Mafanikio ni kitu ambacho kimeandikiwa vitabu na makala nyingi sana. Kuna maarifa mengi sana yametolewa kuhusu mafanikio. Kuna mbinu na siri nyingi mno zimeshafundishwa kuhusu mafanikio. Lakini pamoja na hayo yote, bado ni watu wachache sana ambao wana mafanikio makubwa.Je kuna nini hapa? Je kuna siri kubwa zaidi ambazo hazifundishwi kuhusu mafanikio? 

Ambazo wachache wanazo na wengine hawazijui? Au labda kuna bahati ambayo wachache wanaipata na wengi wanaikosa? Au kuna watu fulani wamepangiwa kufanikiwa na wengine wakapangiwa kutokufanikiwa?

Haya ni maswali ambayo mwandishi Michael Bolduck anayajibu kupitia kitabu alichoandika kinachoitwa Power Of Motivation.

Michael anatufundisha ya kwamba, maarifa pekee hayatoshi, iwapo nguvu kubwa ya hamasa inakosekana. Anatufundisha nguvu kuu mbili ambazo zinatusukuma kuchukua hatua na jinsi ya kuzitumia ili kufanikiwa zaidi.

Michael anatuambia ya kwamba wale ambao hawafanikiwi siyo kwa sababu hawana maarifa sahihi, ila nguvu ya hamasa inafanya kazi kuwazuia kufanikiwa. Anachosema ni kwamba, unaweza kutumia nguvu ya hamasa kufanikiwa, au nguvu ya hamasa ikafanya kazi na wewe usifanikiwe.

Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu hichi, tuweze kujifunza kwa pamoja na kuweza kutumia nguvu ya hamasa ili kufanikiwa zaidi.

1. Watu hawataki mafanikio.

Watu wengi wanapata kile wanachopata sasa, kwa sababu wanaridhika na wanachokipata. 

Ingekuwa hawaridhiki, wasingeendelea kufanya vile wanavyofanya, wangebadili kitu. 

Hivyo kama upo mahali ambapo umekwama kwa muda mrefu, jua tu kwamba umechagua kubaki hapo, ungekuwa hupataki, ungetafuta kila njia ya kuondoka. Na ungeipata.

2. Mafanikio yanahitaji ujasiri.

Ukiangalia kwa ndani, wanaofanikiwa siyo kwamba wanafanya mambo ya tofauti sana ambayo wasiofanikiwa wanashindwa kuyafanya, bali wanakuwa na ujasiri wa kufanya mambo ambayo wale wasiofanikiwa hawathubutu kuyafanya. Na siyo kwamba wao hawana hofu, wanakuwa nayo lakini wanafanya licha ya hofu zao. Unahitaji kushinda hofu zako na kuchukua hatua ili kufanikiwa.

3. Upo tayari kufanya kila linalowezekana ili kufanikiwa?

Kuanza mambo mapya wengi wanaanza, ila pale mambo yanapokuwa magumu, ndipo wanaofanikiwa wanapotofautiana na wanaoshindwa. Wanaoshindwa wanakata tamaa na kuacha, pale mambo yanapokuwa magumu. Lakini wanaofanikiwa wanakuwa wamejipa kiapo kwamba watafanya kila linalowezekana kuhakikisha wanafanikiwa. Hawakubali kurudishwa nyuma na chochote, na dunia inawapa kile wanachotaka.

4. Nguvu kuu mbili zinazotusukuma kuchukua hatua;

Ya kwanza ni TAMAA YA KUPATA (DESIRE FOR GAIN)

Ya pili ni HOFU YA KUPOTEZA (FEAR OF LOSS)

Chochote kile ambacho unafanya kwenye maisha yako, ni kwa msukumo wa nguvu hizo mbili. Unafanya kwa sababu kuna kitu unataka kupata, au unafanya kwa sababu kuna kitu unahofia kupoteza.

Nguvu hizo mbili, ndiyo unazoweza kutumia kutengeneza hamasa kubwa ambayo itakuwezesha kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako.

5. Kama hakuna maumivu, hutaweza kuchukua hatua.

Kitu kikubwa ambacho kila binadamu anakiogopa na kukikwepa sana ni maumivu, hasa yale ya kupoteza kitu. Mtu akipewa nafasi ya kupata shilingi elfu kumi na ya kupoteza shilingi elfu kumi, atachukua hatua ya kuzuia kupoteza.

Hivyo kama hakuna maumivu ya kitu unapoteza, hutasukumwa sana kuchukua hatua. 

Ndiyo maana unapoweka malengo yako, unapaswa kuwa na kitu ambacho utapoteza kama hutachukua hatua, na kwa njia hiyo utapata msukumo zaidi wa kuchukua hatua.

6. Furaha ni msingi muhimu wa mafanikio.

Furaha na mafanikio ni kitu ambacho kimekuwa kinachanganya wengi. Ambao hawafanikiwi, wamekuwa wakiamini kwamba wakifanikiwa ndiyo watakuwa na furaha. 

