Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye tasnia ya mafunzo ya mafanikio huwa kuna usemi kwamba ukitaka kumjua anayekuzuia kufanikiwa, simama mbele ya kioo. Hiyo ina maana kwamba unaposimama mbele ya kioo, unajiona wewe mwenyewe. Hivyo basi, wewe mwenyewe ndiye umekuwa kikwazo kwako kufanikiwa.
Wengi wanaposikia kwamba wao wenyewe ndiyo wamekuwa wanajikwamisha wasifanikiwe huwa hawaamini. Huwa wanadhani ni maneno tu ya kuchangamsha genge. Ndani yao wanakuwa wanaamini kabisa kuna namna nguvu za nje zinawazuia kufanikiwa.
Kitendo tu cha kuwa na hizo imani kwamba kuna nguvu za nje zinazowazuia kufanikiwa, kinawafanya watu wazidi kushindwa kufanikiwa. Hiyo ina maana kwamba kama unabisha kauli ya wewe ndiye adui wa mafanikio yako, basi utazidi kujizuia kufanikiwa.

Kuna mambo matatu ambayo watu huwa wanapenda sana kuyafanya na hayo yamekuwa yanaishia kuwa kikwazo kwao kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yao.
Jambo la kwanza ni kulaumu watu wengine kama sababu ya wao kushindwa.
Lawama huwa ni rahisi kuzitoa, lakini ukishazitoa unakuwa pia umepoteza uwajibikaji ambao ndiyo unahitajika kwenye kujenga mafanikio. Unapowalaumu watu wengine kwa namna yoyote ile unakuwa umeonyesha wao ndiyo wenye nguvu kwenye maisha yao. Unaonyesha kwamba wewe ni dhaifu na usiyeweza kufanya makubwa.
Unapaswa kuacha kabisa kuwalaumu watu wengine na kushika hatamu ya maisha yako. Kama kuna kitu hakipo sawa kwenye maisha yako, ni wewe mwenyewe umesababisha. Unapaswa kuchukua hatua kurekebisha kile ambacho hakipo sawa badala ya kurusha lawama kwa wengine.
Jambo la pili ni kuhalalisha matokeo uliyoyapata.
Watu huwa wana tabia ya kuhalalisha matokeo waliyopata na kuona wapo sahihi. Kwa kuwa wanakuwa wamepata matokeo madogo, wanatafuta namna ya kuonyesha hayo ndiyo matokeo sahihi na wale waliopata zaidi siyo watu wazuri. Hapa watu huwajengea picha mbaya wale ambao wamepiga hatua kubwa, kitu kinachowazuia wao wasipige hatua kubwa kama hizo.
Kataa kuhalalisha matokeo madogo unayoyapata, kuwa na hasira ya kupata matokeo makubwa zaidi. Mara zote kazana kupata matokeo makubwa kuliko yale ambayo umeshayapata. Pia wapende wale wote waliofanikiwa kuliko wewe ili uweze kujifunza kwao na wewe ufanikiwe.
Jambo la tatu ni kulalamika.
Hapa mtu anakuwa anatoa maelezo badala ya kutoa matokeo. Hii ni tabia pendwa kwa watu ambao hawajafanikiwa, huwa wana maelezo mengi sana ya kwa nini mafanikio ni magumu kwao. Wataonyesha jinsi ambavyo wanapambana lakini matokeo hayaji. Lakini ukweli ni unapowachunguza, unakuta kuna mengi wanayojikwamisha nayo.
Acha kuwa mtu wa kulalamika na kutoa maelezo mengi. Wewe kuwa mtu wa matokeo, unapoonekana inajulikana kabisa umeleta matokeo na siyo sababu au visingizio.
Ukiacha kuyakumbatia hayo matatu ambayo yamekuwa yanakukwamisha sana, utaweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yako. Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini unapata fursa ya kujifunza mambo hayo matatu kwa kina na kuachana nayo ili kujenga mafanikio makubwa. Fungua ujifunze na uweke kwenye matendo ili uweze kuyabadili maisha yako.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.