MAKIRITA AMANI:
Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.

Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora.

Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu DUNIA KUTAKA WEWE UWE KAWAIDA…

Hivi umewahi kujiuliza kwa nini watu wanaokataa kuwa kawaida ndiyo wanaoshambuliwa sana?

Wale watu ambao wanachagua kufanya vitu vya tofauti ndiyo wanaoonekana wanakosea, wana matatizo, watashindwa na hata wakati mwingine kuonekana wanapotea.

Hii ni kwa sababu, dunia inataka wewe uwe wa kawaida, ufanye kile ambacho kila mtu anafanya, na maisha yako yawe sawa na ya kila mtu.

Utakapojaribu kufanya tofauti, ndipo utakapopata maoni ya kila mtu, kukuonesha namna gani unakosea.

Unapaswa kujua hili kwa sababu ndiyo kikwazo cha kwanza kwa mafanikio yako.

Hutaweza kufanikiwa iwapo hutaweza kuvuka kizuizi hichi cha dunia.

Kwa kujua kabisa kwamba unapochagua kufanya vitu vya tofauti, watu hawatafurahishwa na hilo, hivyo watataka uache, ndiyo maana watakukatisha tamaa.

Kataa kuwa wa kawaida kwenye kazi zako, zifanye kwa viwango vya juu sana na weka ubora wa hali ya juu.

Kataa kuwa wa kawaida kwenye biashara zako, hakikisha kila wakati unatoa thamani kubwa sana kwa wateja wako.

Kataa kuwa wa kawaida kwenye maisha yako, ishi maisha ambayo yana mchango mkubwa kwa wengine.

Unahitaji kuwa mbishi ili kuweza kuishinda dunia kwenye hilo, vinginevyo itakushinda na utakuwa wa kawaida sana.

Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.

Rafiki yako,

Kocha Makirita Amani,

MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.

http://www.makirita.info