3394; Kuwaudhi baadhi ya watu.

Kutoka Mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Kama hakuna watu ambao unawaudhi kwenye maisha yako,
Kama hakuna watu ambao wanakuambia unakosea kwa namna unavyoishi au kufanya mambo yako,
Maana yake huyaishi maisha yako.

Badala yake unaishi maisha ya kuiga yale ambayo wengine wanafanya.
Unakazana kuwaridhisha watu wote.
Na matokeo yake ni hutaweza kufanya makubwa unayotaka kufanya.

Kwenye fedha, kama hakuna watu wanaokuita bahili,
Kama hakuna wanaosema hujui namna sahihi ya kutumia fedha zako.
Kama hawapo wanaodhani wangeweza kutumia fedha zako vizuri kuliko wewe,
Maana yake unatumia fedha zako kwa kufuata mkumbo wa wengine.
Unajaribu kumridhisha kila mtu.
Na matokeo yake ni kupoteza fedha nyingi bila ya manufaa yoyote kwako.

Kwenye masoko, kama hakuna wanaokutukana.
Kama hakuna wanaokuona wewe ni msumbufu.
Kama hawapo wanaosema umezidi kupiga kelele,
Basi hujafanya kazi yako ya masoko kwa kiasi cha kutosha.
Hujapika kelele kubwa hasa na kuwafikia wengi zaidi.
Matokeo yake ni hutaweza kuwafikia wengi zaidi na wakajua kile unachouza.

Kwenye mauzo, kama hakuna wanaokukataa,
Kama hujakataliwa na wengi na kuambiwa usiwatafute tena,
Kama hakuna wanaokukwepa au kutojibu mawasiliano yako,
Basi hujawakamilisha watu na kuwafuatilia vya kutosha.
Maana yake unawauliza tu watu mara moja na kuishia hapo.
Huna ung’ang’anizi wa kutosha katika kuwasisitiza wakamilishe mauzo na katika kuwafuatilia.

Pale tu unapotaka kupata matokeo makubwa kwenye kila eneo la maisha yako, jua kuna watu ambao utawaudhi.
Na hao watakaoudhika na wewe kutaka kufanya makubwa ni ambao siyo sahihi kwako.
Hivyo siyo kwamba hata unawapoteza watu hao unaokuwa umewaudhi.
Badala yake unakuwa umedhihirisha juhudi unazoweka ni sahihi na hivyo matokeo sahihi yatafuata.

Kwenye maisha, huwezi kuwaridhisha watu wote.
Bali unaweza kuwaridhisha wale walio sahihi kwako.
Na ili kuwaridhisha walio sahihi, lazima uwaudhi wasio sahihi.
Kama hakuna kabisa unaowaudhi haimaanishi wewe ni mwema sana.
Bali inamaanisha bado hujayasimamia kweli mafanikio yako.

Kwenye kila eneo la maisha yako chagua ni aina gani ya watu unaotaka kuwaridhisha na wale ambao upo tayari kuwaudhi.
Jua mapema kabisa wale ambao uko tayari kuwaudhi ili watakapoudhika, wasikuyumbishe.
Pia kwa kujua unaowaudhi, utaweza kujipima vizuri maendeleo yako kulingana na unavyopokea mrejesho wao.

Maisha ni kuchagua,
Waudhi baadhi ya watu ufanikiwe,
Au wafurahishe watu wote na ushindwe.
Mafanikio hayahitaji kila mtu, bali yanahitaji watu sahihi.
Pambania hao sahihi na utaweza kupata matokeo makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr. Makirita Amani
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe