Habari njema muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ukamilishaji ambazo ni mwendelezo wa makala kutoka CHUO CHA MAUZO.
Hongera sana kwa kuendelea kujifunza na kuchukua hatua kwa haya unayoendelea kujifunza hapa.
Leo ni jumatano ya ukamilishaji tukiongozwa na kauli mbiu inayosema ABC ALWAYS BE CLOSING-MARA ZOTE KUWA UNAKAMILISHA WATEJA.
Kama kauli mbiu inavyosema, mara zote unapaswa kukamilisha wateja na wewe pia unapaswa kukamilisha wateja. Na kukamilisha ndiyo wajibu wako namba moja kwenye biashara yako.
Wajibu wako namba moja ni kuuza na unapokuwa umemuuzia mteja maana yake umemkamilisha.
Hivyo basi, kila wakati wageuze wateja tarajiwa uliokuwa nao na waweze kununua na kuwa wateja kamili.
Kwenye somo letu lililopita tulijifunza mbinu mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo nayo ni mbinu namba 21 na 22.
Kwenye mbinu namba 21 tulijifunza ukamilishaji kufanya tu na kwenye mbinu namba 22 tulijifunza ukamilishaji wa ugonjwa.
Kama ulienda kuzifanyia kazi na kupata matokeo basi karibu sana utushirikishe namna ulivyonufaika nazo mbinu hizo.
SOMA; Mbinu Mbili Za Uhakika Za Ukamilishaji Wa Mauzo 21-22
Leo kwenye ukamilishaji tukiongozwa na kauli mbiu yetu inayosema ABC ALWAYS BE CLOSING-MARA ZOTE KUWA UNAKAMILISHA WATEJA, tunakwenda kujifunza mbinu nyingine mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo nazo ni mbinu namba 23 na 24.

Zifuatazo ni mbinu mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo;
23.Ukamilishaji wa ‘fanya kwa ajili yangu’.
Kuna wakati mteja unamweleza umuhimu wa kile unachouza lakini hakuelewi anaishi tu kukupa mapingamizi mbalimbali.
Wewe kama muuzaji kutokubali sababu za mteja kukuzuia wewe kumuuzia.
Watu wengi huwa wanapenda kuwasaidia wengine, kama mengine yote yameshindikana basi waombe wakusaidie.
Kama umemuomba afanye kwa ajili, mwenza wake au watoto lakini hasikii, basi mwombe afanye hata kwa ajili yako.
Unaweza kuona ni kitu cha ajabu, lakini jaribu na utashangaa jinsi watu watavyokuwa tayari kufanya kwa ajili yako.
Kwa mfano baada ya mteja kushindwa kufanya kwa ajili yake au familia yake, mwambie hivi;
“Ndugu, kama huwezi kufanya kwa ajili yako na kama huwezi kufanya kwa ajili ya mwenza wako, basi fanya kwa ajili yangu. Nahitaji uweke sahihi yako hapa.
Nahitaji tukamilishe hili.
Nahitaji ulipie sasa”
Mauzo ni vita isiyoruhusu umwagaji wa damu. Kuwa king’ang’anizi kuhakikisha unamkamilisha mteja na ananunua.
24.Ukamilishaji wa bidhaa ya chini.
Ukamilishaji huu hutumika pale mtu anapokuwa ameshindwa bei hivyo kupendekezewa bidhaa au huduma ambayo inaendana na aliyotaka ila bei yake ni ya chini zaidi.
Ukamilishaji huu pia unatumika kupima kama mtu anaitaka bidhaa kweli au anatumia bei kama kisingizio tu.
Pale mteja anapokuwa anakupa pingamizi kuhusu bei, tumia ukamilishaji wa bei ya chini kwa mfano.
“Je utakuwa tayari kuchukua bidhaa ya chini ya hii? Itakuokolea fedha na malipo ya mwezi yatakuwa kidogo.
Au utachukua hii na kulipa zaidi kila mwezi?”
Kwa kutumia mbinu hii, kama mteja ni mnunuaji atanunua na kama siyo mnunuaji utajua mapema na hilo litakusaidia wewe kuelekeza nguvu kubwa kwa wateja wengine au kufanya shughuli zitakazokusaidia kupata wateja wengine na kuwahudumia.
Hatua ya kuchukua leo; Tumia mbinu hizi mbili za uhakika kabisa za kumkamilisha mteja wako.
Tumia ukamilishaji wa fanya Kwa ajili yangu na ukamilishaji wa bidhaa ya chini na kuuza.
Kitu kimoja zaidi, ukamilishaji unahitaji kujitoa hasa, msimamo na mtazamo wa uwezekano.
Kila wakati jitoe hasa, kuwa na msimamo wa kumfuatilia mteja wako na bila kusahau kuwa na mtazamo wa uwezekano ili uweze kupata ushindi kwenye mchakato wa mauzo yako.
Kutoka kwa muuzaji mwenzako, rafiki anayekupenda na kukujali,
Mwl.Deogratius Kessy
Mwalimu/Mwandishi/Mkufunzi wa mauzo.
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz