Rafiki yangu mpendwa,
Grant Cardone, kwenye kitabu chake cha 10X Rule anaeleza kwamba wakati anaanza huduma yake ya kufundisha kuhusu mauzo, alijiwekea lengo la kuwahudumia wateja wachache kwa ukubwa ili kuwaridhisha na kubaki nao kwa muda mrefu.
Aliona akikusanya nguvu zake kwa wateja hao wachache, atawapa thamani kubwa, wataridhika na kubaki kwake kwa muda mrefu na hivyo kutokuhitajika kuhangaika na wateja wapya kila wakati.

Lakini baadaye alikuja kugundua alikuwa anafanya makosa makubwa sana. Kwani kuchagua kuwahudumia wateja wachache alishindwa kusambaza mafunzo yake mazuri kwa wengi sana waliokuwa wanayahitaji.
Na hata kwa upande wa kipato, alijikuta akiwa amejiwekea ukomo mkubwa wa kipato. Hivyo licha ya kufanya kazi sana, kipato kikawa kidogo na kupelekea uendeshaji wa biashara kuwa mgumu. Hiyo ni kwa sababu aliweka nguvu zake kwa wateja wachache na kuacha kutafuta wateja wapya.
Kitu kibaya zaidi, ni kile alichotegemea kingetokea, kwa upande wa kuwaridhisha wateja kwa kuwa nao wachache, nacho pia hakikutokea. Kwani bado kulikuwa na malalamiko ya baadhi ya wateja, licha ya kuwapa thamani kubwa.
Hapo ndipo alipoamua kubadili mkakati wa biashara yake na kuacha kulenga watu wachache. Badala yake aliamua anataka watu wote duniani wajue kuhusu yeye na biashara anayoifanya. Na hapo ndipo alipoanza kupiga kelele kwa wingi sana, kuhakikisha kila mtu anajua kuhusu biashara yake.
Mwanzo ulikuwa mgumu, kwa sababu wengi walikuwa hawamjui, ilimlazimu kuchukua hatua kubwa sana na ambazo ziliwafanya wengine wamkosoe na kumkatisha tamaa. Lakini kwa sababu alidhamiria, aliendelea kwenda.
Haikumchukua muda alianza kupata wateja wengi, kupitia kujulikana na watu wengi zaidi. Alianza kuingiza kipato kikubwa kutoka kwenye biashara yake, kuweza kujenga timu kubwa na kuwahudumia wateja wengi zaidi.
Malalamiko ya wateja yaliendelea kubwa, lakini akawa amejifunza kitu kimoja, malalamiko ya wateja siyo kitu kibaya, bali ni mrejesho wao kuhusu kuboresha huduma. Hivyo akawa anayatumia malalamiko ya wateja kuboresha huduma aliyokuwa anaitoa.
Kupitia uzoefu wake, Grant Cardone anasema wafanyabiashara wengi wamekuwa wanajikwamisha kufanya mauzo makubwa kwa kuhangaika na lengo lisilo sahihi.
Lengo ambalo anasema wafanyabiashara wengi wanahangaika nalo ni kuwaridhisha wateja, kitu ambacho hakiwezekani. Ni vigumu sana kumridhisha kila mtu, hata kama ungekuwa unatoa vitu bora kiasi gani.
Anaeleza lengo sahihi la kila mfanyabiashara linapaswa kuwa ni kutengeneza wateja wapya tarajiwa wengi zaidi. Kila wakati biashara inapaswa kuwa inawafikia wateja wengi zaidi. Kwa sababu ni kupitia biashara kuwa na wateja wengi ndiyo inaweza kuwaridhisha watu.
Biashara ikiwa na wateja wengi, inakuwa na nguvu ya kufanya makubwa zaidi kuliko ikiwa inategemea wateja wachache. Na japokuwa biashara kuwa na wateja wengi malalamiko nayo yatakuwa mengi, lakini itakuwa ni sehemu nzuri ya kujifunza na kuboresha.
Kuhangaika na wateja wengi haimaanishi biashara inapuuza kabisa kutoa huduma nzuri kwa wateja. Kwanza kabisa kabla biashara haijaanza hata kuwafikia wateja, lazima iwe na thamani kubwa na ya kipekee ambayo inaitoa, thamani ambayo wateja hawawezi kuipata mahali pengine.
Halafu lazima biashara iwaahidi wateja mambo makubwa na wanapokuja kwenye biashara yale yaliyoahidiwa yatimizwe kwa ukubwa zaidi. Yaani wateja wavutiwe na ahadi kubwa, lakini washangazwe zaidi na utekelezaji wa ahadi ambao ni mkubwa sana.
Ukifanya hayo, yaani kuwa na thamani kubwa, kuahidi na kutekeleza makubwa utaweza kuwa na wateja wengi sana waaminifu wa biashara yako. Kuna ambao hawataridhishwa na biashara yako kwa sababu zao binafsi, lakini kwa sababu wanachopata kwako hawawezi kupata kwa mwingine, watajikuta wanaendelea na wewe.
Kama mfanyabiashara, kamwe usijizuie kuwafikia wateja wengi zaidi. Hata kama kwa sasa huna nafasi ya kuweza kuwahudumia wateja wengi zaidi, usiache zoezi la kutafuta wateja wapya. Unachopaswa kufanya ni kuongeza vigezo vya wateja unaowataka na kuachana na wale ambao unaona hawaendani na biashara yako kama unavyotaka.
Ni kwa kuwa na malengo sahihi ya kibiashara kama hivyo ndiyo unaweza kuwa na wateja wengi, kufanya mauzo makubwa na kukuza biashara.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini, kuna mjadala wa washiriki mbalimbali wa mafunzo juu ya dhana hii ya kuweka nguvu kwenye kufikia wateja wengi badala ya kuridhisha wateja. karibu usikilize kipindi ili uweze kujenga biashara kubwa na inayokupa mafanikio unayoyataka.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.