Waliofanikiwa wamekuwa wakiamini kwamba furaha ndiyo inawaletea mafanikio. Na ukweli ni ule wa waliofanikiwa, furaha ndiyo inaleta mafanikio, na siyo mafanikio kuleta furaha.

Furaha ni kitu ambacho kinaanzia ndani yetu, kwa namna tunavyofanya maamuzi yetu, imani zetu na hatua tunazochukua.

7. Aina kuu mbili za hamasa ya mafanikio.

Moja; hamasa ya ndani, huu ni ule msukumo unaotoka ndani ya mtu mwenyewe, wa kutaka kufanya jambo ili kuwa bora zaidi au kuwanufaisha wengine.

Mbili; hamasa ya nje, huu ni ule msukumo unaotoka kwa wale wanaokuzunguka.

Katika aina zote hizi mbili za hamasa, ila mtu anafanya kitu kutokana na tamaa ya kupata, au kuepuka kupoteza na maumivu.

8. Kanuni kuu ya mafanikio kifedha.

Mafanikio kifedha yanaongozwa na kanuni kuu moja, matumizi yako yawe madogo kuliko kipato chako, na tofauti hiyo ya matumizi na kipato iwekezwe sehemu ambapo inaweza kuzalisha zaidi. Na ili uweze kutekeleza hili, lazima uwe na hamasa ya kuweza kudhibiti matumizi yako na kuongeza kipato chako.

Ukifanya kinyume na kanuni hii, huwezi kamwe kufanikiwa kifedha.

9. Hatua nane za kufikia uhuru wa kifedha.

Kama unataka kufikia uhuru wa kifedha, kwanza lazima uwe tayari kuweka kazi na muda unaopaswa kuweka ili kufikia uhuru huo. Hakuna njia ya mkato na wala usitamani kushinda bahati nasibu. Badala yake fuata hatua hizi nane.

Moja; furahia mchakato mzima. Safari itakuwa ndefu, changamoto zitakuwa nyingi, itakuwa vizuri kwako kama utafurahia kile unachofanya.

Mbili; tengeneza mpango kamili wa kufikia uhuru wa kifedha, kisha ufanyie kazi. Kitu kisichopangwa, huwa hakifanyiki. Jua unataka kufika wapi na kwa wakati gani.

Tatu; kuwa tayari kufanya mambo ambayo hupendi kufanya, dhibiti matumizi yako, ongeza kipato chako.

Nne; wekeza vizuri, kwa mipango mizuri ya kutengeneza kipato baadaye.

Tano; fuatilia mwenendo wako, kila hatua unayopiga, angalia kama upo kwenye uelekeo sahihi.

Sita; tegemea mazuri lakini jiandae kwa mabaya. Utakutana na changamoto, utapanga lakini matokeo yatakuwa tofauti, jiandae kwa matokeo tofauti ili usikwame na kurudi nyuma.

Saba; tengeneza na endeleza hamasa yako. Lazima uwe na kitu cha kukusukuma, hata pale mambo yanapoonekana magumu.

Nane; kuwa na mtu wa kukusimamia na kukupa mwelekeo sahihi. Unahitaji kuwa na kocha, ambaye atakufuatilia kwa mipango yako na kuhakikisha upo kwenye njia sahihi.

10. Usihusishe maumivu na mpango wako wa kifedha.

Watu huwa wanaweka mipango mikubwa ya kifedha, lakini wanashindwa kuifuata kwa sababu wanaihusisha na maumivu. Kama ni kudhibiti matumizi basi wanaona maisha yao yatakuwa magumu kwa kukosa vile wanavyopenda. Au kuongeza kipato wanaona maisha yatakuwa magumu kwa kufanya kazi zaidi. Kwa kuwa hamasa yetu ipo kwenye kuepuka maumivu, basi tunaepuka mipango hiyo.

Hatua nzuri ya kuanzia ni kutokuhusisha maumivu na mipango yetu ya kifedha, badala yake tuihusishe na kupata uhuru wa kifedha na kuwa na maisha bora, ili tuwe na hamasa ya kufikia.

11. Njia bora ya kuhakikisha hurudi nyuma.

Unapoweka mipango mizuri na mikubwa, una hatari ya kuiacha pale mambo yanapokuwa magumu. Kuepuka hilo kutokea unapaswa kuwa na mtu ambaye anakufuatilia. 

Unachofanya ni kumwambia mtu ule mpango ambao unafanyia kazi, kisha yeye akufuatilie, na ukikata tamaa, basi utamlipa fedha. Hapo unahitaji kuweka kiasi kikubwa cha fedha ambacho kitakuuma ukikipoteza, na unayempa awe mtu ambaye wala hakuhusu. Hilo litakupa msukumo wa kuendelea hata pale unapokaribia kukata tamaa.

