3382; Soko ndiyo linaamua.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Tuna wajibu wa kutoa thamani kubwa kwa wengine, kwa sababu hiyo ndiyo njia ya kulipwa kwa kiwango kikubwa.
Tunalipwa kulingana na thamani tunayotoa kwa wengine.

Lakini sasa, soko ndiyo linaamua kama tunayotoa ni thamani au siyo thamani.
Sisi tunaweza kuweka juhudi kubwa sana katika kuandaa na kutoa thamani hiyo.
Lakini soko ndiyo litaamua kama kweli hiyo ni thamani au siyo.

Na soko halitaamua kwa upendeleo au uonevu, bali litaamua kwa utayari wake kulipia.
Kama wale unaowalenga kwa thamani unayotoa hawapo tayari kulipa fedha kuipata, basi huo ni mrejesho kwamba hakuna thamani kubwa hapo.
Watu wana uhaba wa fedha, lakini wanapokutana na kitu ambacho kina thamani kubwa kwao, huwa wanahakikisha wanapata fedha za kukipata.

Haijalishi kwa upande wako unaona umetoa thamani kubwa kiasi gani, kama wale unaowalenga hawapo tayari kulipa ili kupata thamani hiyo basi siyo thamani kubwa kama unavyodhani.
Au kama ni thamani kubwa kweli, basi uliowalenga siyo sahihi.

Kwa kujua hili kuhusu soko, unapaswa kuijaribu kwanza thamani kabla ya kuitoa kwa wingi.
Kwa sababu haina maana kufanya uwekezaji mkubwa kwenye kitu ambacho unaowalenga wala hawana muda nacho.
Na njia ya kujaribu soko siyo kwa kuuliza watu kama wana uhitaji au la, maana kwa kuwauliza tu, watakujibu kile unachotaka kusikia ambacho siyo uhalisia wao.
Kuupata ukweli wa soko, njoo na kitu ambacho wateja wanapaswa kulipia kabisa, halafu angalia kama wapo tayari kulipia.

Kila wakati kwetu ni wa kupima thamani halisi ya kile tunachotoa kwa kuliangalia soko. Maamuzi ambayo watu wanayafanya kwenye matumizi ya fedha zao, ndiyo yanayoonyesha uhalisia kuliko yote wanayosema.

Endelea kuleta thamani mpya kila mara kwenye soko na endelea kupima mapokeo ya somo. Fanya maboresho kulingana na mapokeo hayo mpaka uweze kufidiwa kwa usahihi na soko unalolenga.

Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, hatulazimishi mambo yawe vile tunavyotaka sisi. Tunaenda nayo vile yanavyopokelewa na wale tunaowalenga na kuboresha mpaka tunapata kile tunachotaka.
Tunajua kiwango chetu cha kuathiri ni kwenye maandalizi tunayofanya na juhudi tunazoweka.
Mapokeo hayapo kwenye udhibiti wetu, hivyo tunajifunza kutoka kwenye soko kwenye hilo na kisha kuboresha mpaka tupate matokeo tunayoyataka.

Tunajua kura ya kweli ambayo watu wanapiga ni matumizi ya fedha zao. Kama tunachowapa hakiwasukumi kutoa fedha walizonazo, basi hakuna thamani kubwa kama tunavyodhani.
Wajibu wetu ni kurudi kwenye meza na kuboresha zaidi mpaka soko lielewe thamani na kuwa tayari kuilipia.

Kwa kuwa mdadisi na kuendelea kufuatilia kwa karibu bila kuchoka, unajifunza mambo mengi na ukiyafanyia kazi, utaweza kupiga hatua kubwa.
Nenda na soko unalolenga kwa njia hiyo ili kufanya makubwa zaidi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe