Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye mapambano ya mafanikio, kuna vitu viwili tu ambavyo unaweza kuvileta; matokeo au visingizio.
Utayari wa nini ambacho mtu unaleta ndiyo umekuwa unawatofautisha wale wanaofanikiwa na wanaoshindwa.
Wanaofanikiwa huwa wanaleta kitu kimoja tu ambacho ni matokeo, wataonekana wakati wa matokeo. Kama hawana matokeo hawaonekani kabisa, kwa sababu wanakuwa wanapambana kuyapata matokeo. Hakuna kitu kingine wanachokuwa wanaweza kukielezea tofauti na matokeo.
Wanaoshindwa huwa wanaleta kitu kimoja mara zote ambacho ni sababu na visingizio. Ni watu wenye maelezo mengi kwa nini wameshindwa kupata matokeo ambayo walikuwa wanayataka. Wanatoa sababu ambazo zinawafanya wajisikie vizuri, wakitaka kuonekana tatizo siyo wao.

Wanaotoa matokeo ndiyo mashujaa ambao wanaleta mabadiliko makubwa. Ndiyo ambao wanajengewa masanamu na kukumbukwa vizazi na vizazi.
Wanaotoa sababu wanaweza kuonewa huruma, lakini hakuna anayewapa uzito. Kila anayesikiliza sababu zao anajua hawajajitoa vya kutosha kupata kile wanachotaka. Hivyo hawathaminiwi kabisa.
Kama unataka kufanya makubwa kwenye maisha yako, kama unataka kujenga mafanikio yatakayogusa maisha ya wengine, basi achana na sababu au visingizio, leta matokeo.
Kama huna matokeo ya kuleta, hupaswi hata kuonekana, wacha watu wajue uko kuyapambania matokeo kuliko waje wakuone ukiwa unatoa sababu na visingizio.
SOMA; 2341; Visingizio ni vingi, sababu ni moja…
Wewe mwenyewe ona aibu kusimama mbele ya watu na badala ya kutoa matokeo, unaanza kutoa maelezo. Ona jinsi ambavyo watu watakucheka, kukudharau na kukupuuza baada ya kuwa umeshatoa maelezo yako. Hayo yote yakupe hasira ya kupambana mpaka ulete matokeo.
Kutoa sababu badala ya matokeo ni kiashiria kwamba umeshindwa na mbaya zaidi umekubali kushindwa. Kuna kushindwa na kuna kukubali kushindwa, kukubali kushindwa ni kubaya sana.
Unapotoa sababu na visingizio, maana yake unakiri kwamba huwezi kufanya tena. Kwa sababu kama ungeweza, usingekuwa unatoa sababu na visingizio, ungekuwa kwenye kuyapambania matokeo makubwa unayotarajiwa kuyatoa.
Rafiki yangu mpendwa, wito wangu kwako ni mmoja, acha kutoa sababu na visingizio na anza kutoa matokeo. Kama huna matokeo ya kutoa, hakikisha hata hauonekani, badala yake kuwa umetingwa sana kuyazalisha matokeo yanayotegemewa. Ni kujitoa kiasi hicho ndiko kunakupa wewe uhakika wa kujenga mafanikio makubwa unayoyataka.
Jifunze zaidi kuhusu kuacha kutoa sababu na kuanza kutoa matokeo kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.