Rafiki yangu mpendwa,
Mwandishi Stephen Covey kwenye kitabu chake kinachoitwa The 7 Habits Of Highly Effective People ametufundisha misingi sahihi tunayopaswa kuijenga ili kuweza kuwa na mafanikio makubwa na ya kudumu kwenye maisha yetu.
Kwenye misingi ambayo anatufundisha kwenye kitabu chake, ameeleza umuhimu wa kuwa na MAONO BINAFSI, UONGOZI BINAFSI na USIMAMIZI BINAFSI ili kuweza kujenga mafanikio kwenye maisha.
Kwenye somo lililopita tulijifunza kuhusu MAONO BINAFSI na UONGOZI BINAFSI, unaweza kurejea kwa kubonyeza hayo maandishi. Somo hili tunakwenda kuangalia USIMAMIZI BINAFSI tunaopaswa kujijengea ili kujenga mafanikio makubwa. Hiyo ni tabia ya tatu kwenye tabia 7 ambazo Covey anatufundisha.

Pia kwenye somo hili tutajifunza tabia ya nne kuhusu ushirikiano sahihi na wengine ili kuweza kupata yale tunayoyataka. Karibu ujifunze kwa kina na ukayafanyie kazi haya unayojifunza ili kujenga mafanikio makubwa na ya kudumu kwenye maisha yako.
TABIA YA TATU: FANYA VITU VYA KWANZA KUWA KWANZA; MSINGI WA USIMAMIZI BINAFSI.
Mambo mengi, muda mchache ni kauli maarufu kwenye zama hizi. Hiyo ni kwa sababu mambo ya kufanya ni mengi na yanaongezeka kila siku, huku muda wetu ukibaki kuwa ule ule ambao ni masaa 24 tu kwa siku.
Kumekuwa na vizazi vinne vya njia za kuwa na usimamizi na udhibiti wa matumizi mazuri ya muda ili kuweza kufanikiwa.
Kizazi cha kwanza kilihusu kuwa na orodha ya mambo ya kufanya (TO DO LIST) na kufuata hiyo.
Kizazi cha pili kikahusu kutumia kalenda na kuweka miadi ili kutumia muda vizuri.
Kizazi cha tatu kikaleta pamoja cha kwanza na cha pili, kwa kuwa na orodha na kupangilia kalenda, ila kwa kuwa na vipaumbele.
Vizazi vyote vitatu havikuweza kuleta suluhisho la uhakika, kwani bado watu wamekuwa na changamoto ya muda, kwa kuzingatia mambo mengi ambayo yanapaswa kufanyika.
Kizazi cha nne ambacho mwandishi ameshirikisha kwenye kitabu hiki, kinahusisha mtu kujisimamia wewe mwenyewe kwanza ndiyo uweze kusimamia muda. Mwandishi anaeleza kuhangaika kusimamia na kudhibiti muda bila ya kujisimamia wewe mwenyewe ni kujisumbua.
Muda hauna tatizo, upo vile vile kila siku, wewe ndiye ambaye una tatizo. Hivyo badala ya kuhangaika na usimamizi wa muda (TIME MANAGEMENT) unatakiwa kuhangaika na usimamizi wako binafsi (PERSONAL MANAGEMENT).
Katika kujisimamia binafsi, mwandishi ameshirikisha madirisha manne ya kufanyia kazi, kulingana na umuhimu (important) na uharaka (urgency) wa mambo ya kufanya. Madirisha hayo ni kama inavyoonekana hapo chini;
JEDWALI LA USIMAMIZI BINAFSI ILI KUTUMIA MUDA WAKO VIZURI.
| HARAKA (URGENT) | SIYO HARAKA (NOT URGENT) | |
| MUHIMU (IMPORTANT) | DIRISHA LA I; – Dharura – Matukio ya haraka – Tarehe za mwisho (deadline) | DIRISHA LA II; – Kinga – Kuweka mipango – Kutambua fursa mpya – Kujenga mahusiano. – Mapumziko |
| SIYO MUHIMU (NOT IMPORTANT) | DIRISHA LA III; – Simu zinazoita – Jumbe mbalimbali – Mikutano – Dharura zisizo na madhara | DIRISHA LA IV; – Habari – Kufuatilia mambo ya wengine – Kuperuzi mitandao ya kijamii – Starehe |
Dirisha la kwanza ni la mambo ambayo ni muhimu kufanya na yanapaswa kufanyika kwa haraka. Hayo ni mambo ambayo unapaswa kuchukua hatua za kuyafanya mara moja, kwani usipofanya hivyo madhara yake yanakuwa makubwa. Mambo haya yatapungua pale utakapofanyia kazi dirisha la pili kwa uhakika.
Dirisha la pili lina mambo ambayo ni muhimu kufanya, ila hayana uharaka wa kuyafanya. Hapa ndipo maisha yako yanapopaswa kuwa na ufanye mengi zaidi kwenye dirisha hili. Kwa sababu siyo mambo yenye haraka, huwa ni rahisi kuahirisha na baadaye yanakuja kugeuka na kuwa dirisha la kwanza. Msingi mkuu wa tabia hii ya tatu ni kuyajenga maisha yako yote kwenye dirisha la pili, kwa kufanya mambo yaliyo muhimu wakati ambapo siyo haraka kuyafanya.
Dirisha la tatu lina mambo ambayo ni ya haraka kufanya, lakini siyo muhimu. Haya huwa yanachukua muda wako kuhangaika nayo, lakini mchango wake huwa siyo mkubwa kwenye mafanikio unayotaka kujenga.
