Rafiki yangu mpendwa,

Kuna jambo moja huwa linashangaza sana inapokuja kwenye kazi na kujenga utajiri na mafanikio makubwa. Wale ambao tayari wameshafanikiwa sana, ambao hata wasipofanya kazi kabisa bado maisha yao yataweza kwenda ndiyo huwa wanafanya kazi kuliko ambao hawajafanikiwa. Wakati huo wale ambao hawajafanikiwa wakiwa wanahitaji sana kufanya kazi ndiyo maisha yao yaweze kwenda.

Kushangaza hakuishii hapo kwenye ufanyaji wa kazi, bali unakwenda mpaka kwenye mtazamo juu ya kazi ambao watu wanakuwa nao. Wale ambao hawajafanikiwa wakiwaona waliofanikiwa jinsi wanavyofanya kazi kwa juhudi kubwa, huwa wanaona kama wanajitesa tu. Wao wanajiambia wakipata mafanikio makubwa hawatahangaika tena na kazi.

Na hilo linaonyesha dhahiri ni kwa nini wengi ambao hawajafanikiwa hawataweza kufanikiwa, kwa sababu mtazamo walionao kuhusu kazi siyo sahihi.

Wakati waliofanikiwa wakichukulia kazi kama kitu kizuri kwao na hivyo kuipenda na kuifanya kwa viwango vya juu, walioshindwa wanaona kazi kama mateso na hivyo kuichukua na kutafuta njia za kuikwepa.

Ambacho hawajui wale wasiofanikiwa ni kadiri unavyokwepa kuikabili kazi ndivyo wanavyojichelewesha na kujizuia kuyapata mafanikio makubwa wanayoyataka.

Ili kujijengea utajiri mkubwa na kupata mafanikio unayoyataka, unapaswa kujijengea nidhamu kali sana ya kazi. Kufanya kazi kwa viwango vya kawaida, kama ambavyo wengine wanafanya haitakuwezesha kujenga mafanikio makubwa kadiri ya unavyotaka.

Ni lazima uipende sana kazi na kuifanya kuwa kipaumbele chako cha kwanza. Ni lazima muda wako mwingi uutumie kwenye kazi na kwenye muda huo wa kazi unapaswa kufanya kazi tu. Hupaswi kupoteza muda wa kazi kwenye mambo ambayo hayahusiani na kazi.

Ninaposema kazi hapa unapaswa kuelewa sizungumzii kazi ya ajira, bali kazi kama majukumu yako kwenye biashara unayojenga au uwekezaji unaofanya. Kwa chochote ambacho unapanga kufanya ili kupata matokeo unayokuwa unayataka, unapaswa kukifanya kwa viwango vya juu sana ili uweze kupata mafanikio makubwa.

SOMA; #SheriaYaLeo (63/366); Jijengee nidhamu ya kazi.

Kujenga nidhamu kali ya kazi haiishii tu kwenye majukumu ya kazi unayokuwa unafanya, bali pia inaenda kwenye maisha yako ya kila siku. Unapaswa kuwa na nidhamu kali sana kwenye maisha yako kiasi kwamba kazi inakuwa ndiyo kipaumbele cha kwanza kwako.

Kwanza kabisa unapaswa kuacha kuhangaika na mambo ya wengine na kujali mambo yako. Usiwe na wivu, chuki au tamaa kwa vitu vya wengine, hangaika na mambo yako zaidi. Usishiriki kwenye mazungumzo ya umbeya au majungu juu ya watu wengine, tumia muda huo kufuatilia mambo yako.

Maisha yako binafsi pia yanapaswa kuwa rahisi na ambayo hayataathiri mipango yako ya kazi. Ulaji wako, uvaaji wako na hata mapumziko yako havipaswi kuvuruga kabisa nidhamu kali ya kazi unayojijengea. Epuka kabisa vilevi na vyakula vinavyouchosha mwili wako na ukashindwa kuweka juhudi kubwa kwenye kazi.

Unapotenga muda wa kazi, kaa kwenye kazi yako muda wote, sahau kuhusu mapumziko, sahau hata kuhusu kula. Kitu cha kukutoa kwenye jukumu unalofanya ni pale unapokuwa na haja ya kwenda kujisaidia. Vinginevyo ni wewe na kazi, kazi na wewe.

Kama hauna mapenzi makubwa ya kazi kwa kiasi hicho, kama unaangalia muda wa kazi uishe ili uende kwenye mambo mengine. Kama lazima uende kwenye starehe unazopenda hata kama kuna majukumu ya kazi hujayakamilisha, tayari unakuwa umejitenga na mafanikio makubwa.

Kupata mafanikio makubwa ingekuwa ni lele mama, kila mtu angekuwa nayo. Siyo rahisi, machozi, jasho na damu ni lazima vimwagike, je wewe umejitoa kiasi gani kuhakikisha unayapata mafanikio makubwa unayokuwa unayataka?

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimekushirikisha mambo 20 ya kuzingatia kwenye kujijengea nidhamu kali ya kazi itakayokuwezesha kujenga utajiri na mafanikio makubwa. Fungua ujifunze na uchukue hatua ili kupata mafanikio.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.