Kwenye maisha na utendaji wako naamini naamini kuna vitu vidogo vidogo unafanya na kuviona havina shida. Kwa kuwa unaona ni vidogo huoni shida lakini nikumbushe kuwa, “Usipoziba ufa, utajenga ukuta” kama wasemavyo wahenga. Msemo huu una maana kubwa katika utendaji wetu.

Hata katika biashara una nguvu kubwa, hasa yale makosa madogo madogo yasipodhibitiwa huleta shida kubwa katika biashara. Kama tunavyojua sisi binadamu tulivyo, jambo dogo linapotokea tunashirikisha kwa watu wa karibu. Hapa chini ipo simulizi ya bwana mmoja, ifuatilie;

Mr. Jamada amekuwa ukichukua kahawa katika mgahawa fulani kwa muda wa miaka 3. Siku moja akaenda katika mgahawa ule, ikatokea akasubiria huduma kwa muda mrefu bila kujua sababu ni nini. Mr. Jamada katika mgahawa ule hakuwa mgeni, wanamjua jina na kila kitu kuhusu yeye, lakini huduma ilichelewa tofauti na ilivyo kawaida, na hawakumtaarifu kwa chochote.

Mwishowe akamua kurudi nyumbani kwake bila kupata huduma. Maana wahudumiaji wote walikuwa wanazunguka zunguka tu.

Alipoondoka akawashirikisha baadhi ya watu wake wa karibu juu ya namna alivyoshindwa kupewa huduma. Watu wake wa karibu walichukizwa na taarifa hiyo. Kumbe, kulikuwa na migogoro baina ya wafanyakazi na bosi wa mgahawa ule. Ndiyo maana hata huduma hazikuwa vizuri.

Je, kama ni wewe umefika sehemu ya huduma ungesubiri au utaanza kufikiria nini? Nina uhakika kuna kitu utaanza kufikiria, utakuwa na mtazamo usio mzuri. Hutokumbuka namna nzuri ulivyohudumiwa nyuma. Bali utaangalia na kufanya maamuzi juu ya kosa lililotokea leo.
Ukishafanya maamuzi hata muuzaji au meneja wa mgahawa aje na maneno ya namna gani sio rahisi kurudi nyuma. Ikiwa ni hasira itapanda tu.

Ndivyo ilivyo kwenye biashara zetu, makosa madogo madogo yanayoendelea kujitokeza yanasababisha watu kutuona sio watoa huduma wazuri.

Unapokuwa kwenye uhudumiaji, moja ya sera nzuri kuongozwa nayo ni hii, “kosa halipaswi kufanyika” (make no mistake).  Kosa likijitokeza suluhu, ni marekebisho ya haraka.

Inahitaji utatue tatizo kabla halijaonekana kwa watu. Maana likishaonekana kwa watu litaleta mitazamo mibaya, hali itakayoongeza shida zaidi. Chukulia koki ya maji kwenye tenki imepata hitilafu kidogo na maji yanatoka kidogo kidogo. Unadhani itachukua muda gani maji kuisha kwenye tenki? Siyo muda mrefu, yataanza kidogo mwishowe kuisha kabisa.  Hivyo, suluhu ni kuziba mahali maji yanapotokea. 

Hata kwenye biashara ipo hivyo. Kosa dogo likipewa nafasi, huruhusu mianya ya makosa mengi kupenya na kusababisha wateja wanaikimbia biashara.

Makosa ya kuepuka ni kama;

Moja; Kutomsikiliza mteja

Mbili; Uzembe na Ukali wa wahudumiaji.

Tatu; Kutotabasamu kwa wahudumiaji.

Nne;  Kukosekana kwa vitu walivyoagiza.

Tano. Utoaji wa huduma taratibu.

Hapo kuna baadhi ya makosa yaliyoukumba mgahawa alioenda Jamada. Kama yalitoke pale, basi hata kwako inaweza kutokea pia, ikiwa hutoweza kuongeza umakini kudhibiti makosa madogo madogo. Kujitoa katika hali hiyo zingatia haya;

Moja; Timiza ahadi
Mbili; Umanifu
Tatu; Usafi
Nne; Maelewano kati ya staff wote
Tano; Tabasamu pamoja na kusikiliza

Kumbuka; Kutoelewana na mwajiri wako hakuna uhusiano na kumhudumia mteja. Hivyo, hakikisha ukiwa na mgogoro na bosi usiuonyeshe direct kwa mteja wako. Vile vile makosa madogo madogo usiruhusu yaonekane mbele ya mteja wako.

Kitu pekee anachokumbuka mteja ni namna ulivyomfanya ajisikie vizuri wakati wa uhudumiaji. Je, ni kitu gani unachukia unapoenda kupata huduma?

Imeandaliwa na Lackius Robert Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo Na Mwandishi. Tuwasiliane 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz.