Habari njema muuzaji bora kuwahi kutokea,
Karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ushawishi kutoka kwenye programu yetu ya CHUO CHA MAUZO.
Jumamosi ya ushawishi tunaongozwa na kauli mbiu inayosema HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.
Wiki iliyopita tulifanikiwa kukamilisha kujifunza njia sita za kuwafanya watu wakukubali kwenye kila eneo la maisha yako.
Mpaka sasa utakua tayari umeshajijengea uzoefu na kuwa mtu wa ushawishi kama ulikuwa unafanyia kazi njia hizo sita.
Habari njema ni kwamba, leo tunakwenda kujifunza sehemu nyingine ambayo ni jinsi ya kuwafanya watu wakubaliane na mawazo yako.

Sina uhakika kama itakufaa lakini kuna wakati unakutana na watu ambao hamkubaliani kwenye jambo moja lakini unahitaji watu hao wakubaliane na wewe ili kuweza kukamilisha unachotaka.
Watu wengi wamekuwa wanatumia njia ya ubishani na nyinginezo kuwafanya watu wakubaliane na mawazo yao. Lakini, njia hizo zimekuwa hazizai matunda. Kwani hata ukishinda kupitia mabishano, kwa wewe kuwa na hoja zaidi ya wengine, bado watu wataendelea na kusimamia walichokuwa nacho tangu awali.
Hata uwafanye nini, wao wataendelea kubaki na msimamo wao wa awali.
Ili tuweze kushinda mabishano, tunapaswa kujifunza kanuni za kuweza kuwashawishi watu wakubaliane na mawazo yetu bila kutumia nguvu kubwa.
Habari njema ni kwamba leo tunakwenda kujifunza kanuni ya kwanza ya kuwafanya watu wakubaliane na mawazo yako.
Na kanuni hiyo ya kwanza ni ; Njia Pekee Ya Kushinda Mabishano Ni Kuyaepuka.
Mwandishi wa kitabu cha How to Win Friends And Influence People Dale Carnegie anatuambia kwamba huwezi kushinda mabishano kwa kubishana, hata uwe na hoja nzuri kiasi gani, ukishaingia kwenye mabishano jua umekubali kushindwa.
Njia pekee ya kushinda mabishano ya aina yoyote ile ni kuyaepuka, usikubali kabisa kuingia kwenye mabishano.
Unapaswa kuepuka mabishano kama vile unavyoepuka nyoka au ajali.
Kushiriki kwenye mabishano ni kushindwa kwa sababu hata kama utakuwa hoja nzuri, uko sahihi na mwingine amekosea, ataendelea kusimamia kile anachokiamini.
Mtu anapochukua hatua ya kubishana juu ya kitu fulani, maana yake anakiamini zaidi na wala hataki kujiona yeye ni mjinga abishanie kitu ambacho siyo muhimu.
Hivyo basi, hata umpatie hoja nzuri kiasi gani, hatabadili msimamo wake.
Kwa mfano, wewe ni mtu wa mauzo na unauza simu za kampuni A.
Mteja anakuja kukuambia siwezi kamwe kununua simu za kampuni A, hata ukinipa bure sichukui, maana siyo simu nzuri. Nitaenda kununua simu za kampuni B, maana ndiyo simu bora.
Kwa mteja wa namna hiyo, ukianza kubishana naye kwamba simu za kampuni A ni nzuri kuliko anavyofikiri yeye, utamfanya azidi kusimamia kile anachokiamini, atakupa hoja zaidi hata kama siyo sahihi.
Kwa mteja kama huyo, unachopaswa kufanya ni wewe kukubaliana naye kwenye kile anachokiamini kwanza, mwambie uko sahihi, simu za kampuni B ni bora na ukizinunua huwezi kuwa umefanya makosa.
Kwa kuanzia hapo, mtu huyo hatakuwa tena na hoja ya kupambana na wewe kwani umeshakubaliana naye.
Na hapo sasa unakuwa na nafasi ya kumwonesha kwa nini pia simu za kampuni A ni nzuri. Unaweza kumuonesha kile ambacho hajawahi kukijua na huenda akachukua hatua ya kununua simu za kampuni A.
Kwa mfano kama huo, wewe kama muuzaji utakuwa umejifunza kushinda mabishano hayo kwa kuepuka kubishana na badala yake kukubaliana na upande aliopo mtu na kisha kupata nafasi ya kueleza upande wako.
Ni asili yetu sisi binadamu kukimbilia kwenye mabishano pale watu wanapotofautiana na sisi lakini hilo huwa halizai matunda.
Kataa aina yoyote ile ya mabishano, jijengee tabia ya kuepuka mabishano ya aina yoyote yale, ukiwa ni mtu unayependa kubishana inakupunguzia ushawishi kwenye kila eneo la maisha yako.
Ondoka na somo kwamba, wewe kama muuzaji hupaswi kubishana na mteja wako.
Pale anapokuwa anakiamini zaidi kile anachokiamini yeye, mpe ushindi kwanza ili ukate ubishani kwa kukubaliana naye.
Ukitaka kujenga ushawishi na kuimarisha mahusiano yako, USIBISHANE na mtu badala yake wape watu ushindi kwenye kile wanachokiamini.
Na waswahili wanasema, ndugu wakigombana wewe shika jembe ukalime. Hivyo basi, ukiona mabishano tu, shika jembe lako uende ukalime.
Wabudha waliwahi kusema, chuki haiwezi kuondolewa kwa chuki bali upendo.
Halikadhalika hali ya kutoelewana haiwezi kuondolewa na mabishano bali kwa kusikilizana na kuelewana.
Aliyekuwa raisi wa marekani Abraham Lincoln amewahi kunukuliwa akisema, ukikutana na mbwa kwenye njia yako, na ukapambana naye ili upite, utaishia kuumwa na mbwa huyo hata kama utamshinda na kupita, utabakia na jeraha. Ni bora kumwacha mbwa apite na wewe kupita salama.
Mara nyingi huwa tunakimbilia mabishano pale tunapojua sisi tupo sahihi na wengine wamekosea lakini hilo huwa halina msaada kwetu.
Epuka mabishano hata kama mtu mwingine amekosea na wewe umepatia, jiweke kwenye nafasi yake, elewa kwa nini anaamini anachoamini na kisha tumia uelewa huo kumsaidia kuuona ukweli.
Kitu kimoja zaidi, Dale Carnegie anamnukuu Jan Peerce baada ya kumuoa mke wake, waliwekeana makubaliano kwamba wanapokuwa katika hali ya kutoelewana na mmoja akaanza kugomba, basi mwingine anapaswa kukaa kimya na kusikiliza maana watu wawili wanapogombana panakuwa hakuna mawasiliano bali ni kelele.
Rafiki, mara zote USIBISHANE na mteja wako au mtu yoyote yule. Wale ushindi maisha yaendelee na siyo kubishana nao.
Kutoka kwa muuzaji mwenzako, rafiki anayekupenda na kukujali,
Mwl.Deogratius Kessy
Mwalimu/Mwandishi/Mjasiriamali
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz //0717101505//0767101504