokufanya. Badala yake tunapaswa kutumia uwezo mkubwa tulionao ndani yetu kutekeleza majukumu yetu ya kazi kwa uhakika.

Kitu cha pili ni kuifanya kazi kwa sababu ndiyo wajibu wako kuifanya na siyo ili kupata sifa. Watu wengi huwa wanafanya kazi kidogo na kutumia muda mwingi kutafuta sifa kwenye kazi hizo. Hilo linawazuia kuweza kufanya makubwa. Wajibu wako ni kufanya kazi, ifanye kwa uhakika na ukishaimaliza nenda kwenye kazi nyingine. Yaache matokeo ya kazi zako yajisemee yenyewe na siyo wewe kuyapigia kelele.

SOMA; #TANO ZA #JUMA #14 2018; Wewe Kama Mfalme Wa Akili, Mwili Na Matukio, Rafiki Wa Kweli Ambaye Hatakuja Kukuacha, Jinsi Ya Kuepuka Kutumika Kutapeli Wengine Na Unachopata Pale Unaposubiri.

Kitu cha tatu ni kuacha kuvipa vitu umuhimu ambao havina. Watu wengi wamekuwa wanakwama kuweka vipaumbele kwenye kazi zao kwa sababu wanaweka umuhimu kwenye vitu ambavyo havina umuhimu mkubwa. Kwa mfano mtu anaona chakula fulani ni muhimu zaidi, mfano nyama, wakati ukiangalia kwa uhalisia, nyama ni mnyama aliyeuawa tu. Kadhalika vitu kama madini, kiuhalisia ni mawe tu ambayo yamechimbwa ardhini. Kitu muhimu zaidi kinapasa kuwa kazi, vingine vinapaswa kuzingatiwa kwa uhalisia wake na siyo kupewa umuhimu ambavyo havina.

Kitu cha nne ni kufanya kazi yako bila ya kulalamikia ugumu wake au kuacha. Kwa sababu kazi ni ngumu, hupaswi kuchukulia kwamba haiwezekani. Na kama kuna mwingine ameweza kufanya, hata wewe pia utaweza kufanya. Na hata kama hakuna mwingine aliyeweza kufanya, wewe utakuwa wa kwanza kufanya na kuwa mfano mzuri kwa wengine.

Kitu cha tano ni kutokuhangaika na usumbufu mwingi unaokutoa kwenye majukumu yako makuu. Kwa chochote utakachochagua kufanya, kuna vitu vingine vitakavyoonekana muhimu zaidi. Ukiacha kile kikuu na kuhangaika na hivyo vingine utajikwamisha kupata matokeo mazuri ambayo ungeweza kuyapata.

Hayo ni mambo matano ya msingi ya kujijengea nidhamu kali ya kazi kutoka falsafa ya Ustoa. Kuna mengine ambayo Marcus ameyashirikisha kwenye kitabu, ikiwepo nidhamu kali ya kazi ya Antonius ambayo wote tunapaswa kujipima nayo kama tunataka kufanya makubwa. Karibu ujifunze hayo kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.