Rafiki yangu mpendwa,

Ukisafisha chumba chako vizuri sana, ukapangilia kila kitu kikakaa vizuri halafu ukakiacha bila ya kufanya chochote, baada ya muda utakuta uchafu umeanza tena kujikusanya na vitu kuvurugika. Hiyo ni kwa sababu asili ya vitu huwa ni kuvurugika. Hakuna kitu chochote kinabaki kama kilivyokuwa, kila kitu kinabadilika na mabadiliko mengi ni ya uharibifu.

Hiyo ni kanuni ya asili kabisa ambayo wengi wamekuwa hawaielewi na imekuwa kikwazo kwao kufanikiwa. Wengi hudhani ukishafanya kitu mara moja basi umemaliza, huhitaji kuendelea kuboresha. Matokeo yake ni watu kupiga hatua moja mbele na kurudi hatua mbili nyuma. Matokeo yake ni wanakuwa wameshindwa zaidi kuliko kufanikiwa.

Tunaona mifano mingi kwa watu wanaoanzia chini kabisa, wanapambana na kujenga mafanikio makubwa. Baada ya kupata mafanikio wanajiona wameshamaliza kila kitu na matokeo yake yanakuwa ni anguko kubwa. Hata kwenye vitu kama kupunguza uzito, wanaweza kuchukua hatua ambazo zinapelekea uzito kupungua, lakini baada ya muda wanajikuta uzito umeongezeka kuliko hata ulivyokuwa awali.

Rafiki, mambo yanatokea hivyo kwa sababu pale tunapoweka mipango yoyote na kupata matokeo, kuna mambo huwa yanajipenyeza kidogo kidogo kuharibu mipango na matokeo tuliyopata. Haijalishi ni nini tumefanya, hali ya uharibifu kujipenyeza ni sehemu ya asili kabisa.

Wajibu mkubwa tunaopaswa kutekeleza kwenye safari yetu ya mafanikio ni kugundua yale yanayotaka kujipenyeza mapema na kuyazuia yasilete madhara. Chochote ambacho kinaingilia matokeo tunayoyataka hakipaswi kabisa kupewa nafasi. Kwa sababu vitu vingi huwa vinakuwa dhaifu vikiwa vidogo, lakini vinapokua vinakuwa imara na vigumu kuondoa.

Jua kwenye maisha yako, kujenga na kutunza ni vitu ambavyo havipaswi kuwa na mwisho. Kila wakati unapaswa kuwa unajenga vitu vipya ili upate mafanikio makubwa ziadi. Lakini pia unapaswa kuwa unatunza vitu vya zamani ili kudumisha mafanikio ambayo umeyapata.

Kwa kufanya mambo hayo mawili kwa msimamo, utaweza kujenga mafanikio ambayo yatadumu kwa muda mrefu kwenye maisha yako. Utaepuka uharibifu unaoingilia mafanikio unayojenga na kuyalinda mafanikio yako.

Karibu kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambapo nimeeleza kwa kina zaidi dhana hii ya vitu kujipenyeza na kubomoa mafanikio unayoyajenga. Angalia kipindi hicho hapo chini.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.