3372; Ipo au haipo.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha ni kazi kubwa sana, ambayo inamtaka mtu ajitoe kwa viwango vikubwa sana.

Ni kitu kinachopaswa kuwa kipaumbele cha kwanza kwa mtu kama kweli anataka kukifikia.
Safari hiyo imejaa vikwazo na changamoto za kila aina, hivyo mtu anapaswa kuwa tayari kuzivuka bila kukata tamaa.

Na mbaya zaidi, pamoja na juhudi kubwa ambazo wengi wanaweka, wengi hawatayapata mafanikio hayo makubwa.
Sababu ya watu hao wengi kutoyapata mafanikio siyo kwa sababu hawawezi, bali kwa sababu inakuwa haipo ndani yao hasa.

Kupata mafanikio makubwa inakuwa IPO ndani ya mtu pale msukumo wa kuyapata unatoka ndani yake.
Pale mtu anakuwa tayari kujisukuma yeye mwenyewe na siyo mpaka kusubiria msukumo kutoka nje.
Mtu anakuwa tayari kufanya kazi kubwa hata kama hakuna anayemuona au kumsifia.

Utawajua kwa urahisi sana wale ambao kupata mafanikio makubwa IPO ndani yao kwa jinsi ambavyo hawalazimishwi kufanya, bali wanazuiwa wasifanye.
Kwa msukuko huo, wanafanya kwa ukubwa sana na kuvuka kila kinachowazuia.

Kupata mafanikio makubwa inakuwa HAIPO ndani ya mtu pale msukumo wa kufanya makubwa unatoka nje yake.
Pale ambapo mtu hawezi kufanya mpaka asukumwe na watu wengine, inakuwa vigumu sana kwake kujenga mafanikio makubwa.
Kwa kutegemea msukumo wa nje, mtu anakuwa hajaweka mbele ufanyaji anaopaswa kukamilisha ili kupata matokeo makubwa.
Wanapokutana na magumu na changamoto, huwa wanakimbilia kuacha na kwenda kwenye vitu vingine.

Kuwajua kwa urahisi wale ambao kupata mafanikio makubwa HAIPO ndani yao, angalia wanalazimishwa nini. Kama wanalazimishwa kufanya, jua kabisa HAIPO, kwa sababu hicho ni kitu cha muda mfupi na kisichodumu.
Kama msukuko wa ndani wa kufanya haupo, mtu hataweza kuweka kazi ya kutosha kuweza kuyapata mafanikio makubwa.

Hii haimaanishi kwamba msukumo wa nje hauna muhimu kwenye safari ya mafanikio makubwa. Ni muhimu sana, kama ilivyo kuanzisha moto kwa kiberiti. Lakini ili upate moto mkubwa na utakaoleta madhara, lazima nishati iwepo, moto wa kuanzia ni kidogo na wa nje. Nishati ya kuendelea ni kubwa na ya ndani.

Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, tunatumia msukumo wa nje kama kichocheo na kukumbushana kuelekeza juhudi zetu kwenye maeneo sahihi.
Hatutegemei msukumo huo wa nje kama ndiyo msukumo mkuu wa kufanya.
Tayari msukumo upo ndani yetu, tunachohitaji ni kuuruhusu utupeleke kwenye makubwa.

Kinachotuleta pamoja kwenye jamii hii ya KISIMA CHA MAARIFA ni ule msukumo wa kufanya makubwa ambao tayari upo ndani yetu. Na kwa sababu kwenye mazingira yetu ya kawaida hatujazungukwa na wengi wenye msukumo, tunatafuta wale walio sahihi kwetu, wenye msukumo mkubwa kama wetu.
Hao ndiyo tunaowapata kwenye KISIMA CHA MAARIFA, hivyo tunaungana nao katika kufanya kwa ukubwa zaidi kwa msukumo kutoka ndani ya kila mmoja wetu.

Tumia jamii ya KISIMA CHA MAARIFA kama sehemu ya kuwa huru kufuata msukuko mkubwa ulio ndani yako na kufanya bila ya kujizuia.
Maana hilo ndilo hitaji kuu la safari yako ya mafanikio.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe