3383; Tukio na maisha.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Matokeo ambayo tunayapata kwenye maisha yetu yanategemea sana namna tunavyochukulia kile tunachofanya.
Zipo aina mbili za kuchukulia kile ambacho mtu anafanya.
Moja ni kuchukulia kama tukio.
Hapa mtu anakifikiria kitu wakati wa kukifanya na ambao unakuwa ni mfupi.
Wakati mwingine wote hafikirii kabisa kitu hicho.
Kitu hicho kinakuwa ni tukio la muda mfupi tu kwenye siku yao nzima.
Mbili ni kuchukulia kama maisha.
Hapa mtu anakifikiria kitu muda wote hata muda ambao hakifanyi.
Kila anachofikiri na kufanya kwenye siku yake, anahusisha na kupima kwa kile anachofanya.
Anayechukulia kile anachofanya kama tukio hapati mafanikio makubwa.
Kwa sababu anakipa hicho anachofanya muda mfupi tu na muda mwingine unaenda kwenye vitu vingine tofauti.
Anayechukulia kile anachofanya kama maisha anapata mafanikio makubwa.
Kwa sababu anakipa hicho anachofanya muda mrefu na hivyo kuweza kukielewa kwa undani.
Maisha yake yote anayajenga kumwezesha kufanya hicho kwa manufaa zaidi.
Huwa kuna kauli inayosema, jinsi unavyofanya kitu kimoja, ndivyo unavyofanya kila kitu.
Anayechukulia anachofanya kama maisha, maisha yake yote yanakuwa yanamwezesha kukifanya kwa ubora, kwa sababu ndivyo anavyofanya kila kitu.
Anayechukulia kama tukio, anakuwa na mengine yanayomsumbua na hivyo kushindwa kufanya vizuri.
Ukichagua kufanya biashara kama tukio, utaifikiria biashara wakati upo kwenye biashara tu. Nje ya hapo utakuwa unasumbuka na mambo mengine. Hutaweza kupata ukuaji mkubwa sana, kwa sababu kuna fursa nyingi nzuri zitakupita.
Ukichagua kuifanya biashara kama maisha, unaifikiria biashara kwa muda wako wote. Kila unachofikiri na kufanya kinahusisha biashara yako. Hivyo maamuzi yote unayofanya yanakuwa na manufaa kwa biashara yako.
Kuna vitu vidogo vidogo vingi ambavyo huwezi kuviona kama unafanya kitu kama tukio.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye mafanikio kwenye maeneo yote ya maisha yetu.
Mafanikio yanakuwa makubwa na ya uhakika pale mtu anapokuwa anakifikiria kitu muda wote. Hilo linapeleka umakini wake wote kwenye kitu na hivyo kuziona fursa ambazo kwa wengi hazionekani.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, mafanikio siyo tukio, bali ndiyo maisha yenyewe. Mafanikio ndiyo kitu tulichojitoa kukiishi kila muda wa maisha yetu.
Tumechagua kujitoa kweli kwa ajili ya kupata mafanikio makubwa tunayoyataka. Tuna moto mkubwa unaowaka ndani yetu ambao hatuwezi kuuzima au kuuzuia, ni moto huu ndiyo unatufanya kukaa kwenye safari ya mafanikio muda wote.
Mafanikio kwetu siyo kitu cha kupata au kukosa, bali ni kitu cha kupata kwa uhakika. Ni swala la muda tu kuhusu kuyapata mafanikio, kwa sababu ndiyo maisha yetu na hivyo kadiri tunavyokuwa hai, tunakuwa na uhakika wa mafanikio.
Tunakuwa hatuna njia nyingine mbadala zaidi ya ushindi, kwa sababu hayo ndiyo maisha yetu pekee.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe