Rafiki yangu mpendwa,
Mara nyingi unapokuwa unaanzia chini, yaani kwenye umasikini, kitu pekee unachokuwa unafikiria kwenye mafanikio ni kupata fedha na utajiri. Unakuwa unaamini kwamba kwa kupata fedha na utajiri basi utakuwa na mafanikio na uhuru kwenye maisha yako.
Lakini hivyo sivyo hadithi ya fedha imekuwa inaisha, badala yake matokeo huwa tofauti. Kwanza kabisa wengi hawapati kiasi kikubwa cha fedha ambacho kinaweza kuwaweka huru kwa vile wanavyotaka.

Na kwa wachache ambao wanapata kiasi kikubwa cha fedha, wanakuwa wamezidi kukosa uhuru. Yaani kadiri wanavyokuwa wanapata fedha nyingi, ndivyo wanavyozidi kukosa uhuru.
Kwenye ajira mtu anakuwa anaweka juhudi kubwa na kulipwa kiasi kikubwa, lakini kinakua kimeambatana na majukumu mengine makubwa zaidi. Hivyo licha ya kulipwa vizuri, kazi zinakuwa nyingi na zinazomnyima kabisa uhuru.
Kwenye biashara mtu anakuwa amekazana kujenga biashara inayomwingizia kipato kikubwa, anaajiri watu wa kumsaidia majukumu mbalimbali, lakini biashara haiwezi kwenda bila ya uwepo wake. Yaani licha ya biashara kuwa kubwa, bado inakuwa inategemea uwepo wake wa moja kwa moja.
Hizo ndizo hali ambazo wengi wanazipitia kwenye maisha na kujikuta hawapo huru. Wakiwa hawana fedha wanakosa uhuru na wakiwa na fedha nyingi pia wanakosa uhuru.
SOMA; Hatua Nne (04) Za Kupata Uhuru Wa Muda, Fedha Na Eneo Ili Kuwa Na Maisha Ya Mafanikio.
Ukweli ambao wengi wamekuwa hawaujui ni kwamba uhuru kwenye maisha unapaswa kuanza kabla hata ya mtu kupata fedha nyingi anazotaka. Yaani mtu lazima aanze kufikiria uhuru mapema kabla hata hajakuza kipato chake, ili anapochukua hatua za kukuza kipato, ziwe ni ambazo haziathiri uhuru wake.
Uhuru kwenye maisha unahusisha vitu vinne; NINI, LINI, WAPI na NANI.
NINI – Hapa mtu anaamua nini afanye.
LINI – Hapa anaamua afanye wakati gani.
WAPI – Hapa anaamua afanyie eneo gani.
NANI – Hapa anachagua afanye na nani.
Kama mtu hayupo huru kuchagua maeneo hayo manne, hayupo huru, bila ya kujali ni kipato kikubwa kiasi gani anachoingiza.
Uzuri ni kwamba huhitaji kuwa na kipato kikubwa sana ndiyo uweze kuamua hayo manne. Bali unaweza kuanzia hapo ulipo sasa na kuanza kujenga uhuru wa maisha yako. Kinachohitajika ni utayari wako wa kuyabadili kabisa maisha yako.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimekushirikisha jinsi unavyopaswa kuyabadili maisha yako ili uweze kujijengea uhuru kamili wa maisha yako hata kama bado hujawa na kipato kikubwa sana. Karibu ujifunze na uweze kutoka kwenye gereza lako la kujitakia.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.