Dirisha la nne lina mambo ambayo siyo muhimu kufanya na wala hayana uharaka wa kufanya. Mambo hayo ni usumbufu kabisa kwako na hayana maana yoyote kufanya. Ila huwa yanafurahisha kufanya kwa sababu yanafanya mtu ujisikie vizuri.
Katika kujijengea usimamizi binafsi ili uweze kutumia muda wako vizuri na kufanikiwa, mwandishi anatuasa tufanye hivi; TUFUTE KABISA MAMBO YOTE YA DIRISHA LA III NA IV NA TUPELEKE MUDA WETU KWENYE DIRISHA LA II NA LA I. Baada ya muda mfupi wa kufanya hivyo, hatutakuwa na mambo mengi kwenye dirisha la I na hivyo kuweza kujenga maisha yetu kwenye daraja la II pekee. Na hivyo ndivyo tunavyoweza kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yetu.
Kwa kuleta pamoja tabia tatu za ushindi binafsi;
Tabia ya kwanza inatupa nguvu ya kuwajibika kujenga maisha tunayoyataka.
Tabia ya pili inatupa nguvu ya kujiongoza kwenye kujenga maisha hayo.
Tabia ya tatu inatupa nguvu ya kujisimamia katika kuchukua hatua za kuyajenga maisha hayo tunayoyataka.
Jijengee tabia hizi tatu ili uweze kupata ushindi binafsi na utakaokuwa msingi mkuu wa mafanikio makubwa na yatakayodumu kwenye maisha yako.
SOMA; Huu Ndiyo Ushindi Binafsi Unaopaswa Kuupata Ili Uweze Kufikia Mafanikio Makubwa Kwenye Maisha Yako.
TABIA YA NNE: FIKIRI USHINDI KWA WOTE (WIN/WIN).
Baada ya kuwa na ushindi binafsi wa ndani, kinachofuata ili kuwa na mafanikio kwenye maisha ni ushindi wa umma wa nje. Ushindi huu unatokana na namna unavyoshirikiana vizuri na watu wengine.
Ushirikiano mzuri na watu wengine unaanzia kwenye matokeo ya ushirikiano mnaokuwa nao. Kuna matokeo ya aina sita pape watu wanaposhirikiana;
Moja ni WIN/WIN, haya ni matokeo ya pande zote kupata ushindi. Haya ndiyo matokeo bora ambayo yanajenga ushirikiano mzuri baina ya watu kwa sababu kila mtu ananufaika.
Mbili ni WIN/LOSE, haya ni matokeo ambayo mtu anahakikisha anapata ushindi kwa kuwazidi wengine. Hapa mtu ananufaika wakati wengine hawanufaiki. Matokeo haya yanaweza kumpa mtu ushindi mara chache, lakini hayampi ushirikiano mzuri na wengine.
Tatu ni LOSE/WIN, haya ni matokeo ambayo mtu anakubali kushindwa na kutoa ushindi kwa upande mwingine. Hapa mtu anachagua kuwanufaisha wengine bila ya yeye kunufaika. Ni matokeo yanayotumiwa zaidi na wale wanaotaka kuwafurahisha wengine. Matokeo haya huwa hayajengi ushirikiano mzuri.
Nne ni LOSE/LOSE, haya ni matokeo ambayo mtu anahakikisha wote wanakosa. Haya ni matokeo ya kukomoa, hasa pale mtu anapoona anakosa basi anahakikisha na wengine nao wanakosa. Matokeo haya huwa yanaharibu sana mahusiano.
Tano ni WIN, haya ni matokeo ambapo mtu anakazana kushinda bila ya kuhangaika na wengine. Hapa mtu anaangalia ushindi wake tu na hahangaiki kuwashinda wengine. Matokeo haya huwa ni kwa wale wanaohangaika na mambo yao binafsi.
Sita ni WIN/WIN or NO DEAL, haya ni matokeo ambapo mtu anakazana kila upande kupata ushindi na kama hilo haliwezekani basi hawaendelei na majadiliano. Haya ni matokeo ya kukubaliana kutokukubaliana na kuweka mahusiano mbele ya makubaliano. Kama hayatapatikana matokeo yanayowanufaisha wote, mazungumzo yanaachwa ili kutoa fursa nzuri kwa wakati mwingine.
Aina zote za matokeo zinaweza kutumika katika nyakati tofauti tofauti. Kwa mfano mtu anaposhiriki mashindano ya michezo, mshindi anaweza kuwa mmoja tu na wengine wanakuwa wameshindwa. Kadhalika kwenye mahusiano, mtu unaweza kukubali kupoteza kuliko kukazana kushinda na ukaharibu mahusiano.
Lakini katika yote, matokeo ya pande zote kushinda, WIN/WIN, ndiyo matokeo bora ambayo tunapaswa kuyapambania kwenye makubaliano yoyote tunayoingia na wengine. Haijalishi ni kwenye eneo gani la maisha yetu, kama tunataka ushindi ambao unatupa mafanikio makubwa na ya kudumu, basi tuhakikishe tunawapa wengine ushindi pia.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala mzuri juu ya tabia hizi mbili, ya USIMAMIZI BINAFSI na USHINDI KWA WOTE. Karibu usikilize kipindi hapo chini, ujifunze na kwenda kuweka kwenye matendo ili kujijengea mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.