Habari Matajiri Wawekezaji,

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya NGUVU YA BUKU, programu maalumu ya kujenga utajiri kupitia uwekezaji wa hatua ndogo ndogo kwa muda mrefu bila kuacha.

Tumeshajifunza jinsi ambavyo manufaa makubwa ya uwekezaji yapo kwenye muda ambao uwekezaji umefanyika. Kadiri muda unavyokuwa mrefu, ndivyo thamani ya ukuaji inavyokuwa kubwa pia. Lakini hayo yote ni kama huo uwekezaji hautaingiliwa kwa kutolewa na kupelekwa kwenye vitu vingine.

Kanuni yetu kuu ya uwekezaji kwenye programu ya NGUVU YA BUKU ni WEKEZA NA SAHAU. Unapofanya uwekezaji, unasahau kuhusu hiyo fedha unayowekeza. Hiyo ina maana kwamba huhesabii tena fedha hiyo uliyowekeza kwenye mambo yako mengine.

Changamoto kubwa kwenye uwekezaji wa masoko ya mitaji, ambayo ni rahisi mtu kutoa fedha pale anapozihitaji, na hilo limekuwa linawafanya watu kukimbilia kutoa uwekezaji huo pale wanapokuwa na uhitaji wa fedha.

Ili uweze kufikia malengo makubwa ya utajiri kupitia uwekezaji wa masoko ya mitaji, kama kwenye mifuko ya pamoja ya UTT AMIS ambao tunafanya, ni lazima uwe na nidhamu kali sana kwenye kujizuia kutoa uwekezaji huo.

Hapo ndipo unapohitaji kuijua kanuni ya WEKEZA NA SAHAU na kuifanyia kazi kwa uhakika. Ukishawekeza fedha, unaisahau, kwa maana kwamba unaiondoa kabisa kwenye mahesabu yako.

Unapowekeza, unapaswa kuchukulia ni kama umenunua au kulipia kitu. Chukua mfano umenunua chakula ukala, au umenunua nguo. Ukija kuwa na uhitaji wa fedha baada ya kununua nguo, hutarudi kwa muuza nguo na kumwambia akurudishie fedha na umpe nguo zake kwa sababu una uhitaji nazo. Badala yake utatafuta namna nyingine ya kukamilisha mahitaji yako ya fedha.

Hiyo ndiyo nidhamu kali unayopaswa kuwa nayo kwenye uwekezaji tunaoufanya, ili pale unapopata shida, usikimbilie kutoa uwekezaji uliofanya. Hili ni muhimu sana kila mmoja wetu kulielewa, kwa sababu ni vigumu sana kuvumilia shida wakati unaiona fedha yako iko kwenye uwekezaji na unajua unaweza kutoa na kutatua shida zako.

Pale unapopata shida yoyote inayotaka fedha na wewe huna, usifikirie hata kidogo kuhusu fedha ambayo ipo kwenye uwekezaji. Badala yake fikiria huna kabisa uwekezaji huo na utafute njia nyingine za kutatua shida zako.

Ukijilemaza na kuwa rahisi kutoa fedha kwenye uwekezaji ili kutatua matatizo uliyonayo, kila tatizo litakushawishi utoe fedha, kwa kuona ni muhimu kufanya hivyo. Na hutaweza kupiga hatua ambazo ungeweza kuzipiga kama ungefanya uwekezaji kwa kanuni ya WEKEZA NA SAHAU.

SOMA; Fanikiwa kwa uwekezaji wa kukaa kitako.

JE UWEKEZAJI UNAKUWA NA FAIDA GANI KAMA HATUWEZI KUTUMIA KUTATUA SHIDA ZETU?

Swali unaloweza kuwa unajiuliza ni huu uwekezaji tunaoufanya ni wa kazi gani sasa kama mtu huwezi kuutumia kutatua shida ambazo unakutana nazo?

Jibu ni zipo njia nyingi za kutumia uwekezaji kwenye kutatua shida zako, ambacho unapaswa kujizuia ni kufikiria kuutoa uwekezaji kwa ajili ya kutatua hizo shida zako. Kwa sababu shida huwa haziishi, hivyo ukiwa unategemea uwekezaji kwa hilo, kamwe hutakuza uwekezaji wako.

Kama kweli unakuwa na uhitaji ambao huna namna nyingine ya kupata fedha ya kutatua bali kutumia uwekezaji, basi tumia uwekezaji wako kama dhamana ya kupata mkopo kwenye taasisi sahihi za kifedha.

Kwa sababu uwekezaji ni moja ya dhamana zinazokubalika, badala ya kuutoa kwa ajili ya matumizi unayokuwa nayo, utumie kama dhamana na nenda kaombe mkopo. Hili siyo tu litakuwezesha kuacha uwekezaji wako ukikua kwa muda mrefu, bali pia ule mlolongo mrefu wa kuomba mkopo mpaka kuupata itakukatisha tamaa.

Sisi binadamu huwa tunapenda kufanya vitu rahisi na ambavyo havitusumbui. Kama ikiwa kupata uwekezaji wako ni kujaza tu fomu na kusubiri siku kadhaa kupata fedha, ukiwa na shida utafanya hivyo. Lakini kama kuna mchakato mrefu kama huo wa kuchukua mkopo kwa dhamana ya uwekezaji, wengi hawatakimbilia kufanya.

UTARATIBU WA NGUVU YA BUKU KUTUMA UWEKEZAJI KILA WIKI.

Kwenye programu yetu ya NGUVU YA BUKU tunao utaratibu wa kutuma uwekezaji kila wiki, jumla ya thamani ya uwekezaji na taarifa fupi ya akaunti. Lengo ni kukupa wewe uwajibikaji wa kuepuka kutoa uwekezaji wako kirahisi.

Ukiwa peke yako, ni rahisi kujishawishi na ukatoa uwekezaji huo. Kwenye NGUVU YA BUKU tumekubali kuwekeza miaka 10 bila ya kutoa. Hivyo kwenye kila taarifa ya uwekezaji unayotuma kwa wiki, tunaangalia kama uwekezaji unapungua kwa kutoa.

Hatutaruhusu kabisa mtu yeyote kwenye programu ya NGUVU YA BUKU kutoa uwekezaji wake kwa sababu zozote zile. Tutumie fursa hii kujijengea nidhamu kali sana ambayo ndiyo inahitajika ili kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yetu.

Pale unapokuwa na shida hasa huku ukiwa huna namna nyingine, basi utatumia uwekezaji wako kama dhamana ya kupata mkopo kwenye taasisi za kifedha. Sisi tunachotaka kukamilisha zoezi letu la uwekezaji kwa msimamo bila kuacha kwa kipindi cha MIAKA KUMI.

Tunajua tunakwenda kuleta mapinduzi makubwa sana kwa huu mchakato tunaokwenda nao, lakini inahitaji nidhamu ya hali ya juu.

Kwa sasa unaweza usione shida kwa sababu huenda fedha ambayo umewekeza mpaka sasa ni kidogo. Zikianza kusomeka milioni kwenye huo uwekezaji, shida nazo ndiyo huwa zinaanza kujitokeza.

Tutaendelea kukumbusha hili mara kwa mara ili usije ukajenga tamaa kwenye kutumia huu uwekezaji kwa sababu zozote zile. Endelea na maisha yako kama huu uwekezaji haipo na utaweza kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yako.

MJADALA WA SOMO.

Karibu kwenye mjadala wa somo hili kushirikisha yale uliyojifunza kwa kujibu maswali yafuatayo;

1. Elezea kanuni ya WEKEZA NA SAHAU na kwa nini ni muhimu.

2. Ni mbinu gani za kukusaidia usiingie tamaa ya kutumia uwekezaji wako pale unapokuwa na shida na unaiona fedha ikiwa kwenye uwekezaji?

3. Pale unapokuwa huna namna nyingine ya kupata fedha, programu inaelekeza ufanyeje?

4. Toa ahadi yako ya kuwekeza kwa msimamo kwa miaka 10 bila kuacha wala kutoa uwekezaji huo kwa matumizi yoyote.

5. Karibu kama una swali lolote kuhusu somo hili na programu ya NGUVU YA BUKU kwa ujumla.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.