Rafiki yangu mpendwa,

Kila biashara huwa inakuwa na ushindani, lakini biashara zinazopata mafanikio makubwa huwa hazishindani, badala yake huwa zinatawala na kunyima washindani nguvu ya kuzisumbua.

Je hilo linawezekanaje wakati kwa zama hizi kila kitu kipo wazi na rahisi kuigana kwenye biashara? Kwa sababu wewe mwenyewe unaweza kuwa uliingia kwenye biashara kwa kuwaiga wengine.

Na hata kama utaanza biashara kwa ubunifu wako mwenyewe, bado ikifanya vizuri hutaweza kuwazuia wengine kukuiga na kufanya biashara hiyo. Hivyo kuigana kwenye biashara ni kitu ambacho hakiwezi kuisha, kadhalika ushindani.

Namna pekee ya kuzuia ushindani usikusumbue kwenye biashara ni kuwa na kitu ambacho hakiwezi kuigwa. Hapa unakuwa na kitu au vitu ambavyo vipo kwenye biashara yako kwa utofauti na hakuna mtu anaweza kuviiga. Hata kama vitu hivyo vinaonekana wazi kabisa, bado inakuwa vigumu kwa watu kuweza kuviiga.

Ukifikiria kwa haraka haraka, utaona hakuna kitu cha aina hiyo, kwa sababu kila kitu kinaweza kuigwa. Lakini ukweli ni kwamba kipo na kinaanzia ndani yako mwenyewe.

Kitu hicho ni haiba yako, vile ulivyo wewe, ambavyo unatofautiana kabisa na watu wengine. Kuna namna wewe upo na ambayo inakutofautisha kabisa na watu wengine. Ukiweza kupeleka hiyo haiba yako kwenye biashara yako, itaweza kujenga upekee ambao hauwezi kuigwa na watu wengine. Wataona kabisa nini unachofanya tofauti, lakini hawataweza kuiga.

Wanashindwa kuiga kwa sababu wanakosa msukumo wa ndani ambao wewe unao kwenye kufanya vitu hivyo. Kwenye vitu ambavyo ni haiba yako, unakuwa na msukumo wa kuvifanya bila kuchoka. Husubiri mtu akuambie ufanye au kusukumwa ufanye, bali unajisukuma mwenyewe kufanya mpaka watu wanakutaka upunguze.

Hivyo ndiyo vitu ambavyo ukivigeuza kuwa biashara yako utaweza kujenga biashara yenye mafanikio makubwa sana na isiyoyumbishwa na ushindani. Hiyo ni kwa sababu kile kinachoonekana kama mchezo kwako, kwa wengine kinaonekana ni kazi ngumu. Wakati wewe una msukumo wa ndani wa kufanya, wengine hawafanyi mpaka wapate msukumo wa nje.

Msukumo unaokuwa nao wa kufanya, unakufanya unakuwa mbele sana ya watu wengine, kitu kinachokupa mafanikio makubwa na kupelekea usisumbuke na ushindani unaokuwepo.

Uzuri ni kwamba, tayari unayo haiba, tayari una vitu ambavyo unapenda sana kufanya, hata kama hakuna anayekulipa. Wajibu wako sasa ni kuviweka vitu hivyo kwenye biashara yako, angalia namna ambavyo unaweza kuvifanya kuwa sehemu ya biashara.

SOMA; Ukweli Mchungu; Kama Unataka Mafanikio Makubwa, Usiwe ‘Fair’.

Muhimu ni usichanganye vipaji ulivyonavyo na haiba tunayojifunza hapa. Kwa sababu ukizungumzia vipaji hiyo ni biashara nyingine. Hapa ni ule msukumo unaokuwa ndani yako juu ya vitu fulani.

Kwa mfano kama unapenda sana kupangilia vitu vyako, basi ifanye biashara yako kuwa na mpangilio bora kabisa.

Kama unapenda sana kuwa na viwango vya juu kwenye mambo yako, ifanye biashara yako kuwa na viwango vya juu kabisa kwenye kila kinachofanyika.

Kama una wajali sana watu, ifanye biashara yako kuwajali sana wateja.

Yote hayo yafanye kwa namna ambayo hakuna biashara nyingine inaweza kufanya, japo inaona kabisa unafanya, lakini ule msukumo wa kufanya unakuwa siyo mkubwa kwao kama unavyokuwa kwao.

Hivyo ndivyo unaweza kujenga biashara ambayo haisumbuliwi na ushindani kwa kuweka haiba yako kwenye biashara. Kunakuwa na vitu unavyofanya kwa uwazi, lakini wengine wanashindwa kuviiga kwa sababu hawana msukumo kama unaokuwa nao.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala mzuri kwenye eneo hili la kupeleka haiba yako kwenye biashara. Washiriki wa kipindi wametoa shuhuda zao binafsi jinsi wanatumia haiba zao kujenga biashara ambazo zinazidi kuwa imara kadiri muda unavyokwenda. Karibu ujifunze kwenye kipindi ili na wewe ukaweke haiba yako kwenye biashara yako na kupata mafanikio makubwa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.