12. Kanuni ya mafanikio kiafya.

Mafanikio kiafya ni kuwa na afya bora, ambayo hii itatokana na vitu vitatu muhimu;

Moja ni vyakula unavyokula, unapaswa kula zaidi vyakula vinavyotokana na mimea, matunda na kuepuka vyakula vya viwandani.

Mbili ni mtindo wa maisha, hapa inahusu kufanya mazoezi, kupata muda wa kupumzika na mahusiano bora na wengine.

Tatu ni kuulinda mwili dhidi ya magonjwa na hatari nyingine.

13. Mwili wako una uwezo mkubwa.

Mwili wa binadamu una uwezo mkubwa sana ndani yake, kama utapelekwa kwa njia ya asili. Mwili una uwezo mkubwa wa kupambana na magonjwa na hata kujitibu, iwapo tu utapata mahitaji yake kwa njia za asili. Lakini mwili unapokuwa na sumu nyingi, kutokana na kukosa vyakula vya asili, unapoteza nguvu hii ya kujilinda na kujitibu.

14. Ufunguo wa mafanikio una vitu vinne muhimu.

Moja; jua ni nini hasa unachotaka.

Mbili; chukua hatua kubwa sana kuweza kupata kile unachotaka.

Tatu; angalia kipi kinafanya kazi na kipi hakifanyi kazi.

Nne; badili njia zako kulingana na kile kinachofanya kazi ili uweze kufika unakotaka kufika.

Hatua hizo nne, ni mfumo wa mafanikio ambao haushindwi kamwe.

15. Mafanikio ni rahisi, hamasa ndiyo ngumu.
Mafanikio siyo magumu, ugumu upo kwenye hamasa ya kuweza kuendelea na mpango ulioweka, hata pale mambo yanapokuwa magumu sana.

Ukiweza kutengeneza hamasa kubwa kwako utakuwa na uhakika wa kufikia mafanikio makubwa.

16. Aina mbili za watu duniani.

Hapa duniani, wapo watu wa aina mbili;

Aina ya kwanza ni wale ambao ni wajengaji, hawa ni watu ambao wana mchango mkubwa kwa wengine na dunia kwa ujumla. Wanachukua hatua ya kutoa ili kuifanya dunia kuwa bora zaidi.

Aina ya pili ni wale ambao ni wabomoaji, hawa kila wanachofanya wao ni kuchukua tu, hawachangii chochote. Wana mtizamo hasi, wa kukosoa na kukatisha tamaa. Wanaharibu watu, mazingira na hata dunia kwa ujumla. Wanataka kupata tu, lakini hawapo tayari kutoa.

17. Utumwa wa kujitakia.


Watu wengi hapa duniani, wamekuwa watumwa wa kujitakia, kwa kukubali kuendeshwa na tamaa zao. Tamaa hizi zinatokana na zile nguvu mbili, kupata na kuogopa kupoteza. 

Unaposhindwa kuzitawala tamaa hizo, unaishia kuwa mtumwa.

18. Ukweli ndiyo uhuru na mafanikio.

Ukweli umekuwa mgumu na adimu kwa sababu moja, watu wanaona vitu kama wanavyotaka kuona, na siyo kama vilivyo. Ili kuwa na mafanikio, unahitaji kuujua ukweli, na hatua ya kwanza ya kufanya hivyo ni kuona vitu kama vilivyo, na siyo kuviona kama unavyotaka wewe.

Kama utataka kupata ukweli, kwa kuhoji na kudadisi, utaona vitu kama vilivyo.

19. Sheria ya majukumu.

Kila kitu kinachotokea kwenye maisha yako, kimesababishwa, hakuna ajali. Kila kinachotokea kimesababishwa na hatua ulizochukua au kutokuchukua huko nyuma. Kama biashara yako inakufa, ni kwa sababu ulifanya uzembe huko nyuma. Kama kazi yako hailipi ni kwa sababu ulifanya uzembe, labda wa kukosa elimu sahihi ambayo ingeongeza thamani yako, au kuweka juhudi kwenye kazi ambayo ingeongeza kipato chako.

Ili kufanikiwa, lazima ubebe majukumu ya maisha yako na uache kutafuta watu wa kuwalaumu. Wewe ndiye mhusika mkuu wa mafanikio na kushindwa kwako, chukua hatua.

20. Kuwasaidia wengine, hakikisha wewe unakuwa bora kwanza.

Iwapo una msukumo wa kuweza kuwasaidia wengine kuchukua hatua, anza kuchukua hatua wewe kwanza. Kama unataka kuwawezesha wengine kuwa na maisha bora, anza kuwa na maisha bora wewe kwanza. Na muhimu zaidi, lazima uwapende wale ambao unataka kuwasaidia na kuwahamasisha.

Nguvu ya hamasa ya mafanikio ni namna mtu unavyofanya maamuzi ya maisha yako, kwa kujua nini unataka kwenye kila eneo la maisha yako, kujua hatua unazopaswa kuchukua na kuzichukua, bila ya kukata tamaa, hata pale mambo yanapokuwa magumu. 

Na hii ndiyo inatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita