3384; Ushindi ni lazima.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Unapoichagua safari ya mafanikio kuna matokeo ya aina mbili, moja ni kupata ushindi na mbili ni kuishia njiani. Ni hivyo tu, hakuna matokeo ya aina nyingine.
Unapata ushindi pale unapokaa kwenye mchakato wako wa mafanikio bila ya kukata tamaa. Licha ya kupitia changamoto na magumu mbalimbali, unaendelea kupambana bila ya kusimama.
Unapata ushindi pale unapokuwa umeamua dhahiri na kujitoa kwa kila namna kuhakikisha unapata ushindi huo.
Unaishia njiani pale unapokata tamaa na kuachana na safari ya mafanikio kabla hujayapata mafanikio uliyoyataka.
Licha ya kuwa ulipanga kabisa nini unataka kupata au kufikia na licha ya kuianza safari, unashindwa kuendelea mpaka upate unachotaka.
Unapokutana na changamoto na vikwazo, unaona safari yako haiwezekani tena na kuacha.
Hapo unakuwa umekubali wewe mwenyewe kushindwa kwa yale mafanikio uliyoyataka.
Na hivyo ndivyo unavyotengeneza maisha ya kushindwa.
Tatizo la kuishia njiani ni unakuwa umekubali kushindwa mara mbili.
Moja unakuwa umeshindwa kupata yale mafanikio ambayo uliyataka.
Na mbili unakuwa umepoteza juhudi zote ambazo unakuwa umeweka mpaka hapo unapokatia tamaa.
Kila juhudi unazoweka kwenye safari yako ya mafanikio zina mchango fulani kwa baadaye. Lakini mchango huo utawezekana pale ambapo unaendelea kufanya bila kuacha.
Ukiacha kufanya kabla hujafanikiwa, unakuwa umepoteza juhudi zote ambazo ulikuwa umeziweka mpaka hatua hiyo.
Kitu kibaya zaidi kwenye kuishia njiani ni majuto utakayoishi nayo kwa kipindi chote cha maisha yako.
Pale unapoishia njiani na kukata tamaa kwenye mafanikio uliyotaka, siyo kwamba utasahau kila kitu.
Bali utaendelea kujikumbusha juu ya mafanikio uliyoyataka na ukakata tamaa.
Utakuwa na majuto ambayo yatakusumbua sana. Kila wakati utakuwa unajiambia huenda ungeweka juhudi zaidi ungefanikiwa.
Kuondokana na yote hayo, chagua safari yako ya mafanikio na komaa hapo mpaka kifo au ufanikiwe.
Kuishia njiani isiwepo kabisa kwenye machaguo yako. Wewe ni kuendelea na mchakato wako kwa kipindi chote cha maisha yako.
Kwa kuamua hivyo, ushindi unakuwa ni wa uhakika, kwa sababu labda utapata unachotaka au utakufa ukiwa unakipambania.
Kwa vyovyote vile huo ni ushindi.
Kama tu hujaacha kufanya, wewe ni mshindi.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, tumechagua kupata ushindi kwa uhakika.
Tumechagua kuendelea na kile tulichopanga bila ya kujali nini tunapitia.
Tunauona kabisa ushindi ambao tunataka kuufikia na tunaupambania bila ya kukwamishwa na chochote.
Mafanikio yetu ya kwanza kwenye KISIMA CHA MAARIFA ni kuiishi kila siku kwa ushindi.
Siku yenye ushindi ni ile ambayo tumeiishi kwa mchakato wetu kamili na kutekeleza yale tuliyoyapanga kama tulivyopanga.
Tunajua kwa kuikabili kila siku kwa namna hiyo, hakuna namna tunaweza kushindwa.
Kwa sababu mwisho wa siku, mafanikio kwenye maisha ni mkusanyiko wa siku ambazo tumeishi kwa ushindi.
Kama kuyaangalia mafanikio yako makubwa kunakufanya utake kukata tamaa na kuishia njiani, basi angalia ushindi wa kila siku.
Kila siku kazana kuishi mchakato wako na kukamilisha yale uliyopanga kukamilisha kila siku.
Kwa kuzikusanya siku nyingi zaidi ambazo umeishi kwa ushindi, unapata maisha ya mafanikio makubwa.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe