Rafiki yangu mpendwa,

Fikiria matukio haya mawili;

Tukio la kwanza unapita njiani na unakutana na mtu anayeuza kitu cha shilingi mia tano. Unavutiwa kukinunua, lakini mfukoni hauna fedha ndogo, una noti za shilingi elfu 10 tu.

Tukio la pili unapita njiani na unakutana na mtu anayeuza kitu cha shilingi mia tano. Unavutiwa kukinunua, na mfukoni una fedha ndogo, una noti za shilingi elfu 1.

Katika matukio hayo mawili, ni lipi ambalo utakuwa kwenye nafasi kubwa zaidi ya kufanya matumizi hayo ya shilingi mia tano? Tutakubaliana kwamba kwenye tukio la pili ni rahisi zaidi, pale unapokuwa na fedha ndogo ndogo huwa ni rahisi kufanya matumizi madogo madogo.

Rafiki, hilo siyo kwako tu, bali pia utafiti uliofanywa kwa watu wengi ulitoa matokeo ya aina hiyo. Kwamba matumizi ya watu huwa yanaongezeka pale wanapokuwa na fedha ndogo ndogo kuliko wasipokuwa nazo.

Kama hiyo ndiyo hali sasa, maana yake kuna fursa ya kupunguza matumizi hapo na fursa yenyewe ni kuhakikisha hutembei na fedha ndogo ndogo. Hakikisha kila unapokuwa unabeba noti za kiwango cha juu cha fedha tu, usiwe na fedha ndogo ndogo ambazo zitarahisisha wewe kufanya matumizi madogo madogo ambayo kwa sehemu kubwa hukuwa hata umeyapanga.

Rafiki, nikusihi usidharau udogo wa matumizi na kuona hauna madhara kwenye mpango wako wa kifedha. Kwenye programu ya NGUVU YA BUKU, ambapo mpango ni kuokoa angalau elfu 1 kila siku na kuiwekeza kwa muda mrefu, tunaona jinsi ambavyo fedha hizo ndogo ndogo zina nguvu pale zinapowekezwa kwa muda mrefu.

Hivyo kama utaweza kuokoa fedha ndogo ndogo ambazo ungezitumia, kwa kujizuia kutembea nazo na ukawekeza, utajiweka kwenye nafasi ya kujenga utajiri mkubwa kwa kipindi kirefu kijacho.

Lakini pia faida nyingine ya hilo ni tabia unayojijengea. Kila kitu kwenye maisha kinaongozwa na tabia, ambayo unaweza kuijenga kwenye eneo moja lakini pia ikatumika kwenye eneo jingine. Kama ukiweza kudhibiti matumizi madogo madogo kwa kutokuwa na fedha, utaweza pia kudhibiti matumizi makubwa. Maana ukishajenga tabia ya kudhibiti matumizi, inakuwa na manufaa kwenye maeneo yote ya maisha yako.

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutajirika Kwa Kuanza Na Shilingi Elfu Moja.

Rafiki, umeshajifunza zoezi dogo ambalo lipo ndani ya uwezo wako kufanyia kazi na likawa na manufaa makubwa. Anza kulifanya mara moja, kila unapokuwa na fedha ndogo ndogo ziache nyumbani na tembea na fedha kubwa tu. Usifanye matumizi yoyote madogo ambayo siyo lazima kabisa. Ona uchungu kutoa fedha yako kubwa kwa ajili ya matumizi madogo na kwa kufanya hivyo kwa muda mrefu, utaokoa kiasi kikubwa cha fedha.

Pia hatua muhimu ya kuchukua ni kuhakikisha upo kwenye programu ya NGUVU YA BUKU ili hizo fedha ndogo ndogo unazookoa kwenye matumizi uweze kuziwekeza kwenye maeneo ambayo yanazalisha faida na kukua thamani. Kupata nafasi kwenye programu hii ya NGUVU YA BUKU, tuma ujumbe wenye maneno NGUVU YA BUKU kwenda namba 0678 977 007 na utapewa utaratibu wa kujiunga.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimefafanua zaidi dhana hii ya kuepuka kutembea na fedha ndogo ndogo ili kudhibiti matumizi. Karibu uangalie kipindi hicho hapo chini ili uendelee kujifunza na kuchukua hatua ili kudhibiti matumizi yako ya fedha.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.